NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
MWANAMITINDO Hamisa Mobetto amesema ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond Platinum, kwa takribani miaka tisa hadi sasa.
Mobetto alitoa kauli hiyo Dar es Salaam juzi usiku alipokuwa akihojiwa na Mtangazaji wa Kipindi cha Shilawadu kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds, Soudy Brown, katika hafla ya mtoto wake Abdullatiff, iliyofanyika katika Ukumbi wa King Solomon baada ya Oktoba 5, mwaka huu kumfungulia Diamond kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu upande wa watoto.
“Mwanamke ambaye anakubali kukubebea mimba, mnalea wote mimba miezi tisa mingine hadi 10 halafu mgombane kidogo hakupeleki mahakamani, haijawahi kutokea labda huyo mtu awe hajawahi kukupenda.
“Mtu ambaye nina uhusiano naye takribani miaka tisa na sasa inaingia kumi, siwezi kukurupuka na kusema namfungulia mashtaka,” alisema.
Mobetto alisema Diamond ambaye ni mzazi mwenzake ndiye aliyemshauri kutafuta mwanasheria wa kufungua kesi ya kudai gharama za matumizi ya mtoto wao Abdullatiff au kwa jina jingine Dyallan, ili kumsaidia kupata matunzo na haki za msingi kwa mujibu wa sheria.
Pia alisema kilichotokea hawezi kukiita kesi moja kwa moja isipokuwa ni utaratibu wa kisheria alioufuata ili kutengeneza mazingira yatakayomsaidia mtoto wake kupata haki zake kama watoto wengine wa Diamond.
“Lile lilikuwa ni wazo la baba mwenyewe, kasema anataka kumhudumia mwanaye akaleta mwanasheria wake na mimi akaniomba nilete mwanasheria wangu ikabidi nimtafute, mimi hayo mambo ya sheria nilikuwa siyajui.
“Nadhani aliona siku ya mwisho nitakuwa kama nyumba ndogo na mwanangu anakua, sasa ili mtoto asipate shida yeye kama baba nadhani aliona inabidi amlinde mtoto wake kwa kufuata sheria ambazo zinatamsaidia mtoto kupata haki zake baadaye bila mgogoro wowote,” alisema.
Mobetto alisema hakuna mwanamke anayeweza kukimbilia mahakamani kumshitaki mzazi mwenzake kabla ya kuwa na makubaliano.
“Watu ni lazima waelewe mwanamke hawezi kuinuka moja kwa moja kwenda mahakamani, kuna hatua zinatakiwa zifanyike, mimi nampenda mwanaume hadi nikaamua kuzaa naye na kabla ya kuzaa mnaanza kujadili, mwanaume hapangi kuzaa na mtu kama hayupo tayari, baadaye mnakubaliana wacha tuzae.
Mobetto alidai hawezi kuendelea kulizungumzia suala hilo kwa kuwa tayari lipo mahakamani na alisema hatua iliyofikiwa ilikuwa ni makubaliano baina ya mwanasheria wake na yule wa Diamond na ndiyo maana msanii huyo hajawahi kumlalamikia popote.
Kuhusu utata wa majina ya mtoto wake ambaye kwa sasa anatambulika kwa majina mawili ya Dyallan alilopewa na Diamond na Abdullatiff alilolitoa yeye, alisema majina yote alitoa baba yake.
“Kwanza kabisa mtoto alipewa jina la Abdullatiff na baba yake nikiwa mjamzito, hiyo ni kwa sababu linaendana na la dada yake Latifa, kwa hiyo alipewa hilo na baba yake vitu vikaenda yakatokea yaliyotokea akakataa ujauzito katika mahojiano ya kipindi cha XXL (kinarushwa Redio Clouds FM),” alisema.
Mobetto alisema pamoja na kuikataa mimba kupitia mahojiano ya redio, lakini baada ya kujifungua alimpigia simu na kuagiza mtoto aitwe Abdulatiff.
Alisema jina la Dyallan lilikuja baada ya Diamond kufanya mahojiano ya mara ya pili katika kipindi cha Leo Tena cha Clouds Fm na kumkubali mtoto huyo.
“Aliita Dyallan ili liendane na Nillan, mimi nikawa nishapenda Abdullattiff kwa sababu ni jina lenye nguvu, nikashindwa kubadilisha kwa kuwa hata mimi nina majina mawili naitwa Hamisa na Christina, kwa hiyo sasa nimeamua mwanangu ataitwa DyllanAbdullatif,” alisema.
Alipoulizwa anamzungumziaje Zarina Hassan maarufu kwa jina la Zari ambaye ni mama wa watoto wawili wa Diamond aliyewasili hapa nchini juzi akitokea nyumbani kwake anakoishi Afrika Kusini,
Mobetto alisema haoni haja ya kuendelea na malumbano kwa kuwa sasa hivi watoto wao wameshakuwa ni ndugu.
“Kwa sasa watoto wetu ni ndugu haya yaliyopo ni mapito, natamani tuyamalize, kugombana kupo hata glasi zinagongana katika kabati, ni mapito tu yatapita lakini natumai siku moja tutakuwa pamoja kwa sababu siku ya mwisho mtoto wake ama watoto wake watahitaji kuja kumtembelea ndugu yao ama mwanangu atatoka kwenda kuwaona,” alisema.
Kuhusu fedha za matumizi ambazo Diamond alipohojiwa alidai anampa Sh 70,000 kila siku kuanzia kipindi cha mimba hadi sasa, alisema haiwezekani mwanamume akawa na kiwango kimoja cha fedha cha kumpa mpenzi wake kwa kuwa katika maisha kuna kupata na kukosa.
“Napewa shilingi elfu sabini, kama mtu mzima mwenye akili ukiishi na mpenzi wako au ukiwa na mpenzi wako huwezi kusema kwa siku nampa shilingi laki moja au kiasi kipi, maana kuna siku unaweza ukaamka ukasema leo nina shilingi elfu kumi lakini kikubwa isiwe ndogo wala kubwa,” alisema.
Akitoa msimamo wa uhusiano wake wa kimapenzi na Diamond, Mobetto alisema kwa sasa anaangalia zaidi nafasi aliyonayo kama mama na kufanya jambo litakaloleta tija kwa watoto wake.
“Kumpenda mtu ni kitu kingine kutaka kuendelea naye napo ni kitu kingine, kwa sasa naangalia katika nafasi yangu na watoto kama Mungu amepanga tuwe pamoja basi ni heri,” alisema.
Pia alisema maneno yanayozunguka katika mitandao ya kijamii kuhusu yeye huwa hayamsumbui ila anapata shida wakizungumziwa watoto wake.
Alisema maneno mengi anayozungumziwa ni uongo kwa kuwa wazungumzaji wengi hawamfahamu zaidi ya kumuona mitandaoni.
Katika hatua nyingine, Zari ambaye ni mama wa watoto wawili wa Diamond, alitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na alisisitiza kuwa ujio wake huo haumaanishi kuwa amemfuata Diamond.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili juzi, Zari alisema amekuja nchini kwa ajili ya shughuli ya uzinduzi wa duka la samani la Danube lililopo Mlimani City, Dar es Salaam uliotarajiwa kufanyika jana.