Na Clara Matimo, Mwanza
BAADA ya uwepo wa tatizo la uhaba na mgawo wa maji katika Jiji la Mwanza, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Maji kuongeza uzalishaji kwenye mradi mpya unaojengwa Butimba ili kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.
Dk. Mpango ametoa agizo hilo leo Septemba 14, 2022 jijini hapa baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji Butimba kinachojengwa na mkandarasi Ms Sogea Satom kutoka nchini Ufaransa kwa gharama ya Sh bilioni 69.3 akisimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) ambao ukikamilika utakua na uwezo wa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku na utanufaisha wakazi 450,000.
Amesema inashangaza kuona wakazi wa jiji hilo wanahangaika na kupata shida ya maji wakati wanakaa kando ya Ziwa Viktoria hivyo akaagiza mradi huo ukamilishwe mapema Desemba mwaka huu badala ya Februari, 2023.
“Kutaneni na mkandarasi mumpe maelekezo mahususi ili ukamilike Desemba mwaka huu na muhakikishe wananchi hawa wanapata maji ya uhakika nikiona mnasua sua nitaamua kuja kulia krismasi hapa Mwanza, msithubutu kunizingua maana kabla sijaenda kwa mama (Rais) mtakuwa mmepata habari yenu.
“Sitakubali kutoa ahadi ya uongo mbele ya wananchi hawa, muwasimamie wakandarasi kweli kweli wafanye kazi usiku na mchana,” alisema Dk. Mpango.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais aliipa maagizo manne Mwauwasa katika kutoa huduma bora kwa wananchi wanaotumia huduma ya maji, ikiwemo kuhakikisha wale wanaoishi karibu na chanzo chicho cha Butimba kupewa kipaumbele wakati wa usambazaji wa maji na waliopata ajira walipwe kwa wakati stahiki zao.
Pia, kutochelewesha huduma ya kuunganisha maji kwenye makazi ya wananchi kwa kuhakikisha huduma hiyo wanaipata ndani ya siku saba, kutowabambikizia wateja wao ankara za maji zisizo na uhalisia huku akiwataka Watanzania waliopata nafasi kwenye mradi huo kuwa waaminifu na kutojihusisha na wizi wa vifaa vya ujenzi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema makadirio hadi mwishoni mwa mwaka 2021 mahitaji ya maji katika mkoa huo ni lita milioni 160 kwa siku, ambapo chanzo kilichopo cha Capripoint kinazalisha lita milioni 90 hivyo upungufu uliopo ni lita milioni 70 kwa siku ambao unasababisha Mwauwasa kutoa huduma hiyo kwa mgao hususani katika maeneo ya miinuko mikali na pembezoni mwa jiji.
“Kukamilika kwa mradi huu hakika itakuwa ni faraja kubwa sana kwa wakazi wa mkoa huu tunaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wewe Makamu wa Rais Dk Mpango kwa kutuletea mradi huu,”amesmea Malima.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameahidi kulisimamia agizo la Dk. Mpango kwa kuwasimamia wakandarasi wanaojenga mradi huo ili ukamilike ndani ya kipindi alichoelekeza (Desemba mwaka huu) huku akibainisha kuwa katika kutatua changamoto ya upatikanaji maji Serikali imeiwezesha wizara hiyo fedha za kununua mitambo ili kuchimba visima kila mkoa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga alisema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na benki ya uwekezaji ya Ulaya(EIB) ukilenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Mwanza pamoja na maeneo ya wilaya zinazozunguka jiji hilo.
Naye Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula amesema utekelezaji wa ujenzi wa chanzo hicho ambacho ni kikubwa ni hatua nzuri kwa wakazi wa jiji la Mwanza kwani kukamilika kwake kutakuwa mkombozi kwa wakazi wa jimbo lake.
“Imani yetu wakazi wa Nyamagana chanzo hiki kikikamilika tutakuwa tumepona na tena tumepona sana, tunaishukuru Serikali kwani mbali na mradi huu tunao mradi wa soko kuu na stendi ambayo inajengwa ndani ya jimbo letu, miradi hii ikikamilika itakuwa ni vyanzo vikubwa vya mapato vitakavyowasaidia wananchi kupitia halmashauri yao kusukuma miradi mingi ya maendeleo,” amesema Mabula.