MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imefuta kesi ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa ya kupinga kustaafishwa kwake na kumtangaza kuwa askofu wa kanisa hilo.
Wiki iliyopita Askofu Mokiwa aliwasilisha barua mahakamani hapo akiiomba mahakama kuiondoa kesi aliyoifungua dhidi ya Askofu Mkuu wa Makanisa ya Anglikana Tanzania, Mhashamu Dk. Jacobe Chimeledya na Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo, akipinga kustaafishwa kwa nguvu ili wakamalizane katika nyumba ya maaskofu.
Akitoa uamuzi mahakamani hapo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, amesema mahakama imeridhia maombi ya kufutwa kwa shauri hilo akitaja sababu kuwa ni kutokana na juhudi zinazoendelea za kutatua mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu, kwa hiyo sasa ruksa kwa mlalamikaji na wadaiwa kumalizana nje ya mahakama.
Askofu Mokiwa alifungua kesi hiyo Februari 22, mwaka huu baada ya kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini yakiwamo kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela.
Aidha, askofu huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa yadi ya kuuza magari.