MWAKA jana Serikali ilitangaza kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Ikaiagiza Hazina kutoa Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharimia mpango huo.
Rais John Magufuli amekuwa akiutangaza mpango huo kila mara anapopata nafasi ya kuzungumza na wananchi akiwa ziarani mikoani au Ikulu. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Suleiman Jafo, amekuwa akisema mara kadhaa kwamba, fedha hizo zitatumika kwa ajili ya mitihani ya taifa, chakula cha wanafunzi, ada ya wanafunzi kwa wanafunzi wa bweni na kutwa pamoja na fedha za uendeshaji wa shule. Katika miezi sita ya kwanza ya utekelezaji wake, Serikali ilikuwa imetenga Sh bilioni 131.4 kwa ajili hiyo.
Sisi pamoja na umma kwa ujumla tulitarajia mpango wa elimu bure uongeze ufanisi na kupandisha ubora wa elimu nchini, hususan katika shule za umma.
Hata hivyo, matokeo ya darasa la saba mwaka huu hayaakisi mwenendo mzuri wa ubora wa elimu kwa shule za umma. Matokeo ya darasa la saba mwaka huu yanaonesha kupanda kwa ufaulu kwa asilimia mbili, huku shule nyingi za binafsi zikiongoza katika matokeo ya jumla.
Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), watahiniwa 10 (aliyeshika namba moja hadi 10) bora kitaifa  wanatoka shule zinazomilikiwa na watu au mashirika binafsi. Shule zilizoongoza ni za binafsi pia. Baadhi yake ni St. Peter (Kagera) iliyokuwa na watahiniwa 46 na imeshika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili imeshikwa na St. Severine (Kagera) iliyokuwa na wahitimu 66, Alliance (Mwanza) iliyokuwa na wahitimu 42 imeshika nafasi ya tatu, wakati nafasi ya nne ikichukuliwa na Sir John (Tanga) iliyokuwa na wahitimu 41.
Shule 10 zilizoshika nafasi za mwisho ni Nyahaa (Singida), ya pili ni Bosha (Tanga), ya tatu ni Ntalasha (Tabora), ya nne ni Kishangazi (Tanga), ya tano ni Mntamba (Singida), ya sita ni Ikolo (Singida), ya saba ni Kamwala (Songwe), nane ni Kibutuka (Lindi), ya tisa ni Mkulumuzi (Tanga), huku shule ya mwisho kabisa ikiwa Kitwai ‘A’ (Manyara).
MTANZANIA Jumapili tunasema lazima Serikali ijipange kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka katika shule za umma. Fedha inayotolewa na Serikali kugharimia mpango wa elimu bure lazima ionekane kutoa matunda. Na hakuna matunda bora kama kuona idadi ya watoto wanaofaulu kwenda sekondari ikiongezeka.
Tunasema kutenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu bure kwa watoto wetu ni mpango mzuri, lakini lazima uendane na mambo mengine, kama kuboreshwa kwa maslahi ya walimu, vifaa, mazingira ya kufundishia pamoja na kudhibiti nidhamu ya walimu.
Moja ya sababu ambazo tunadhani shule binafsi zimefanya vizuri ni pamoja na ukweli kwamba walimu wake wanalipwa vizuri zaidi kuliko wale wa shule nyingi za umma. Serikali ilichukulie hili kama changamoto. Ni kweli mpango wa elimu bure umeongeza idadi ya watoto wanaokwenda shule. Awamu zinazofuata za mpango wa elimu bure zijikite zaidi katika kuangalia ubora wa wanafunzi hao.