Mwandishi Wetu, Dodoma
Faru maarufu anayejulikana kwa jina la Fausta amezua gumzo bungeni baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Suzana Mgonokulima, kuhoji ni kwa nini serikali inamhudumia faru huyo kwa gharama kubwa wakati hazalishi kutokana na kuwa mzee.
“Serikali inamhudumia Faru Fausta kwa gharama ya Sh milioni 64 kwa mwezi, lakini serikali haiwezi kuhudumia mwananchi aliyezeeka ambaye hawezi kufanya shughuli yoyote ya kujikimu na maisha na hana mtu wa kumsaidia, je ni kipi muhimu zaidi kati ya Faru Fausta au mwananchi mzee asiyeweza kufanya lolote na hana wa kumsaidia,” amehoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema faru huyo amekuwapo katika Hifadhi ya Ngorobgoro tangu mwaka 1965 ambapo kwa sasa ndiye faru mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani.
“Kutokana na uzee, Faru Fausta alijeruhiwa na fisi Septemba mwaka juzi, hivyo kulazimu atunzwe kwenye kizimba kwa ajili ya uangalizi maalumu ambao unahusisha matibabu na chakula, hivyo gharama iliyokuwapo kipindi hicho ilitokana na hali ya dharura iliyohitajika ikiwamo miundombinu, ulinzi, matibabu na malisho ambayo matumizi yote hayo kwa mwezi yalikuwa Sh milioni 1.4 kwa sasa hali yake inazidi kuimarika na gharama imepungua hadi Sh 285,000 kwa mwezi.
“Hata hivyo, faru huyo si kwamba ni muhimu kuliko wazee bali uamuzi wa kumtunza kwenye kizimba ulifanyika kwa lengo la kunusuru maisha yake ili aendelee kuwa kivutio cha utalii na kuingiza fedha za kigeni nchini,” amesema.
Hata hivyo, majibu hayo hayakumridhisha mbunge suzana ambaye katika swali lake la nyongeza alihoji tena umuhimu wa faru huyo ambaye hata hivyo amefungiwa watalii watamuonaje na kwamba umuhimu wake ni zaidi ya wazee waliopigania nchi na kuleta amani lakini hawatunzwi na serikali.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Hasunga amesema faru huyo anahifadhiwa kutokana na umuhimu wake na jinsi alivyoliingizia taifa fedha nyingi za kigeni na wengi wanataka kujua ataishi miaka mingapi ambapo sasa hivi ana miaka 53.
Hata hivyo, hali hiyo ilimuibua Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile ambaye amesema kwa mujibu wa sera ya afya serikali inatambua wazee ambapo imeweka utaratibu wazee zaidi ya miaka 60 wanapata matibabu na wanapata kipaumbele kwenye huduma ya afya ambapo mapato yanayopatikana katika Sekta ya Utalii ndiyo hayo hayo yanakwenda kuhudumia wazee hao.