31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YA LISSU: TUPO GIZANI

*Yamshukia IGP Sirro, yasema itanyamaza iwapo waliompiga ngugu yao watakamatwa

*Yakumbushia yaliyotokea kwa marehemu Barlow, yaeleza walichojibiwa na AG

Na ABRAHAM GWANDU-ARUSHA


MWANASHERIA Alute Mughwai, ambaye ni kaka mkubwa wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amesema familia hiyo ipo gizani juu ya upelelezi wa tukio la ndugu yao kupigwa risasi, huku akieleza  kushangazwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kutaka mjadala wa jambo hilo ufungwe.

Sirro alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwashangaa waandishi wa habari na watu wengine ambao wamekuwa wakimuuliza tukio la Lissu na kusema tukio hilo ni la kawaida kama yalivyo matukio mengine.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Mughwai alisema. “Familia iko gizani haijui kinachoendelea katika upelelezi sasa tunanyamaza vipi? Tuwe tunapata taarifa za hatua zilizofikiwa katika upelelezi ili tusipige kelele,” alisema.

Alisema kauli ya IGP Sirro  kuwa tukio la kushambuliwa kwa Lissu ni sawa sawa na matukio mengine ni ushahidi kuwa polisi imezidiwa  na ndiyo maana familia imeomba uchunguzi usaidiwe na vyombo kutoka nje.

“Ni kweli matukio ya kushambuliwa na kuumizwa hata kuuwawa watu kwa kutumia risasi  yapo mengi ndio maana sisi kama familia tunasema kama wamezidiwa na kazi kwa hili la ndugu yetu waruhusu wachunguzi kutoka nje ya nchi.

“Anapodai kuwa ni tukio la kawaida analinganisha na tukio lipi ambalo kiongozi wa umma alishambuliwa hadharani kama Lissu? Kama ni lile la RPC wa Mwanza (marehemu Liberatus Barlow), pamoja na kwamba alishambuliwa usiku, mbona waliohusika walikamatwa kesho yake na sasa wako mahakamani? Kwanini hili la mchana kweupe hatuambiwi kinachoendelea?

“Familia itanyamaza pale ambapo wahalifu waliokusudia kumuua Lissu na wale wote waliohusika kupanga njama hizo watakapotiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani

“Sisi hatumfundishi kazi (Sirro) lakini Polisi ni chombo cha Serikali na Katiba yetu Ibara 8 (1) (c ) inaeleza serikali itakavyo wajibika kwa wananchi na sisi ni sehemu ya wananchi wa Tanzania” alieleza.

Mughwai alisema badala ya IGP Sirro kupuuza ushauri wa watu, yeye kama mtumishi wa umma angeupokea hata kama hatoufanyia kazi badala ya kukataza watu kusema kwa madai kuwa wanakifundisha kazi chombo hicho.

Alisema iwapo familia ingekuwa inapata taarifa za hatua zilizofikiwa katika upelelezi, kusingekuwa na malumbano yoyote na akashangaa polisi kutowajulisha waathirika wa tukio hilo hasa familia hatua iliyofikiwa mpaka sasa zaidi ya amri na makatazo ya IGP Sirro.

“Matarajio yetu badala ya kusema asifundishwe kazi angesema tu kwa unyenyekevu kuwa amepokea ushauri ataufanyia kazi au laa,” alisema Mughwai.

Alisema njia pekee ni kwa Sirro kuacha upelelezi wa kwenye vyombo vya habari na badala yake afanye kazi yake kwa weledi, haki na kwa haraka.

“Hatuwezi kukaa kimya kama familia, nasema sijui kama IGP alinukuliwa vizuri lakini hawezi kutunyamazisha kuhusu sula la kushambuliwa kwa Lissu.

“Njia pekee ni yeye kuacha malumbano ya kwenye vyombo vya habari kwa kufanya upelelezi unaojitosheleza, wenye matokeo yenye tija na kwa haraka,” alisema.

Majibu ya Barua ya AG

Kuhusu barua ambayo familia hiyo ilimuandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuomba upelelezi wa tukio la Lissu kupigwa risasi ufanywe na vyombo kutoka nje ya nchi, alisema mawasiliano kati yao na Serikali yanaendelea vizuri kiasi cha kuonyesha matumaini ya ndugu yao kupata haki.

Mughwai alikiri kupokea barua kutoka kwa AG yenye majibu ya barua yao ya awali yenye ujumbe wa familia kuhusu namna suala la kushambuliwa kwa ndugu yao linavyoshughulikiwa na vyombo vinavyohusika.

Alisema hivi sasa familia hiyo isingependa kuendelea na utaratibu wa kujibizana na Serikali kupitia vyombo vya habari na badala yake wameanza kutumia utaratibu wa kuwasiliana.

Huku akimwonesha mwandishi wa gazeti hili faili lenye barua ya AG na ambayo Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwaandikia akiomba kukutana nayo, Mughwai alisema kwa sasa familia inavipa nafasi vyombo vinavyohusika vifanye kazi.

“Ni kweli majibu ya barua yetu ambayo tulimwandikia AG tumeyapata na ieleweke sisi tuliandika barua tatu moja kwenda kwa mwanasheria mkuu, nyingine kwa waziri wa sheria na nyingine kwa Spika chombo ambacho ndugu yetu ni mtumishi akiwakilisha wananchi wa Singida Mashariki.

“Siwezi kukuruhusu ukasoma maudhui yote yaliyoko kwenye barua hizi, kama unavyo ona ina muhuri wa siri ni ‘confidential’. Hata barua ya Spika kutaka kuonana na familia hii hapa pia sisi hatukujipeleka kwenda kuonana nao, kwa ujumla familia inawapa nafasi ili Serikali iweze kufanyia kazi yale tuliyohoji kwenye barua yetu.

“Pamoja na kwamba hivi sasa ninapozungumza na wewe natumia chombo cha habari lakini tusingependa kuendelea na utaratibu huu wa kuzungumzia kinachoendelea katika mawasiliano yetu na Serikali mpaka hapo tutakapokwama kwa njia hii au hata tukifanikiwa tutawajulisha umma,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles