Na MWANDISHI WETU
KITENDO cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, kuripotiwa na gazeti la MTANZANIA la jana kuwa ameanza kufanya kazi katika duka kubwa (supermarket) huko nchini Canada, kimeibua mjadala mkubwa miongoni mwa jamii.
Ndani ya mjadala huo yameibuka makundi mawili, la kwanza linaloshangazwa na la pili ambalo linauona uamuzi wake huo kama ni jambo la kawaida, hasa katika nchi zilizoendelea.
Kundi la kwanza limeeleza kutoamini mwanasiasa huyo ambaye alikuwa na hadhi ya juu hapa nchini, akipata kuwa mbunge wa Jimbo la Karatu kwa takribani miaka 15 na baadaye mwaka 2010 kugombea urais, kufika katika kiwango hicho cha maisha.
Kundi hilo limekwenda mbali na hata kuhofu juu ya umri wake wa miaka 69, kwamba anatakiwa kupata muda mwingi wa kupumzika, lakini yeye ameamua kujiingiza katika maisha ya kufanya kazi kwa saa.
Mjadala huo, ambao sehemu kubwa umetawala katika mitandao ya kijamii, umewavuta wengi, huku baadhi wakijenga hisia kwamba, pengine uamuzi wake huo umetokana na ugumu si tu wa maisha, bali wa ajira nchini Canada.
Kwa mujibu ya tovuti ya Trading Economics ya Canada, takwimu za mwezi Oktoba zinaonyesha kuwa, nchi hiyo ilikuwa na wastani wa upungufu wa ajira wa asilimia 6.3.
Kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 0.1 kutoka kiwango cha mwezi Septemba, ambao ulikuwa na wastani wa ukosefu wa ajira wa asilimia 6.2.
Pia mtandao huo umetanabahisha kwamba, kiwango cha kuajiriwa kimeongezeka zaidi katika kundi la vijana ambao wengi wameingia kwenye ajira za masoko kama kazi anayofanya Dk. Slaa kwa sasa.
Taarifa mpya ya tovuti hiyo inaeleza kuwa, ajira za ndani ya taifa hilo lenye watu takribani milioni 35 imeongezeka kwa kiwango cha asilimia 0.2, kwa maana ya ongezeko la watu elfu 35 katika kundi la watu walioajiriwa ambao idadi yao ni milioni 18.489.
Mtandao huo umefafanua kwamba, sehemu kubwa ya watu walioajiriwa wamepewa mikataba ya kudumu na wachache ndio wana ajira za muda mfupi.
Watu wenye uzoefu na maisha katika nchi za Dunia ya Kwanza na ambao kimsingi katika mjadala huu wanaunda kundi la pili wameeleza kutoshangazwa na uamuzi huo wa Dk. Slaa, wakisema si kitu kigeni kwa msomi kama yeye kufanya kazi hiyo.
Pamoja na hayo, katikati ya mjadala mzima, yumo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, ambaye amemwelezea Dk. Slaa kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kubadilika kulingana na mazingira.
Profesa Baregu anasema Dk. Slaa ametoka kwenye upadri, akaingia ubunge na baadaye akawa katibu kkuu wa chama cha siasa.
“Ukiangalia maisha yake binafsi katoka upadri ambao hauruhusiwi kuoa, akaoa mke mmoja akamwacha akaoa mke mwingine, kwa hiyo ni mtu ambaye ninaweza kusema ana uwezo mkubwa kubadilika kutokana na mazingira.
“Lakini sijui alikuwa na malengo gani wakati anaingia kwenye siasa, pia sijui alikuwa na malengo gani alipokuwa anajiuzulu ukatibu mkuu wa Chadema. Pamoja na kwamba alisema amesutwa na nafsi yake kuhusu uteuzi wa Lowassa, lakini yale mengine ambayo yalimfuata na kwenda kujikuta yuko Canada sijui kama alikuwa ameyaona mbele yake,” alisema.
Profesa Baregu alisema kwamba, wakati mwingine anafikiri Dk. Slaa anajuta kwa kiasi fulani, kwa sababu wapo waliokuwa naye kwa kufanya maamuzi magumu, lakini yeye akaonekana si mtu mwepesi wa kufanya maamuzi magumu.
Alisema maamuzi magumu ukiyafanya huna budi kuyasimamia kikamilifu, kwa sababu alikuwapo hadi uamuzi wa mwisho wa kumtangaza Lowassa kuwa mgombea, lakini baadaye akashindwa kusimamia alichokiamua.
“Unajua hakuna mtu aliyetegemea Dk. Slaa angekuwapo hapo alipo, kwamba amekwenda kufanya kazi ya duka, sijui kama ni ya muda au kudumu, lakini sijui kama ni maisha magumu ya kule. Hata hivyo, inaonekana wazi kama angekuwa ni mtu mwenye uwezo wa msimamo, labda asingekuwa huko alikofika.
“Sitaki kuyaingilia maisha yake binafsi, lakini ndio hivyo, sasa mtu mwingine anaweza akasema ana udhaifu katika kusimamia yale aliyoyaamua, kwa maana hiyo, labda kesho tutamkuta kwenye ofisi nyingine kwa kitu cha muda au kudumu.
“Hatujui kwa sababu tumeona leo kawa padri, akawa mbunge, inawezekana labda kapenda kazi ya kuwa muuza duka kwa sababu ni mtu wa kujaribu vitu vingi.
“Inawezekana kaamua kufanya hivyo, labda kaona ni kitu cha maana sana,” alisema Profesa Baregu.
Wakati mjadala ukiendelea katika mitandao ya kijamii, MTANZANIA Jumamosi, katika uchambuzi wake limebaini kuwa ujira wa Dola za Marekani 10 (Sh 22,290) kwa saa ambazo Dk. Slaa mwenyewe ameeleza kulipwa kama Mshauri wa Mauzo wa Supermarket ya Costco ya nchini Canada, kwa mwezi hayawezi kufikia kiwango cha mshahara na marupurupu yake aliyokuwa akilipwa ndani ya Chadema.
Inaelezwa kwamba, hadi Dk. Slaa anaondoka ndani ya chama hicho alikuwa akilipwa mshahara wa Sh milioni 13.8 kwa mwezi, kiwango ambacho kilitajwa kuwa ni kikubwa kuliko makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa katika nchi za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa mchanganuo wa mshahara wake, ambao ulishawahi kunukuliwa kwenye vyombo vya habari miaka miwili nyuma, unatanabahisha kwamba, alikuwa analipwa na Chadema mshahara kwa mwezi wa Sh milioni 9.3, fedha ya usafiri Sh milioni mbili na fedha za matumizi ya ofisi Sh milioni 2.5.
Kama haitoshi, inadaiwa kwamba, Dk. Slaa alikuwa analipwa posho ya Sh milioni 1.5 katika kila kikao.
Ujira wa Dola 10 (Sh 22,290) kwa saa, anaolipwa sasa, endapo kazi hiyo ataifanya kwa saa nane kwa siku na kwa mwezi mzima, atakuwa anapokea Sh milioni 5.3.
Kiwango hicho kinaweza kuwa pungufu au kikubwa, hasa kutokana na ukweli kwamba, Dk. Slaa mwenyewe, licha ya kukiri kufanya kazi kwa mikono yake zaidi ya moja, lakini hakuweka wazi kiwango cha fedha anazolipwa kwenye kazi hizo nyingine.
Dk. Slaa, ambaye amepata kuwa padri wa Kanisa Katoliki kabla ya kuingia kwenye siasa na kuwa mbunge, mgombea urais na katibu mkuu wa Chadema, aliliambia gazeti la MTANZANIA la jana kuwa, duka kubwa ‘Supermarket” anayofanya kazi kwa sasa lina hadhi kama yalivyo maduka ya Nakumat, Shoppers na Imalaseko.
Katika maelezo yake kwa gazeti hilo, Dk. Slaa alisema kuwa, kwa sasa anaishi kwa kazi ya mikono yake, kwani ili aweze kuishi anahitaji kufanya kazi zaidi ya mbili hadi nne kwa siku.
“Niko ninafuatilia matukio Mutukula (ziara ya Rais Dk. Magufuli). Siku zote nimesema ninaishi kwa jasho na kazi ya mikono yangu. Canada ili uishi vizuri unahitaji kazi zaidi ya mbili au tatu mpaka nne. Hayo nimeweka wazi, sijui jambo jipya kama mtu alikuwa hafuatilii.
“Mimi ninafanya kazi PWD/CDS/ COSCO kama Sales Advisor, baada ya kumaliza masomo yangu, hasa Interpersonal Communication. Cotsco ninakofanya kazi ina wanachama (Members 10,000). Kwa siku wanaofika warehouse ni kati ya 5,000 hadi 7,000,” alisema Dk. Slaa.
Mbali na hilo, alisema kuwa, pia anafanya kazi nyingine, ikiwa ni pamoja na ushauri (consultancy).
Alisema kila mara amekuwa akiwataka Watanzania na vijana wafanye kazi, kwani fedha haziji kwa kukesha kwenye mitandao wala propaganda.
“Canada ni kazi, Profesa wa Chuo Kikuu anafanya kazi ya Uber (sijui kama Uber inafahamika Tanzania, dereva taxi kwa kutumia gari lake binafsi). Ofisa wa Serikali usiku anaosha vyombo hotelini.
“Ndiyo maana familia ina magari mawili au zaidi, TV, nyumba ya kisasa, chakula cha kisasa. Wanatekeleza sera ya Hapa Kazi Tu kwa matendo. Nadhani nimekupa taarifa za kutosha, ikiwa ni pamoja na kujibu ya propaganda kuwa nilihongwa mabilioni.
“…niwahakikishie tena, wakati wa kusoma nilikuwa na scholarship, tangu nianze kazi ninaishi kwa jasho la mikono yangu. Mke wangu yeye ameingia Chuo Kikuu cha York baada ya diploma yake na bado anapata scholarship.
“Ndiyo maana tuna uwezo wa kuwa na magari mawili aina ya Jeep na Dodge, ukifanya kazi utaishi vizuri. Hii ni pamoja na kugharimiwa bima ya afya (Health Insurance), watoto kusomeshwa na Serikali ya Canada,” alikaririwa Dk. Slaa katika gazeti la MTANZANIA la jana.