Na Walter Mguluchuma- Sumbawanga
JESHI la Polisi Mkoa wa Rukwa linamshikilia Diwani wa Kata ya Izia (Chadema), Pascal Silwimba (41) na mkewe Dorisi Karugu (36) kwa kukutwa na gobole na robo kilo za dawa za kulevya aina ya bangi wakiwa wamehifadhi ndani ya duka lao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi katika eneo la Soko Kuu la Manispaa ya Sumbawanga.
Alisema Pascal na mkewe walikamatwa kutokana na msako walioufanya baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa watu hao wanamiliki silaha kinyume cha sheria na pia wamekuwa wakijihusisha na biashara ya kuuza bangi.
Kyando alisema baada ya taarifa hizo kuwafikia walianza kufanya uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo na baada ya uchunguzi kufanyika waliamua kufanya msako katika eneo hilo.
Alisema baada ya kufanya uchunguzi huo, walifika dukani kwa Pascal na walipekua ndani ya duka hilo walilokuwa wakiuza mifuko ya salfeti na walikuta gobole hilo na bangi zikiwa zimehifadhiwa katikati ya mifuko hiyo.
Alisema baada ya kukamatwa na vitu hivyo dukani mwao walihojiwa na kukiri  kuvimiliki. Kyando alisema upelelezi wa tukio hilo umekamilika na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
HONGERA TASAF KUTOWA MALIPO KWA MTANDAO.