Na MWANDISHI WETU
MSANII wa Bongo Fleva, Gigy Money, anayetamba na wimbo wake wa ‘Nampa Papa’, ni miongoni mwa wasanii watakaopanda jukwaani katika tamasha la Tigo Fiesta, litakalofanyika Ijumaa katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Msanii huyo, ambaye alikuwa ‘Video Queen’, kwa mara ya kwanza ametajwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaopanda katika jukwaa la Tigo Fiesta jijini Tanga, kutokana na kujizolea umaarufu katika muziki wa Bongo fleva.
Mbali na Gigy Money, wasanii wengine watakaopagawisha Tigo Fiesta Tanga ni Mavocal, Chege, Nandy, Maua Sama.
Wengine ni Vanessa Mdee, Jux, Ben Pol, Aslay, Rostam, Weusi, Darassa, Lulu Diva, Zaiid, Mimi Mars, OMG, Bright na Nchama.
Meneja wa Tigo, wanaodhamini tamasha hilo, William Mpinga, alisema kuwa, hadi sasa tamasha hilo limekuwa burudani tosha kwa mashabiki wa miziki wa Bongo fleva na kwamba wao wataendelea kuwajali wateja wao kwa kuwapa ofa mbalimbali, lakini pia burudani.
“Tigo Fiesta 2017 kama ilivyo kauli mbiu yetu ‘Tumekusoma’, tunazidi kuwajali wateja wetu na ndiyo maana tunawasikiliza na kuwapa kile wanachokipenda, ikiwamo burudani kama hii ya kuwashuhudia wasanii wao wanaowapenda,” alisema.