RAIS Dk. John Magufuli leo atawaongoza Wazanzibari katika sherehe ya kumwapisha Rais mteule wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Hata hivyo sherehe hizo zinafanyika huku kukiwa hakuna taarifa za kuhudhuriwa na wageni kutoka mataifa ya nje, hasa nchi za Ulaya.
Baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 na matokeo kumtangaza Dk. Shein kuwa mshindi kwa kupata asilimia 91 ya kura zilizopigwa, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini walitoa tamko la kupinga Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendesha uchaguzi huo.
Mmoja wa maofisa wa juu serikalini ameiambia MTANZANIA kuwa pamoja na sherehe hizo, bado hawajapata taarifa za wageni wengine mashuhuri kutoka nje watakaohudhuria hadi jana jioni.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye jana zilisema mabalozi waliothibitisha kushiriki sherehe hizo ni kutoka nchi za Oman na India pekee.
Taarifa kutoka Ikulu Zanzibar, zinasema sherehe hizo zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Amaan na kuanza saa 12 asubuhi, zitahudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri mbalimbali kutoka Tanzania Bara.
Katika sherehe hizo pia amealikwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, pamoja na wenyeviti wa vyama vya siasa nchini.
Serikali pia imetangaza siku ya leo kuwa ni ya mapumziko ili kuwapa nafasi wafanyakazi na wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio la kuapishwa Dk. Shein.