Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Heineken Tanzania kwa kushirikiana Lead Foundation wameanza mkakakati wa kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kuoambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuoanda miti ili kurejesha misitu mkoani Dodoma.
Lengo la ushirikiano huo ni kufanya mipango endelevu ya kurejesha misitu iliyoharibiwa na kulinda mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Meneja Heineken Tanzania, Obabiyi Fogade walipotembelea moja ya mradi wa uhifadhi wa mazingira katika Kata ya Mpamantwa, wilayani Bahi, amesema kuna umuhimu wa kulinda mazingira kwa mustakabali endelevu.
Fogade ameeleza kuwa utulivu wa mazingira unasaidia katika mfumo wa ikolojia na viumbe hai, hivyo wameona ni muhimu kushirikiana na Lead Foundation ambayo inahusika na mazingira.
“Mazingira ni muhimu kwetu, bila ya uhifadhi wake, shughuli zetu na jumuiya tunazohudumia zingeweza kuathirika. Ushirikiano huu na Lead Foundation, hasa kupitia mradi wake wa urejeshaji wa miti ya Kisiki Hai, unahusisha mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Arusha,” amesema.
Naye Meneja Biashara na Masoko wa kampuni hiyo, Lilian Pascal, ameunga mkono jitihada hizo kwa kusema ulinzi wa mazingira ni jukumu muhimu kukabiliana na athari mbaya mabadiliko ya hali ya hewa.
“Ahadi yetu ya utunzaji wa mazingira inawiana na wajibu wetu kwa wateja wetu na jamii. Uzalishaji wa bidhaa za Heineken unategemea sana maji, hivyo basi ni muhimu kwetu kuweka kipaumbele katika uhifadhi wa mazingira,” amesema Liliani.
Mkurugenzi wa Miradi wa Taasisi ya Lead Foundation, Njamasi Chiwanga akitoa maelezo kuwa mipango inayoendelea inalenga ufufuaji wa misitu na uvunaji wa maji ya mvua.
Ameeleza kuwa mradi wa ‘Kisiki Hai’ unaolenga kuotesha miti, tayari umepiga hatua kubwa na kufikia zaidi ya vijiji 500 katika mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Arusha.
“Hadi sasa mradi wetu umefanikiwa kulima miti zaidi ya milioni 18 na kushirikisha wananchi zaidi ya 200,000,” amebainisha Chiwanga.
Kwa upande wake mkazi wa eneo hilo, Bosco Malogo amesema wamefurashwa mradi huo kupitia mbinu bunifu kama vile kupanda miti kutoka kwa vishina vilivyo hai.
“Wakazi wameshuhudia manufaa yanayoonekana ikiwa ni pamoja na malisho ya mifugo, matunda ya dawa, na uanzishwaji wa haraka wa misitu kwa gharama ndogo.
“Mradi huu umebadilisha mazingira yetu, kutoa suluhu endelevu ambazo zinanufaisha watu na asili,” amesema Malogo.