26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Dk Shein aeleza awamu zote za SMZ zilivyowekeza kwenye majengo ya kisasa

Mwandishi wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema ujenzi wa majengo bora ya Serikali ni azma iliyoanza mara tu baada ya mapinduzi Januari 1964.

Akinukuu maelezo ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Rais Dk. Shein alisema nchi inaendelea kwa kujengwa majengo na ndio maana awamu ya saba nayo inatekeleza hatua hiyo.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo jana katika hafla ya ufunguzi wa jengo la Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati na Taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA), huko Maisara, Jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Shein alisema awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilifuata mkondo huo ambapo kila awamu ilijenga majengo bora na ya kisasa mjini na vijijini.

Alisema Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar ina historia katika ujenzi wa majengo yakiwemo yale iliyoyajenga wenyewe kwa kupitia wataalamu na wajenzi wazalendo yakiwemo majumba ya Michenzani, Kilimani, Mpapa, Kikwajuni, Mkoani, Wete na Chake Chake kwa kupitia idara maalum ya ujenzi iliyokuwa chini ya SMZ.

Alisema ujenzi wa kutegemea wataalamu wa nje unaviza elimu na utaalamu wa wajenzi wazalendo na kueleza nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Kampuni ya Ujenzi yake wenyewe ambayo tayari imeshaanza kazi.

Alisema kampuni hiyo ishaundwa kwa lengo la kujenga majengo bora na ya kisasa ambayo itawashirikisha wataalamu na mafundi kutoka idara za vikosi vya SMZ na pale itakapoonekana haja ya kukaribishwa kampuni za nje zitakaribishwa.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kampuni hiyo itajengewa uwezo na kwa kuanzia itaanza kujenga majengo ya hospitali ya Binguni, iliyopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakwenda na wakati licha ya kuwepo watu ambao hawapendi pale inapofanya mambo mazuri huku akirejea kauli yake ya kukemea wale walioharibu miundomnibu ya taa za barabarani kwa kuzivunja kwa makusudi huko kisiwani Pemba.

Alisisitiza kuwa waliofanya hivyo wana matatizo ya akili kwani si rahisi kwa mtu mwenye akili zake timamu akaharibu kwa makusudi taa za barabarani ambazo zinawasaidia wananchi wote.

Sambamba na hayo Rais Dk. Shein alisema mwelekeo wa matokeo ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia unakwenda vizuri na taarifa maalum itatolewa baada ya Kampuni ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) na RAK Gas ya Ras Al Khaimah kumaliza kazi waliyopewa.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina uwezo mkubwa na ikiamua kufanya mambo yake wenyewe inafanya tena bila ya kuwezeshwa kama ilivyofanya kwa ujenzi wa jengo hilo ambapo fedha zote ni za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 Naye Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib, alimshukuru na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa niaba ya wafanyakazi na uongozi wa wizara hiyo kwa kujenga jengo hilo sambamba na miongozo aliyokuwa akiitoa.

Mapema,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Ali Khalil Mirza, alisema gharama zote za ujenzi wa jengo hilo Sh bilioni 19.9 zimetolewa na SMZ.

Aliongeza kuwa ghorofa 7 za juu ya ardhi za jengo hilo zitatumika kwa shughuli za kiofisi kwa watendaji  wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati pamoja na Taasisi zake.

Alieleza ghorofa iliyoko kwenye usawa wa ardhi imepangwa kutumika kwa shughuli za kibenki na iliyopo chini ya ardhi ni kwa ajili ya kuegesha vyombo vya usafiri vya wafanyakazi watakao tumia jengo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles