24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

HONGERA WASIMAMIZI MISS TANZANIA KUKATAA ZAWADI ‘KIMEO’

NA CHRISTOPHER MSEKENA


MASHINDANO ya urembo nchini katika ngazi ya kanda yameendelea kufanyika nchini kote tayari kwaajili ya kuwapata washindi watakaowania kinyang’anyiro cha Miss Tanzania ngazi ya Taifa.

Waandaaji wa mashindano hayo katika ngazi ya kanda wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kwenda sawa na malengo ambayo wasimamizi wakuu, Kampuni ya The Look wamejiwekea, ili kurudisha hadhi ya Miss Tanzania.

Tukiwa tunajiandaa kushuhudia washindi kutoka kanda mbalimbali wakitwaa mataji yao leo, Kamati ya Miss Tanzania imekataa zawadi ya gari chakavu aina ya Passo alilotakiwa kupewa mshindi wa Kanda ya Ziwa (Miss Lake Zone 2018).

Kamati hiyo imelazimika kuwaandikia barua waandaaji wa Miss Lake Zone kutafuta zawadi nyingine yenye hadhi ya mashindano hayo na si gari hilo kimeo, ambalo halifanani na mshindi.

Kabla ya kupewa barua, waandaaji wa Miss Lake Zone walilitambulisha gari hilo walilodai lina thamani ya Sh 8,000,000 na lilikuwa tayari kutolewa kwa mshindi wa kanda hiyo atakayeshinda taji usiku wa leo jijini Mwanza.

Huu ni mfano wa kwanza wa makali ya wasimamizi wapya wa mashindano haya makubwa ya urembo nchini, chini ya Mkurugenzi wake, ambaye ni mrembo wa zamani, Basila Mwanukuzi, toka achukue mikoba kwa Hashimu Lundenga.

Itakumbukwa kuwa, moja ya sababu kubwa iliyofanya mashindano hayo yapoteze hadhi yake ni washindi kutopewa zawadi zao au kupewa zawadi ambazo hazina hadhi ya mashindano hayo.

Jambo hilo lilikuwa linawakatisha tamaa warembo waliokuwa wanapoteza muda, nguvu na maarifa yao kushiriki mashindano hayo, ambayo mwisho wake hayaeleweki.

Ndiyo maana Waziri mwenye dhamana na sanaa, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyasimamisha mara kadhaa mashindano hayo na kutaka waandaaji wakabidhi kwanza zawadi zenye hadhi ya Miss Tanzania ofisini kwake kabla hayajafanyika.

Bila shaka kwa hili lililotokea Kanda ya Ziwa litawapa somo waandaaji wa mashindano katika kanda nyingine kufanya mambo yanayoendana na hadhi ya mashindano hayo, ili kuchangia kurudisha hadhi ya Miss Tanzania.

Hongera sana kwa Kamati ya Maandalizi Miss Tanzania kwa kuliona hilo na kuchukua hatua, kwani muda wa kurudisha heshima ya mashindano hayo ni huu na vitu kama zawadi ndiyo zilichangia kuporomosha hadhi ya shindano hilo kwenye jamii.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles