*Asema hakuna mwananchi aliyeachwa nje
Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Waziri wa Fedha na Mipango,Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa lengo la Rais Samia Suluhu Hassan katika bajeti ya mwaka huu ilikuwa ni kutoa unafuu kwenye maisha ya Watanzania pamoja na kuzalisha ajira.
Dk.Mwigulu ameyasema hayo leo Jumamosi Juni 18, 2022 wakati akichangia kwenye katika mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka 2022/23 mjadala wa Kitaifa ulioendeshwa mtandaoni.
Amesema kwa ujumla wake bajeti ya mwaka huu ilikuwa imekusudia kukabiliana na masuala ya msingi na muhimu ambayo ndiyo ilikuwa kwenye kipaumbele cha Rais Samia katika kuletea wananchi maendeleo.
“Moja ya jambo kubwa ambalo limeonekana kwenye tafasri ya bajeti ni kwamba dunia ilikuwa kwenye msukosuko na bado iko kwenye msukosuko, tumetoka kwenye janga la Uviko-19, hatujatulia ikaja mvutano wa Urusi na Ukraine.
“Kwa maana hiyo uchumi na maisha ya watu hapa duniania hayajatengemaa kama ilivyokuwa hapo mwanzo, yamekuwa katika hali ya tofauti kwa kupanda gharama za maisha, hivyo bajeti hii haikuwa na fursa kubwa sana ya kusema kuwa tutaongeza kodi juu.
“Kwani tayari wananchi ambao ndiyo walipakodi wakubwa walikuwa kwenye tatizo hilo la kupanda kwa gharama za maisha, kwa hiyo Mheshimiwa Rais alichoelekeza ni kuona namna gani bajeti hii inatoa unafuu kwenye maisha ya Watanzania.
“Jambo la pili ambalo alielekeza nikwamba pamoja na tatizo la uviko na vita ya Ukraine, lipo tatizo ndani ya nchi yetu la ukosefu wa ajira kwa vijana na ukosefu wa umaskini kwa Watanzania.
“Kwa hiyo bajeti hii alisema lazima imlike kuona tunachukua hatua gani kwa ajili ya watu wetu, ndiyo maana utaona kwamba maeneo ambayo utakuta tumepandisha kodi au tozo ujue ni eneo ambalo kisera tulipanga kuchochea uzalishaji wa ndani,” amesema Dk.Nchemba na kuongeza kuwa:
“Katika maeneo ambayo tulipanga kutoa unafuu utaona kwamba ulekeo wa kodi na ada ulishuka chini ili kuweza kutoa uchocheo wa kisera wa kuweza kuamsha uchumi wetu.
“Kwa hiyo hilo ndilo lilikuwa lengo hata kwenye dhima kubwa ya bajeti ya Afrika Mashariki ambayo ilikuwa inaongelea kasi ya kufufua uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.Kwa maana hiyo katika kuviunganisha hivi vya kutoa unafuu na kuchochea uzalishaji lengo ni moja ya kushughulika na suala la ajira na umaskini wa watu wetu,” amasema Dk. Mwigulu.
Amefafanua zaidi kuwa tathimini ya uhimilivu wa deni la taifa iliyofanywa na Shirika la Fedha la Kimataifa(IMF) na Benki ya Dunia(WB) ilionyesha kwamba Tanzania imetikisika na kwamba njia za kujinasua ilikuwa ni kuwekeza katika sekta za uzalishaji hatua ambayo itachochea kuongezekwa kwa uuwiano wa deni la taifana mauzo ya nje tofauti na sasa.
“Hivyo, kwa picha kubwaya bajeti hayo ndiyo maeneo ambayo tulikuwa tunaelekezwa kuyatafutia majibu yake,” amesema Dk. Mwigulu.
Bajeti ya wananchi
Akizungumzia sababu za bajeti hiyo kuitwa ‘yawanchi’ amesekuwa kuwa wananchi waliowengi wako katika sekta ya uzalishaji hatua ambayo bajeti ya mwaka huu imeongeza fungu kwenye sekta hususan za kilimo, mifugo na uvuvi.
“Tumeongeza bajeti kutoka Sh bilioni 200 hadi zaidi ya Sh bilioni 900 kwenye kilimo ambako huko kuna zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wote.
“Tumeongeza bajeti ambayo ni nyongeza ya ile ambayo ilipita kwenye kamati na kufikia Sh bilioni 100 kwenye sekta ya Mifugo na Uvuvi ambapo huko pia kuna Watanzania waliowengi, hivyo asilimia 40 inaendakwenye mifugo na inayobaki inaenda kwenye uvuvi.
“Ukitoka hapo, tumetenga fedha kwa ajili ya biashara ndogo ndogo Sh bilioni 45 kando na fedha za Halmashauri na Majiji, kwa ajili ya kujenga miundombinu kwa kila mkoa na kutoa mikopo, hivyo utaona kwamba tumegusa makundi yote muhimu,” amesema Dk. Nchemba na kuongea kuwa wamebadilisha sheria 19 ambazo zilikuwa ni kikwazo kwenye mazingira bora ya kufanya biashara.
“Kwani sekta binafsi ndio injini ya kuendesha uchumi, hivyo unapoipa fursa sekta binafasi unakwenda kugusa maisha ya Watanzania na kupunguza umaskini.
“Ukirudi kwa wale waliko maofisini utaona kwamba watumishi wa umma bajeti hii imepandisha mishahara yao kwa watu wa kima cha chini kwa zaidi ya asilimia 23 kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingine, imeangalia upya kikokotoo na mafao, hivyo ukijumlisha hapa utaona kwamba hakuna mwanchi aliyeachwa nje, hiyo ndiyo maana hali ya bajeti ya wanananchi,” amesema Dk. Nchemba.