24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

DK. MPANGO AZITAKA BENKI KUGEUKIA VIWANDA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango

Na ASHA BANI – Dar es Salaam

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amezitaka sekta za fedha nchini, hasa mabenki kuwa kichocheo cha uchumi wa viwanda.

Dk. Mpango ameyasema hayo jana Dar es Salaam wakati wa  uzinduzi wa jina na nembo mpya ya Benki ya Posta Tanzania (TPB).

Alisema kuwa sekta ya mabenki ni muhimu hasa katika uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo na viwanda vya kati  hali itakayoweza kuchangia uchumi wa viwanda vikubwa nchini.

“Mabenki, hasa ikiwamo Benki ya Posta ndiyo kichocheo kikubwa katika kuwainua akina mama wanaofanya biashara ndogo ndogo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dk. Mpango aliipongeza bodi ya benki hiyo kwa kufanya kazi kwa ufanisi, ikiwamo kuongeza idadi ya matawi kutoka 28 ya awali na kufikia 60 ya sasa.

Dk. Mpango alisema benki hiyo imefanikiwa kuwanufaisha wastaafu mbalimbali mijini na vijijini jambo ambalo ni hatua nzuri na ya kupongezwa.

Alisema Serikali itahakikisha inafanya nayo kazi bega kwa bega ili kuwaongezea nguvu iweze kusaidia jamii zaidi.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi, alisema benki imekamilisha mchakato wa muda mrefu wa kuisajili kuwa chini ya sheria ya makampuni. Mchakato wake ulikamilika mwanzoni mwa mwaka jana.

“Benki iliamua kubadilisha nembo yake ili kwenda sambamba na jina hilo pamoja na mabadiliko makubwa ya kuiboresha yanayoendelea,’’ alisema Moshingi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Profesa Letticia Rutashobya, alimhakikishia Dk. Mpango kwamba benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake na kuweka jitihada zaidi ili kuwafikia Watanzania wengi, hususan walioko pembezoni ili waweze kunufaika na huduma hizo za kifedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles