25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu ya majanga itolewe kuepusha maafa

4

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

SEPTEMBA 10, mwaka huu lilitokea tukio la tetemeko la ardhi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kusababisha madhara Mkoa wa Kagera hasa Manispaa ya Bukoba Mjini.

Katika tukio hilo hadi kufikia jana watu  16 walifariki na 253 kujeruhiwa.

Tetemeko hilo pia limesababisha  maelfu ya watu kukosa makazi baada ya nyumba zao 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa zikiwamo 44 ambazo ni za taasisi mbalimbali za umma ambapo takwimu hizo zinaweza kuongezeka.

Hakika taifa limepoteza watu wengi ambao ni nguvu kazi sambamba na kupata hasara kutokana na uharibifu uliotokea wa majengo.

Tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za awali za kuwasaidia waathirika sanjari na kugharamia majeneza ya waliofariki, ni jambo jema kuchukua hatua hiyo.

Tumewasikia wataalamu mbalimbali wa masuala ya miamba na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) wakielezea namna hali hiyo inavyoweza kutokea ambapo tahadhari za matetemeko mengine madogo zimetolewa.

Imeelezwa kwamba, chanzo cha tetemeko la ardhi husababishwa na  matabaka ya miamba  kuwa katika hali ya fukuto jingi la  joto na kusigana kwa miamba  na kusababisha miamba hiyo kukatika hali ambayo hufanya ardhi kutikisika.

Imeshauriwa kwa wananchi kuwa inapotokea tetemeko, wanapaswa kuchukua tahadhari ya kukaa mbali na miti, nguzo za umeme, nyumba ndefu kama vile maghorofa na iwapo wapo ndani ya jengo ni vema kukaa katika kona za ukuta ili kujizuia na madhara.

Lengo la andiko hili si kurudia kile kilichosemwa na wataalamu na kuandikwa au kutangazwa  kwenye vyombo vya habari,  la hasha bali ni kutaka kuwakumbusha wakazi wa Mwanza ambao asilimia 90 ya makazi yao yamejengwa milimani.

Mbaya zaidi nyumba nyingine zimejengwa chini ya mawe makubwa yenye taswira au uelekeo wa kuanguka  muda wowote.

Bila shaka kila mmoja anayeijua Mwanza anafahamu kama tetemeko hilo lingetokea ndani ya mkoa huo ingekuwa maafa makubwa kuliko yaliyotokea  Kagera.

Kwa wale wenyeji wa Mwanza wanafahamu jinsi nyumba zilivyojengwa juu na chini ya milima ya Kitangiri, Kabuhoro, Nyakabungo, Mabitini, Sinai, Igogo, Bugarika, Igoma, Kishili na sehemu nyingine, tunaweza kusema zipo hatarini.

Hadi sasa baadhi ya watu mkoani Mwanza wameingiwa na hofu juu ya maisha yao iwapo kitovu cha tetemeko  kitakuwa Mwanza.

Wakazi wa jiji hilo bado wana kumbukumbu ya jinsi ya  mawe yanavyoporomoka nyakati za mvua na kusababisha  vifo.

Zipo nyumba ambazo zimejengwa juu ya mawe yaliyobebana katika milima iliyopo Jiji la Mwanza ambapo tumeelezwa na wataalamu kwamba inapotokea tetemeko lazima ardhi inatikisika, je, hao watu watakuwa salama endapo hali hiyo itatokea?

Tukio hili liwe mfano na fundisho kwa Serikali na Watanzania wote kuchukua tahadhari ambapo elimu inatakiwa kutolewa kwa umma jinsi ya kuepuka madhara makubwa pale inapotokea tetemeko la namna hii.

Wataalamu wa ikolojia wasisubiri tukio kutokea ndipo wajitokeze kuelezea matetemko bali wawe na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma kwani matukio ya namna hii yalikuwa yakitokea katika mataifa mengine lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi sasa yameanza kutufikia.

Ni vyema hatua zikachukuliwa haraka kwa wakazi wa Mwanza wanaoishi milimani ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.

Aidha, elimu juu ya kuepuka majanga itolewe na si kusubiri matukio kutokea.

[email protected], 0683608958

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles