BEIJING, CHINA
GAZETI linalochapishwa na Chama cha Kikomunisti nchini hapa, Global Times, limetoa onyo kwa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, likisema China ‘italipa kisasi’ iwapo atavunja sera ya China-Moja.
Ujumbe huo umekuja saa chache tu baada ya Rais wa Taiwan, Tsai Ing-wen kukutana na wabunge waandamizi wa Chama cha Republican wakati alipotua kwa muda mjini Houston akiwa njiani kwenda Amerika ya Kati, ambako atazuru Honduras, Nicaragua, Guatemala na El Salvador.
Beijing imeitaka Washington kutomruhusu Tsai kuingia Marekani na kuwa hapaswi kuwa na mkutano wowote rasmi chini ya sera ya China-Moja.
“Kuheshimu msingi (China-moja) si ombi lenye kubadilika kwa marais wa Marekani, bali wajibu kwa marais hao kuheshimu uhusiano wa China na Marekani na kuheshimu utaratibu uliopo Asia-Pasifiki,” tahariri ya Global Times ilisomeka.
Sera hiyo ya China-Moja ilianzishwa mwaka 1979 na Rais wa Marekani, Jimmy Carter kutambua kwamba Taiwan ni sehemu ya China.
Trump ambaye mara kadhaa huko nyuma alisema kwamba hajisikii kufungwa na sera hiyo, aliikasirisha China mwezi uliopita kwa kukubali kupokea simu ya pongezi kutoka kwa Tsai.
Hata hivyo, katika mahojiano ya Desemba mwaka jana, ambayo Trump aliiambia Fox News kuwa hajisikii kufungwa na sera hiyo, pia alisema hatakutana na Tsai.
China ina wasiwasi kwamba Tsai yu katika harakati za kuhakikisha uhuru wa Taiwan, kisiwa kinachojitawala ambacho Beijing inakihesabu kama jimbo lake lililoasi.