NEW YORK, Marekani
HATIMAYE bilionea Donald Trump ameishtusha Marekani na Dunia, akiwa ametokea kukabiliana na wimbi kubwa lililomkabili la mashambulio ya chuki kumshinda mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Hillary Clinton.
Kwa ushindi huo, Trump anakuwa rais wa 45 wa Taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi na kijeshi duniani.
Mgombea huyo wa Chama cha Republican, alimshinda Hillary baada ya kupata kura 276 za wawakilishi wa majimbo dhidi ya 218 za mpinzani wake.
Ushindi huo usiotarajiwa, ulishuhudiwa ukiyatumbukiza masoko ya hisa duniani katika mkanganyiko na kuvuruga mwelekeo wa siasa wa muda mrefu duniani.
Baada ya kushindwa,Hillary alimpigia simu Trump na kumpongeza.
Mapema Jumanne, Mwenyekiti wa kampeni ya Clinton, John Podesta aliwataka mamia ya mashabiki walokusanyika katika ukumbi  mjini New York kurudi nyumbani na kwamba mgombea wao hatazungumza.
Muda mfupi baadaye, mgombea mwenza wa Trump, Mike Pence alikuwa wa kwanza kutoa neno la shukrani kwa wafuasi wao.
Baada ya kumaliza kuzungumza, Pence alimkaribisha rais mteule wa 45 wa Marekani. Hilo likiwa ni tukio la historia mtu ambaye hajawahi kushika nafasi au wadhifa wowote   serikalini kuchaguliwa kuliongoza Taifa kuu la dunia.
Akihutubia mamia ya wafuasi wake Jijini New York,Trump aliahidi kuwa rais wa wote na  kuyatibu majeraha ya nchi, huku akimsifu mpinzani wake, Hillary kwa utumishi wake wa umma kwa muda mrefu.
Ushindi wa Trump mbali ya kuwashangaza watu wengi duniani, Â unahitimisha utawala wa miaka minane wa Chama Democrat na kuipeleka Marekani katika njia ambayo wengi wanasema isiyojulikana.
Akiongozana na familia yake mbele ya wafuasi waliojawa na furaha, Trump, kwanza amemsifu mpinzani wake,Hillary kwa utumishi wake wa muda mrefu   akisema amepokea simu kutoka kwake ya kumpongeza baada ya matokeo ya Pennsylvania ambalo limekuwa likikipigia chama cha Democrat tangu mwaka 1992.
Alisema, “nimepokea simu kutoka kwa Clinton. Ametupongeza, ni kwa ajili yetu, kwa ajili ya ushindi wetu na ninampongeza yeye na familia yake kwa namna alivyopambana katika kampeni. Amepambana kweli. Hillary amefanya kazi kwa bidii na kwa muda mrefu na tuna deni kubwa kwake kwa mchango wake katika nchi yetu”.
Mfanyabiashara huyo ameahidi kufanya kazi kwa usawa na kila mmoja yakiwamo mataifa yote ambayo yatakuwa tayari kufanya kazi naye, akiongeza kwamba Marekani itakuwa na uhusiano mzuri.
Rais huyo mteule sasa anacho kibarua cha kuwaunganisha Wamarekani waliogawanyika baada ya kumalizika  uchaguzi.
“Sasa ni wakati wa Marekani kutibu majeraha ya mgawanyiko uliotokea, tunahitaji kushirikiana. Kwa Republican wote, wana-Democrat wote na wale walio wasio na upande wowote,nasema ni muda sasa kwetu kuungana   kama Wamarekani. Ni muda sasa,” alisema Trump.
Kwa mujibu wa makadirio ya kituo cha habari cha Fox na Shirika la Habari la Associated Press (AP), Trump alijikusanyia kura za kutosha kati ya kura 270 za wajumbe zilizokuwa zikihitajika yeye kushinda muhula wa miaka minne.
Pamoja na hilo, matokeo yalionyesha Chama cha Republican kinaelekea kudhibiti Baraza la Wawakilishi na lile la Seneti. Trump alifanikiwa kushinda katika majimbo yaliyokuwa yakingombaniwa na yenye kete za ushindi yakiwamo Florida na Ohio.
Akiingia Ikulu bila  kuwa na uzoefu wowote wa uongozi, Trump atakuwa na umri wa miaka 70 na kuweka rekodi ya rais mwenye umri mkubwa kuwahi kuliongoza Taifa hilo.
Kwa upande mwingine,Hillary iwapo angeshinda angekuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza Taifa hilo. Kutokana kushindwa kutimiza ndoto zake, alikataa kutoa hotuba ya baada ya matokeo jana usiku.