Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango ameainisha maeneo matatu yatakayohakikisha zao la Korosho linaleta tija kwa Taifa na wakulima kwa ujumla ambayo ni upatikanaji wa masoko ya uhakika, kuimarisha tafiti ya zao hilo na kutafuta wawekezaji.
Dk. Mpango ametoa kauli hiyo Oktoba 11 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa zao la Korosho ulioshirikisha wadau 640 mbalimbali kutoka nchi 33 ukiwa na kauli mbiu ya ‘Wekeza kwenye korosho kwa maendeleo endelevu’.
Amesema wadau wajadili jinsi ya kukuza zao la korosho kwani lina faida nyingi katika mwili wa binanadamu na linachangia kukuza uchumi.
“Wizara ya kilimo hakikisheni mnaimarisha tafiti ya zao la korosho ili kuongeza uzalishaji utakaokidhi masoko, pia wadau hakikisheni mnatafuta changamoto na kuumizwa kichwa juu ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya zao hili,” amesema Dk. Mpango.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, thamani ya soko la korosho duniani inakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 10.5 ifikapo mwaka 2031 kutoka dola bilioni saba mwaka 2022, hivyo mkutano huo umekuja wakati muafaka ili kuzisaidia nchi zinazozalisha zao hilo kuweka mikakati madhubuti ya kunufaika nalo.
Amesema licha ya jitihada zilizofanywa na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzani, bado changamoto ya kuongeza thamani ya zao la korosho ipo kwa asilimia 90.
Amesema korosho inayozalishwa inauzwa nje ikiwa ghafi hali inayoshusha bei lakini pia bidhaa zingine zinazotokana na korosho kama siagi, mvinyo, juisi na maziwa zinakwenda kwenye nchi zingine na siyo nchi wazalishaji.
Ametaja changamoto nyingine kuwa huduma za ugani, pembejeo na teknolojia ambazo ni muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji kwa kuwa wakulima wanahitaji kusaidiwa ili kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa ya mikorosho.
“Kuna changamoto ya soko inayofanya uuzaji wa zao hili kwa ufanisi kuwa mgumu kutokana na kuwepo kwa ulaghai kati ya wanunuzi, wasafirishaji na madalali jambo linalowanyonya wakulima kwenye suala la bei, hivyo wadau wa mkutano huu wanapaswa kujadili na kuja na mikakati ya namna nchi wazalishaji zinavyoweza kuondokana na changamoto hizi,” amesema Dk. Mpango.
Aidha, amezitaka nchi za Afrika kupambana kutatufuta changamoto ya zao la korosho kwa kuondoa utitiri wa kodi.
Aidha, Dk. Mpango amewataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza nchini kwani hali ya hewa na ardhi ni nzuri kwa uzalishaji wa zao la Korosho.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, David Silinde amesema lengo la mkutano huo ni kutimiza adhma ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza tija kwa zao la Korosho na kutangaza fursa za uwekezaji ili kufikia malengo ya mwaka 2025 ya kuongeza uuzwaji wa zao hilo nje ya nchi likiwa limebanguliwa.
Amesema mkutano utawapa nafasi ya kujifunza Kwa nchi nyingine jinsi walivyoendelea katika uzalishaji na uongezaji thamani wa zao hilo.
“Mwaka jana uzalishaji nchini ulikuwa tani 186,000 na mwaka huu tunatarajia kuzalisha tani 300,000 kutokana na hali nzuri ya hewa tunatarajia ndani ya miaka miwili ijayo kufikia tani 700,000 huku malengo ya mwaka 2030 ikiwa tani milioni moja,”amesema Silinde.
Amesema ili kufikia malengo hayo inatakwa kuwa na wawekezaji wa kutosha na kuongeza thamani ya mazao Kwa sababu nchi ilikuwa ikizalisha Korosho ghafi na asilimia 90 ya Korosho zote zimekiwa zikoenda nchi ya India na Vertinam ikiwa gafi.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara, Exaud Kigahe amesema Wizara hiyo itavutia wawekezaji kwa kuhakikisha asilimia 90 ya zao hilo linauzwa likiwa limebanguliwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudunu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Detopile amesema tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani, sekta ya kilimo imekuwa na Maendeleo makubwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema anamshukuru Rais Dk. Samia kwa kazi kubwa anayofanya ya kuhudumia wananchi hasa wakulima wa korosho.
“Bodi ya korosho inaunga mokono mkakati wa kuwapa pembejeo wakulima na hivyo aliahidi kufuatilia ubora wa zao na kuhakikisha linahifadhiwa katika magahala,” amesema Brigedia Jenerali Mstaafu Mwanjile.