MONROVIA, LIBERIA
TUME ya Uchaguzi nchini Liberia imetangaza kuwa mwanasoka wa zamani barani Afrika, George Weah, ameshinda uchaguzi kuwa Rais wa Liberia baada ya kuongoza kwa asilimia 61.5 kati ya kura asilimia 98.1 zilizohesabiwa.
Weah amemtangulia mpinzani wake Joseph Boakai kwa kura asilimia 60 na anatarajiwa kuchukua nafasi ya mwanamke wa kwanza Afrika kuwa rais, Ellen Johnson Sirleaf anayemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo na ambaye pia ni mshindi Nobel. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo kupata kiongozi kwa njia ya kidemokrasia.
Baada ya kutangazwa ushindi huo furaha na shangwe zimesikika katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Monrovia na maeneo mengine nchini Liberia kwa ujumla tangu mchezaji nyota wa zamani wa soka ulimwenguni atangazwe   kuwa rais.
Mara baada ya habari kuhusu ushindi wa George Weah kutangazwa, maelfu kwa maelfu ambao tayari walikuwa wamejazana pembezoni mwa makao makuu ya Tume ya Uchaguzi, waliteremka njiani na kuanza kushangilia.
“Weah Weah, tutaandika historia,” ni miongoni mwa matamshi yaliyosikika mjini humo.
Liberia, nchi iliyoundwa na watumwa walioachiwa huru nchini Marekani, inaingia katika utaratibu wa kwanza wa kubadilishana madaraka kwa njia za kidemokrasia katika kipindi cha zaidi ya miaka 70, baada ya rais wa kwanza mwanamke, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Ellen Johnson Sirleaf, kustaafu.
George Weah mwenye umri wa miaka 51, Seneta aliyeingia katika uwanja wa kisiasa baada ya kustaafu katika viwanja vya soka mwaka 2002, aliongoza duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais ulioitishwa Oktoba mwaka huu, lakini hakufikia wingi wa kutosha wa kura dhidi ya mpinzani wake Boakai mwenye umri wa miaka 73 ambaye ametumikia wadhifa wa makamu wa rais kwa kipindi cha miaka 12. Sirleaf hakumuunga mkono mgombea yeyote yule kati ya hao wawili.
Msemaji wa Chama cha Boakai, Unity Party, Mohammed Ali, amekiambia kituo cha matangazo cha Capital FM kwamba chama chao hakitatuma malalamiko mahakamani kwa    sababu wananchi walio wengi wa Liberia wameshaamua.
Rais mpya George Weah anatazamiwa kukabidhiwa hatamu za uongozi  Januari mwakani.
“Tumesubiri miaka 12, sasa madaraka yanawarejea wananchi,” amesema Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa vijana na mmojawapo wa washirika katika muungano wa upinzani unaoongozwa na George Weah, Seneta Jewel Howard-Taylor, mke wa zamani wa kiongozi wa zamani wa waasi na rais wa zamani anayeshikiliwa jela, Charles Taylor.
Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi huo wamesema zoezi la uchaguzi lilikuwa la haki na huru.