Na Gustafu Haule, Pwani
Diwani Viti maalum katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini, Josephine Gunda (CCM) amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii ikiwa elimu, afya na maji.
Gunda amechaguliwa jana na madiwani waliopo katika kamati hiyo uchaguzi ambao ulifanyika katika Mamlaka ya Mji mdogo Mlandizi ukishuhudiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Vijijini Sozi Ngate.
Nafasi ya Gunda imekuja baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Erasto Makala kuunda majina ya kamati mbalimbali ambapo katika kamati ya huduma za afya, elimu maji waliteuliwa madiwani nane.
Aidha, madiwani waliounda kamati hiyo ni pamoja na Sangaine Tikwa Mwajuma Denge, Godfrey Mwafulilwa, Josephine Gunda, Habiba Mfaramagoha, Ramadhani Hussein, Rehema Jongo na Abdallah Kiddo.
Hata hivyo mbali na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo lakini pia Gunda ameteuliwa katika kamati ya maadili ambayo na kwamba hatua hiyo inampata fursa ya kuingia moja kwa moja katika kamati ya fedha na mipango.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo Gunda, amesema anawashukuru madiwani wenzake kwa kumuamini na kwamba ataiongoza kamati hiyo kwa kufuata kanuni,sheria na taratibu zilizopangwa.
Gunda amewaomba madiwani hao kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha wanapigania maendeleo ya Halmashauri na hasa katika kutatua changamoto za wananchi wao.