27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango: Pato la taifa linakua kwa asilimia 6.9

Ramadhani Hassan – Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema katika kipindi cha mwaka 2016 hadi mwaka jana, pato la taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka.

Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21 mbele ya wabunge jijini Dodoma jana, Dk. Mpango alisema ukuaji huo ulichochewa na sekta ya ujenzi kufuatia kuongezeka kwa uwekezaji, hususan katika miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege.

Dk. Mpango alisema pia kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za maji, kuimarika kwa huduma za usafirishaji, kuimarika kwa shughuli za habari na mawasiliano na  kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe, kulisaidia ukuaji huo.

Alisema ukuaji mzuri wa pato la taifa umechangia kuongezeka kwa ajira 6,032,299 ambapo kati ya hizo, 1,975,723 ni kutoka sekta rasmi na 4,056,576 sekta isiyo rasmi.

Dk. Mpango alisema mojawapo ya malengo ya Serikali ya awamu ya tano ni kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

“Moja ya nyenzo za kutekeleza lengo hilo ni kuzikwamua kaya masikini kutoka katika lindi la umasikini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Serikali imesaini mkataba na Washirika wa Maendeleo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 883.31,” alisema Dk. Mpango.

MFUMUKO WA BEI

Waziri Mpango alisema mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya wigo wa tarakimu moja wa wastani wa asilimia 4.4 kati ya mwaka 2016 na mwaka 2019.

Alisema kati ya Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.7 ambao uko ndani ya lengo la ukomo la mfumuko wa bei wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wa asilimia 5.

“Mwenendo wa mfumuko wa bei nchini kwa mwaka 2019 uliendelea kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja kutokana na upatikanaji mzuri wa chakula, utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia na utekelezaji na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti,” alisema Dk. Mpango.

UJAZI WA FEDHA

Alisema ujazi wa fedha umeendelea kukua kwa kasi kulingana na mahitaji ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ambapo katika mwaka 2019, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi – M3, uliongezeka na kufikia Sh bilioni 28,313.1 kutoka Sh bilioni 25,823.5 mwaka 2018 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.6, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.5 mwaka uliotangulia.

“Ukuaji huo

unadhihirisha kuwepo kwa fedha za kutosha kuendesha shughuli za uchumi na kuongezeka kwa uwezo wa sekta ya kibenki kutoa mikopo kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, ujenzi na madini,” alisema Dk. Mpango.

MIKOPO SEKTA BINAFSI

Alisema mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka na kufikia Sh bilioni 19,695.4 mwaka 2019, kutoka Sh bilioni 17,726.8 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 11.1, likilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.9 mwaka 2018.

“Ukuaji huo unaenda sambamba na mwendelezo wa utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwenye uchumi, na utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha mazingira ya biashara nchini,” alisema Dk. Mpango.

Aidha, alisema kuimarika huko kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kumechangiwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kupunguza kiwango cha mikopo chechefu, ikiwemo kuboresha matumizi ya mfumo wa taarifa za wakopaji na kusimamia utekelezaji wa maadili bora kwa watumishi wa sekta ya kibenki katika kutoa mikopo.

Alisema sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye kutengeneza faida.

“Sekta hiyo pia imeendelea kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha unaowezesha kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kibenki kwa ajili ya shughuli za maendeleo,” alisema Dk. Mpango.

 Alisema katika kipindi kilichoishia Desemba mwaka jana, mtaji wa sekta ya kibenki uliongezeka na kufikia Sh bilioni 4,102.7 kutoka Sh bilioni 3,800.3 Desemba 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.0.

“Kiasi hiki cha mtaji wa msingi ni sawa na asilimia 16.8 ya rasilimali za benki ikilinganishwa na kiwango cha chini cha kisheria cha asilimia 10.0,” alisema Dk. Mpango.

KUSIMAMIA SERA ZA FEDHA NA BAJETI

Alisema Serikali itaendelea kutekeleza na kusimamia sera madhubuti za fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kuwa imara, jumuishi na endelevu.

 “Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli, itaendelea kutekeleza na kusimamia sera madhubuti za fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unaendelea kuwa imara, jumuishi na endelevu,” alisema Dk. Mpango.

Alisema Benki Kuu (BoT) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa imeanza utekelezaji wa sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha, ikiwemo kusajili watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja yote.

“Aidha, Benki Kuu inashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango katika kuutekeleza mpango wa elimu kwa umma kuhusu sera, sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha.

“Sheria na kanuni hizi mpya zitasaidia kuimarisha mfumo wa taarifa za wakopaji, kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma ndogo za fedha, ikiwemo riba kubwa na ukusanyaji wa madeni usiozingatia maadili,” alisema Dk. Mpango.

Alisema sheria na kanuni hizi pia zitasaidia kuongezeka kwa huduma jumuishi za fedha na elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wanaotumia huduma hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles