Upendo Mosha, Moshi
Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro, inatarajia kuanzisha utalii wa mnyama aina ya faru kama zao jipya la utalii nchini, hifadhi pekee Tanzania kuwa na Aina ya utali huo
Akizungumza wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa mitaji ya Umma, Kamishna Mkuu wa hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), Alan Kijazi amesema lengo ni kukuza sekta ya utalii nchini.
Amesema hifadhi ya hiyo itakuwa ya kwanza kuwa na utaratibu wa kuona faru weusi ambao walikuwa hatarini kutoweka kabisa na kwamba ni frusa nzuri kwa wageni wote kutoka mataifa mbalimbali kuja na kufanya utalii.
Amesema zaidi miaka 20 hifadhi hiyo ilikuwa na mradi wa uzalishaji faru lengo likiwa Ni kuongeza idadi ya mnyama huyo ambaye alikuwa ametoweka katika maeneo mengi.
Naye Kamishina msaidizi wa hifadhi hiyo, Abel Peter amesema katika kuendeleza utalii nchini hifadhi hiyo itatumia zaidi ya Sh bilioni 3.5 na matarajio ni kuwa na wageni takribani 7,680 kwa mwaka.
Amesema kutokana na uwekezaji huo wanatarajia kuingiza zaidi ya milioni 422.3 kwa mwaka kwani hifadhi hiyo ni sehemu ambayo ina wanyama aina ya faru na vivutio vya aina mbalimbali nyingine za wanyama.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti kamati hiyo ya bunge, Zeynabu valu ametaka Tanapa kutangaza ubunifu uliofanywa na hifadhi ya taifa Mkomazi kwa kumfundisha faru na kumlisha vyakula kama karoti kwa kumuita kwa jina lake la Debora.
Alitaka kutengenezwa kwa video fupi inayoonesha mawasiliano baina ya mtumishi wa Mkomazi na faru Debora ambayo ni nadra kutokea duniani.