26 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

GGML watoa magodoro 50 kwa Kituo cha Wazee Bukumbi

Na Mwandishi wetu Mtanzania Digital

KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali kuwajali na kuboresha maisha ya wazee nchini, Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu Geita (GGML) imetoa msaada wa magodoro 50 kwa Kituo cha Wazee Bukumbi kilichopo mkoani Mwanza.

Sehemu ya wazee wa Kituo cha Wazee cha Bukumbi wakisubiri msaada wa GGML.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo jana mkoani Mwanza, Ofisa Mwandamizi wa Mahusiano ya Jamii kutoka GGML, Shunashu Musa alieleza kuwa msaada huo unalenga kuboresha makazi bora na hali ya maisha ya wazee wanaoishi katika kituo hicho.

Aliongeza kuwa baadhi ya wafanyakazi wa GGML na wenzao wamekuwa wakisaidia kituo hicho kwa nyakati tofauti na kuchangia baadhi ya vifaa vya matumizi. Kipindi hiki menejimenti ya kampuni hiyo imeamua kusaidia kituo hicho kwa kuchangia uboreshaji wa vyumba vya kulala vya wazee hao.

“Tulipokea ombi la kufikiria kusaidia kituo hiki kwa njia mbalimbali. Tunafahamu kituo hicho kilianzishwa miaka mingi iliyopita hivyo baadhi ya miundombinu na vifaa vinahitaji maboresho ndiyo maana uongozi uliamua kuchangia magodoro 50.

“Kama sehemu ya AngloGold Ashanti, moja ya maadili ya biashara ya GGML ni kwamba jumuiya na jamii tunakofanyia kazi lazima ziwe na maisha bora. Tunatumaini magodoro haya yataboresha maisha ya wazee zaidi ya 50 wanaoishi hapa,” amesema.

Aidha, Msimamizi wa Kituo cha Wazee cha Bukumbi, Jonas Tarimo alishukuru GGML kwa msaada huo na kuongeza kuwa utasaidia kutoa huduma za malazi bora na salama kwa wazee wa kituo hicho.

“Hiki ndicho kituo pekee cha kuishi wazee kilichopo karibu na mikoa ya Geita na Mwanza. Tumebahatika kuungwa mkono na Mgodi wa Dhahabu wa Geita ndio maana tunaona wakazi wengi wanafurahia msaada huu,” amesema Tarimo.

GGML imekuwa kinara wa uwekezaji katika jamii tangu ilipoanzishwa mwaka 2000, huku vipaumbele vikubwa vikiwa ni miradi ya afya, elimu, maji, barabara, miradi ya maendeleo na miradi mingine ya kijamii inayolenga kuboresha ustawi wa jamii inayowapokea.

Mapema mwaka huu, Kampuni ilitangazwa kuwa mshindi wa jumla wa makampuni yaliyofanya vyema katika sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka wa 2020/2021 baada ya kushinda tuzo za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipakodi bora na maudhui ya ndani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles