Na MWANDISHI WETU
WAKAZI wa Mkoa wa Tanga wapo tayari kuwashuhudia wasanii wanaowapenda leo katika tamasha la burudani la Tigo Fiesta, litakalofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani, mjini hapa.
Msanii Gigy Money, anayetamba na wimbo wake wa ‘Nampa Papa’, anaingia kwa mara ya kwanza katika jukwaa la Tigo Fiesta, kutokana na kuwa gumzo na wimbo wake huo.
Licha ya Gigy Money, wengine ni Roma Mkatoliki na Stamina, ambao wanatamba na wimbo wao wa ‘Hivi ama Vile’, wakisubiriwa kunogesha tamasha hilo kwa wakazi wa Tanga.
Wasanii hao wamekuwa wakifanya vema katika mikoa yote ya Tigo Fiesta waliyopanda jukwaani tangu tamasha hilo lilipozinduliwa kutokana na wimbo wao huo.
Licha ya wasanii hao, wengine watakaopanda jukwaani katika tamasha hilo lenye kauli mbiu ya ‘Tumekusoma’ ni Mavocal, Chege, Nandy, Maua Sama.
Wengine ni Vanessa Mdee, Jux, Ben Pol, Aslay, Weusi, Darassa, Lulu Diva, Zaiid, Mimi Mars, OMG, Bright na Nchama.
Akizungumzia tamasha hilo, Jumaa Zecha, mkazi wa Chumbageni, alisema kuwa, tayari amenunua tiketi yake kwa ajili ya kuwashuhudia Gigy Money, Roma Mkatoliki na Stamina, kwa kuwa ni miongoni mwa wasanii anaowapenda.
“Mimi kwa kweli sitokosa kwenye Tigo Fiesta Ijumaa na hapa ninapozungumza tayari nimenunua tiketi yangu kwa Tigopesa ili niweze kushuhudia burudani,” alisema.
Naye Mwanasha Ally, mkazi wa Makorora, alisema haoni sababu ya kukosa kushuhudia Tigo Fiesta na kwamba faraja yake ni kuwaona wasanii anaowapenda, kama Gigy Money, Roma, Stamina na Vanessa Mdee.
Meneja wa Tigo Kanda ya Kati, John Tungaraza, alisema maandalizi yamekamilika na wanachosubiri ni kushuhudia Tigo Fiesta ikifanyika kwa mafanikio zaidi, ikilinganishwa na mwaka jana.
Alisema kuwa, wasanii wapo tayari kwa ajili ya kuwapatia burudani wakazi wa Tanga na wanaamini kila kitu kitakwenda sawa, kwa kuwa wamejipanga ipasavyo.
“Maandalizi yamekamilika na mashabiki wa burudani na wateja wa Tigo wakae mkao wa kula, chakula kwa maana ya burudani iko tayari, nitumie fursa hii kuwakaribisha tujumuike na kufurahi pamoja, huku tukifurahia huduma bora kutoka Tigo.
“Tumejipanga vizuri kwa ajili ya Tigo Fiesta Tanga, mwaka jana tulipata mashabiki wengi na mwaka huu tunatarajia watazidi kutokana na hamasa ya wasanii waliyotoa tangu wamefika hapa Tanga, matumaini yetu wasanii hawa wataacha simulizi ili mwakani waone tena burudani hii, tiketi bado zinauzwa na ni vizuri wakanunua kwa Tigopesa ili wapate punguzo,” alisema.
Alisema kuwa, wakazi wa Tanga hawajawahi kuwaangusha na ndiyo maana Tigo Fiesta mwaka huu imekuja tena na hata mwakani wana imani itakuja tena, kutokana na kupokelewa kwa shangwe na hata kufanya vizuri kwa huduma mbalimbali.
“Tigo Fiesta 2017 kama ilivyo kauli mbiu yetu ‘Tumekusomaa’ tunazidi kuwajali wateja wetu na ndiyo maana tunawasikiliza na kuwapa kile wanachokipenda, ikiwamo burudani kama hii ya kuwashuhudia wasanii wao wanaowapenda,” alisema.