Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk. Dalaly Kafumu pamoja na makamu wake, Vicky Kamata wamejiuzulu nyadhifa zao.
Uamuzi huo wameuchukua baada ya kuwepo kwa sintofamu kati yao na Serikali huku kila upande ukimwona mwenzake ni adui.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, Dk. Kafumu ambaye ni Mbunge wa Igunga (CCM), pia alikuwa tayari kujiuzulu na ubunge, lakini alizuiwa na viongozi wa ngazi za juu wa nchi.
Akitangaza uamuzi wa kijiuzulu mbele ya wanahabari jana mjini hapa, Dk. Kafumu alisema ameamua kujiuzulu kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kamati yake kupewa ushirikiano hafifu na Serikali.
Alisema kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa lakini mara nyingi wamekuwa wakikumbana na changamoto kadhaa kutoka serikalini.
“Tulikwenda Bandari, Arusha na vituo vingi vya uwekezaji lakini pia mtakumbuka wakati tunahitimisha taarifa ya mwaka kwa kweli nilieleza changamoto nyingi ambazo Serikali inazo katika kuipeleka Tanzania katika nchi ya viwanda.
“Kamati iliona inahitaji kuwa na mtazamo wa pamoja zaidi kati yetu na Serikali badala ya kuwa na mtazamo wa mtu mmoja mmoja. Changamoto ni nyingi nyingine ni uelewa wa viongozi na wananchi wenyewe.
“Jambo la viwanda ni la kufa au kupona, nilisema na kuna wengine hawaelewi sawasawa kwa hiyo unaposhauri kuna wengine wanaona tofauti,” alisema Dk. Kafumu.
Dk. Kafumu alisema wakati mwingine walikuwa wanapishana na Serikali na kuonekana kama wanaisema lakini akadai lengo lao lilikuwa ni kuieleza ili kufanikisha mambo.
“Nimeona ni vizuri tunapoanza mwaka wa pili wa bajeti, niyaseme haya maneno kuwa kulikuwa na ushirikiano hafifu miongoni mwa sisi wabunge na Serikali.
“Wakati mwingine unasema jambo mwingine anakuwa tofauti na wewe hii sio sawa acha tukae pembeni tufanye kazi zingine,’’alisema.
Hata hivyo mbunge huyo alisema kutokana na hali hiyo yeye na makamu wake, Vicky Kamata wamepima na kuamua kwa hiyari yao kuachia nafasi hizo.
Mbunge huyo aliitaja sababu nyingine iliyomfanya akae pembeni kuwa ni kukosa muda wa kukaa jimboni kwake hali iliyomfanya kushindwa kuhudhuria vikao vya Baraza la Madiwani ikiwemo Kamati ya Fedha.
“Ukiwa Mwenyekiti unapewa kazi kubwa zingine za kuiwakilisha nchi ambazo napewa na Spika, nimejikuta jimboni napungukiwa nafasi ya kufanya na hii imenifanya nitazame upya kwenye nafasi yangu hii nyeti yenye kuhitaji nchi ifike kwenye viwanda.
“Nimekosa nafasi mimi kama Mbunge wa Igunga ya kukaa na wananchi wangu na kumekuwepo na malalamiko mengi kule ya kwamba, umepewa kazi kubwa umekaa huko huko,” alisema.
Alisema tayari ameshazungumza na Spika wa Bunge, Job Ndugai na kukabidhi rasmi barua yake ya kujiuzulu uenyekiti wa kamati.
“Kama wananchi nimewaacha kidogo nikirudi nitakuwa na uhakika wa kugombea 2020/25 lakini nikiacha, wapo vijana wanapita kule tena kwa nguvu sana hivyo ningependa niwe karibu na wananchi,’’ alisema.
Kuhusina na Tanzania ya Viwanda, Dk. Kafumu alisema Serikali isipotengeneza mkakati wa kuipeleka nchi kwenye Tanzania ya viwanda haitawezekana.
Pia alisema wapo wabunge wengi wazuri ambao wanaweza kushika nafasi hiyo na kuongoza vizuri na kwamba hatua hiyo inaweza kuwakatisha tamaa wajumbe kwa muda na haitakuwa na madhara makubwa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vicky Kamata, alisema katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kazi yao ilikuwa ni kuishauri Serikali kazi ambayo wameifanya.
“Kutokana na changamoto mbalimbali ambazo si vizuri kuzisemea hapa, binafsi nimeona nijiuzulu nafasi hii ili kutoa nafasi kwa wabunge wengine kuongoza nafasi hii,” alisema.
Septemba 5, mwaka huu Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira chini ya Dk. Kafumu ilitangaza kuwakutanisha wadau kujadili mdororo wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilizua maneno huku viongozi wa Serikali wakiishutumu kamati hiyo kuhongwa na wafanyabishara ili watangaze kupungua kwa mizigo bandarini.