Na ABDUL MKEYENGE
BAADA ya kupisha michuano ya Chalenji iliyofanyika nchini Kenya na kuipisha ile ya FA, wiki hii mchakamchaka wa Ligi Kuu Tanzania Bara umerudi tena kwa viwanja mbalimbali kuwaka moto.
Ligi hiyo imerudi kwa msisimko wa hali ya juu kwa kila timu kutaka kushinda mchezo wake ili kujiweka eneo zuri kabla ya mzunguko wa kwanza kumalizika na kuingia mzunguko wa pili.
Ligi hiyo ilitarajiwa kuendelea jana usiku kwa mchezo mmoja kupigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kwa kuwakutanisha wenyeji Azam FC ambao walikwaana na timu ya Stand United ya Shinyanga.
Azam FC licha ya kuachana na mastaa wao wengi waliojiunga na timu mbalimbali, lakini bado wameonekana kuwa wabishi katika usukani wa ligi hiyo kwa kukabana koo na Simba.
Kabla ya mchezo wao wa jana, Azam FC walikuwa na pointi 23 kama ilivyo kwa Simba, lakini wamerudi katika duru hili la 12 wakiwa na mshambuliaji mpya, Benard Arthur kutoka Ghana ambaye amekuja kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji iliyofunga mabao tisa mpaka sasa.
Baada ya mchezo huo wa jana, ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo mitatu ambayo itachezwa katika viwanja vya Samora (Iringa), Nangwanda Sijaona (Mtwara) na Manungu (Morogoro).
Vinara Simba wao watakuwa ugenini Mtwara kucheza dhidi ya Ndanda FC inayoshika nafasi ya 11 na kujikusanyia pointi 11. Simba wataingia uwanjani hapo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa kwenye michuano ya FA na timu ya Daraja la Pili (SDL) Green Warriors, lakini watatambia nyota wao mpya, Asante Kwasi, waliyemsajili dirisha dogo.
Vinara hao pia watakuwa wakicheza mchezo wao wa kwanza wa ligi bila kuwepo kwa kocha wao, Joseph Omog, aliyetimuliwa baada ya Simba kufungwa na Warriors.
Hivyo kikosi chao kitakuwa chini ya kocha raia kutoka Burundi, Masoud Djuma ambaye ana kaimu nafasi ya Omog, huku uongozi wa timu hiyo ukiwa katika sakasaka ya kutafuta kocha mpya.
Ndanda FC walio chini ya kocha Malale Hamsini, wamekuwa na rekodi mbaya wanapocheza dhidi ya Simba, iwe uwanjani hapo au uwanja mwingine, lakini katika kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo, wamembadilisha nahodha wao kutoka kwa William Lucian ‘Gallas’ aliyewahi kupita Simba na sasa nahodha wa kikosi hicho ni Jacob Massawe.
Simba iko katika hatihati ya kuwatumia nyota wake wa kimataifa Mganda Emmanuel Okwi raia na Mnyarwanda Haruna Niyonzima, wanaotajwa kuwa na majeraha, huku Ndanda FC wakitarajia kuwa na Mrisho Ngassa aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Mbeya City.
Pambano lingine litakuwa la Lipuli dhidi ya Tanzania Prisons litakalopigwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa. Lipuli FC wataingia katika mchezo huo bila ya mlinzi wao king’ang’anizi, Kwasi, aliyejiunga na Simba.
Kwasi alikuwa akiibeba timu hiyo katika safu ya ulinzi na wakati mwingine akifunga mabao. Mpaka anaondoka kikosini humo alishafunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara. Mchezo huo utachezwa mchana.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa vuta nikuvute kutokana na timu hizo kupishana pointi moja, utawahitaji Lipuli FC walioko nyumbani kushinda pambano hilo ili kukaa juu ya Tanzania Prisons ambao wanashika nafasi ya sita na kuwa na pointi 15, huku Lipuli FC wao wakiwa na pointi 14 nafasi ya saba.
Ngome ya Lipuli FC iliyoondokewa na kamanda wake Kwasi, inahitaji kuwa makini na mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Mohamed Rashid, aliyefunga mabao sita na akionekana kuwa mwiba mkali kwa walinzi wa timu pinzani.
Mtibwa Sugar baada ya kuitoa katika michuano ya FA timu ya Villa Squad inayoshiriki Daraja la Pili (SDL) kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, leo imerudi uwanja wa nyumbani Manungu kwa kucheza dhidi ya Majimaji ya Songea.
Mtibwa Sugar walioanza ligi vyema na sasa kuonekana kama inapepesuka, itahitaji kushinda mchezo huo ili kufufua matumaini yao ya kufanya vyema msimu huu kama walivyotamba awali.
Timu hiyo yenye pointi 18 na kujiimarisha katika nafasi yao ya tano, itaingia katika pambano hilo ikimkosa mshambuliaji, Kelvin Sabato, mwenye majeraha ya nyonga, huku ikitarajiwa kupata urejeo wa mlinda mlango wao, Shaban Kado, aliyekosa michezo yote 11, kutokana na majeraha.
Majimaji walioanza ligi kwa kusuasua nao wameanza kuimarika mchezo kwa mchezo na kufanya washike nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi hiyo, huku wakiwa na pointi 11.
Ndani ya mchezo na michezo mingine ya ligi, Majimaji itaanza maisha mapya bila ya aliyekuwa nahodha wao, Danny Mrwanda ambaye ametolewa kwa mkopo kwenye timu ya JKT Mlale inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mabingwa watetezi Yanga watakaokuwa ugenini kukipiga na timu ‘korofi’ Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Yanga yenye pointi 21 na kushika nafasi ya tatu, itaingia katika mchezo huo kwa kuwakosa wachezaji wake kadhaa kwa sababu mbalimbali. Itawakosa Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Kelvin Yondan, Baruani Akilimali wenye majeruhi na itamkosa Ibrahim Ajib mwenye kadi tatu za njano, Obrey Chirwa aliyeko kwao Zambia.
Lakini faraja kubwa katika mchezo huo ni urejeo wa kinara wa mabao wa timu hiyo, Amissi Tambwe ambaye alikosekana kwa michezo yete ya Yanga msimu huu na amerudi katika mchezo wa FA dhidi ya Reha na kuonyesha kuwa kuna kitu Yanga kimeongezeka.
Yanga watakuwa na faida ya kuwa na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Mbao FC kwenye kikosi chao, Pius Buswita. Kiungo huyo alikuwa sehemu ya wachezaji wa Mbao FC waliofanya vyema msimu uliopita na kuifikisha timu hiyo kwenye fainali ya FA ambayo walicheza dhidi ya Simba na kupoteza mchezo huo.
Lakini Mbao FC iliyo chini ya kocha Etienne Ndayiragije, imejikusanyia pointi 11 na kushika nafasi ya nane. Timu hiyo imeonekana kuwa mwiba mchungu kwa timu za Simba na Yanga zinapokwenda Uwanja wa Kirumba kucheza dhidi yao.
Itakumbukwa mwanzoni mwa msimu huu, Mbao FC iliwalazimisha Simba sare ya kufungana mabao 2-2, katika uwanja huo na kuamsha shangwe iliyowalaza mapema mashabiki wa Simba walioutazama mchezo huo kupitia runinga na wale waliokuwa uwanjani kuutazama.
Mchezo mwingine wa kesho utakuwa wa Njombe Mji ya jijini Njombe ambayo itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sabasaba kucheza dhidi ya timu ya Singida United.
Njombe Mji wanaoshika nafasi ya 15 katika timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, wanatakiwa kupambana kiume katika mchezo huu ili waweze kuondoka na ushindi, la sivyo mvua ya mabao inaweza kuwaangukia.
Singida United wanaoshika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 20, wamekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu tangu walipopanda daraja kwa kufundishwa na Hans Van Pluijm aliyewahi kuifundisha Yanga. Mchezo huu nao utachezwa mchana.
Mzunguko wa 12 wa michezo ya ligi hiyo unatarajiwa kuhitimishwa Jumatatu ya sikukuu ya mwaka mpya kwa michezo miwili kuchezwa siku hiyo.
Mbeya City watakuwa nyumbani kwao Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine kuwakaribisha Kagera Sugar. Mbeya City inayotetereka kwa kiwango misimu ya hivi karibuni, inashika nafasi ya 12 na kuwa na pointi 11, itahitaji kurekebisha makosa yake katika michezo ya nyuma ili iweze kurudisha heshima yake wakati huu ilioachana na kiungo wake mshambuliaji, Mrisho Ngassa, aliyetimkia Ndanda FC.
Mbeya City wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa kwenye michuano ya FA kwa kufungwa na timu ya Daraja la Pili, Ihefu FC.
Kagera Sugar walioanza kujipapatua upya wamekuwa wakiimarika hivi sasa baada ya kupoteza michezo kadhaa ya mwanzoni mwa ligi na mpaka sasa inashika nafasi ya 10 na kujikusanyia pointi 11 kama ilivyo Mbeya City wanaokwenda kukwaana nao.
Wachimba Madini wa Mwadui FC watakuwa nyumbani kwao Mwadui Complex kucheza dhidi ya Ruvu Shooting ya Masau Bwire.
Mwadui FC inayojikongoja katika nafasi ya 14 kwa kuwa na pointi tisa, wanatakiwa kujipanga vyema ili kuhakikisha mpaka mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo unamalizika wako kwenye nafasi nzuri.
Ruvu Shooting nayo haiko kwenye nafasi nzuri. Inashika nafasi ya 13 kwa kujikusanyia pointi 11, hivyo nao wanahitaji kuzichanga vyema karata zao ili kujiweka katika mazingira mazuri.
Timu nyingi zinazoshiriki ligi hiyo zinaonekana kuwa karibu kipointi, hivyo timu inayoweza kumshinda mwenzake katika michezo hii ya kufungia na kufungulia mwaka inaweza kujiweka katika mazingira mazuri.