MANCHESTER, ENGLAND
KOCHA wa vinara wa Ligi Kuu nchini England, Manchester City, Pep Guardiola, amewataka wachezaji wa timu huyo kutumia muda wao kujifunza Kiingereza ili waweze kuelewana zaidi wakiwa uwanjani.
Kikosi cha kwanza cha Manchester City wachezaji wake wote wanatoka mataifa tofauti, lakini wengi wao wanajua kuongea Kihispania na Kireno, lakini kocha huyo amewataka wachezaji hao kujifunza Kiingereza ambayo ni lugha rahisi kwa mawasiliano.
Hivyo kocha huyo amewapangia utaratibu wachezaji wake kwamba kila baada ya mchezo wa nyumbani lazima wakutane na kula chakula pamoja ili kuwafanya wachezaji ambao hawajui Kiingereza waweze kujua kupitia wenzao.
Hata hivyo, nyota wa klabu hiyo ambaye anacheza nafasi ya ulinzi, Nicolas Otamendi, ameweka wazi kuwa Desemba mwaka huu anatarajia kurudi darasani kwa ajili ya kufanya mtihani wa Kiingereza.
“Guardiola ametuwekea ratiba ya kukutana na kula pamoja mara baada ya kucheza mchezo wa nyumbani, hivyo tunatumia muda mwingi kujifunza Kiingereza tukiwa pamoja. Kwa upande wangu Desemba mwaka huu nitakuwa na mtihani wa Kiingereza,” alisema Otamendi.
Hata hivyo, beki huyo raia wa nchini Argentina, alizidi kummwagia sifa kocha huyo kwa kudai kwamba anazifanya familia za wachezaji kuwa pamoja.
“Guardiola ni kocha wa aina yake, ana uwezo mkubwa wa kufundisha na tunakuwa hatuna wasiwasi siku ya mchezo wetu kwa kuwa anatuandaa vizuri kuelekea mchezo huo.
“Hata nje ya uwanja kocha huyo anazifanya familia zetu kuwa pamoja, lakini kitu ambacho anakichukia katika maandalizi ya mchezo ni kuleta utani, hivyo kocha huyo anatufanya wachezaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu,” aliongeza Otamendi.
Manchester City kwa sasa inaongoza katika msimamo wa ligi ikiwa na jumla ya pointi 22 ikifuatiwa na wapinzani wake Manchester United wenye pointi 20 baada ya kucheza michezo nane na nafasi ya tatu ikichukuliwa na Tottenham, wenye pointi 17.