Winfrida Mtoi na Onesmo Kapinga
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, amekitaka Chama Cha Soka Wilaya ya Temeke(TEFA), kulinda na kuendeleza heshima ya kimpira wilayani humo kwa kuepuka migogoro.
Dk. Ndumbaro alipiga simu wakati hafla ya uzinduzi wa ofisi za chama hicho uliofanyika leo Mei 11, 2024 kwenye Uwanja wa TEFA, Tandika, jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo mwenye dhamana ya michezo nchini, amempongeza Mwenyekiti wa TEFA, Ally Kamtande kwa kusimamia marekebisho ya Katiba na kuunda kamati zitakazosimamia maendeleo ya soka.
“Kamati ndio nguzo ya mafanikio Temeke, zitaufanya mpira wa Temeke kuendelea. Kitu muhimu ni kuepuka migogoro na mtu yeyote anayetaka kuwagawa,” amesema Dk. Ndumbaro.
Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Wallace Karia ambaye naye alipiga simu wakati wa hafla hiyo, amesema amefurahishwa na jitihada za uongozi wa chama hicho na kuahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha uwanja wa TEFA unafanyiwa maboresho ili kuingiza mapato.
“Dar es Salaam isipofanya vizuri mpira wetu utakufa. Uwanja wa TEFA mimi pia nimechezea mpira hapo ni wa zamani sana. Lakini niwapongeze viongozi wa sasa kwa jitihada wanazofanya na sisi tutahakikisha uwanja unafanyiwa matengenezo ili kuingiza mapato,” ameeleza Karia.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Kwanza wa TFF, Athuman Nyamlani ambaye alikuwa mgeni katika uzinduzi wa ofisi hizo, amebainisha kuwa walikotoka migogoro kwenye mpira ilikuwa kawaida lakini sasa suluhisho limepatikana ambalo ni Katiba.
Amesema kutokana na mabadiliko ya soka duniani, mpira kwa sasa unatengeneza ajira na chanzo cha kukuza uchumi wa nchi.
“Tunajua mabadiliko ya katiba siku zote yanakuja na hofu lakini niseme kwamba Katiba ya TEFA sasa itakuwa ni suluhisho la matatizo mengi, sisi tulichelewa kufanya hivyo katika kipindi chetu.
“Tuondokane na mazoea na kwenda sehemu nyingine, lazima mpira uendeshwe kama kiwanda, hivyo kitakachosaidia kufanya yote hayo ni Katiba nzuri,” amesema Nyamlani.
Ameutaka uongozi kuhakikisha wanabana matumizi na kufanya maendeleo ya chama na kuongeza vyanzo vya mapato na vitega uchumi vitakavyosaidia vizazi vijavyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA)Lameck Nyambaya, amekiri kuwa ndani ya miezi mitano ya uongozi mpya Temeke imeweza kubadilika, hali inayowafurahisha kwa kuwa wanategemea uimara wa vyama vya Wilaya.
Akizungumzia maendeleo aliyofanya katika kipindi cha miezi mitano cha uongozi wake, Mwenyekiti wa TEFA, Kamtande amesema amefanikiwa kufanya ukarabati wa ofisi na maeneo mengine ikiwamo miundombinu.
Ametaja ofisi alizotengenza kuwa ni za waamuzi, soka la wanawake, makocha na vyumba vya kubadilishia nguo kipindi timu zikiwa zinacheza uwanjani kwao, huku akitengeneza choo chenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 100.
“Nimebadilisha historia ya TEFA, palikuwa panaitwa mabatini, geti la kuingilia lilikuwa la mabati, nimefanikiwa kulitoa na kuweka lingine la chuma, nimetengeneza ofisi, nimekarabati visima viwili vya maji safi na kila kamati itakuwa na ofisi yake hapa,” amefafanua.
Aidha amewataka wadau wa soka Temeke kumuunga mkononna kuondoa migogoro ili kuweza kuendeleza mpira katika Wilaya hiyo.