KULWA MZEE
MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP) ameomba Mahakama ya Rufaa iamuru rufaa iliyofunguliwa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wakipinga kufutiwa dhamana itupiliwe mbali na kwamba rufaa hiyo ni batili.
Akiiwakilisha Jamhuri mbele ya jopo la majaji watatu, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai wajibu maombi waliwasilisha rufaa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Sam Rumanyika bila kuambatanisha uamuzi wa Mahakama ya Kisutu na mwenendo wa kesi hiyo.
Nchimbi alidai rufaa yao ina sababu tatu ambapo sababu ya pili inayodai kwamba Jaji Rumanyika alikuwa na upendeleo aliiondoa baada ya jopo kuhoji na kuonekana haijawahi kuwasilishwa Mahakama Kuu.
Jopo la majaji hao, Stellah Mugasha, DK. Gerald Ndika na Mwanaisha Kualiko.
Nchimbi anadai kwa kupokelewa kwa rufaa ya kina Mbowe Mahakama Kuu ikiwa hakijaambatanishwa na uamuzi na mwenendo wa kesi kama Sheria namba 362(1) inavyoelekeza kunaifanya rufaa hiyo kuwa batili na kuonekana haiko sahihi mahakamani.
Akijibu Wakili Peter Kibatala alidai rufaa hiyo iliwasilishwa mahakamani bila sababu za msingi na kwamba hakuna ubishi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu hakuwa na mamlaka ya kuita jalada la kesi na kuendelea kusikiliza rufaa.