Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete ameahidi kushiriki katika mbio za hisani za Msoga Half Marathon, zitakazofanyika Juni 29,2024, kwa lengo la kuchangia Sh. milioni 330 za kununulia vifaa tiba ili kuboresha huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya Msonga Wilaya ya Chalinze, mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 14,2024 wakati akizindua mbio hizo, jijini Dar es Salaam, Dk. Kikwete amesema kama avyoshiriki mbio za kuchangia kwa wengine, sasa amepata fursa ya kutoa mchango kwake na kuamini wengine watamuunga mkono.
“Mimi ahadi yangu naomba niwe na afya nzuri, nimejiandaa kushiriki kwa kweli, kama vile ninavyochangia kwa wenzangu nimepata fursa ya kuchangia kwangu. “Niwapongeze kwa wazo hili, nimepongeze Mbunge wa Chalinze Mheshimiwa Ridhwani kwa kubuni wazo la kuwa na hii hospitali,” ameeleza.
Amefafanua kuwa pamoja na kuhitaji milioni 330 kwa ajili ya hospitali ya Msoga lakini zikipatikana zaidi ya hizo itakuwa jambo zuri kwa sababu zitasaidia hospitali nyingine za Wilaya ya Bagamoyo kutokana na uwepo wa uhitaji wa vifaa.
“Mahitaji yapo kwa kweli kuna vitu vingi nimekuwa nikisaidia kwa sababu ni hospitali inayoendelea kujengwa. Bado mahitaji ni makubwa kwa kuwa vituo vya afya ambavyo watoto njiti wanazaliwa ni vingi,” amesema Dk. Kikwete.
Katika mbio hizo zenye kaulimbiu ya ‘Upendo wa Mama na Mwana’ mshindi wa kwanza kilomita 21, wanaume kwa wanawake atajipatia Sh. 1,000,000.