Na Mwandishi Wetu, Arusha
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amesema unahitajika ufadhili unaozingatia jinsia, endelevu na wenye uwiano katika kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi(UNFCCC) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Amesema nchi zinazoendelea zinahitaji zaidi ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kufikia azma ya kuzingatia jinsia katika ufadhili huo.
Halikadhalika ametoa wito kwa washiriki wa mkutano kufanya mijadala ya kina, kubadilishana uzoefu katika mafanikio, changamoto na mafunzo ili kuweza kupata suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ufadhili unaozingatia jinsia.
Amesema kwa kuunganisha maarifa na utaalamu wa washiriki kutoka mataifa mbalimbali kutawezesha kuongeza juhudi za kitaifa na kimataifa na kuharakisha maendeleo katika kufikia malengo ya pamoja ya ufadhili endelevu wa mabadiliko ya tabianchi unaozingatia jinsia.
Makamu wa Rais amesema mkutano huo unapaswa kusaidia katika kuhakikisha ahadi za nchi zilizoendelea za utoaji wa dola milioni 100 kila mwaka zinatimizwa ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya ahadi za nchi hizo za kuwezesha utekelezaji wa mkataba wa Paris.