29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Chegeni atumwa kumshawishi Lowassa

EdwardLowassaNa Mwandishi Wetu, Mwanza

WAKATI vita ya kuwania nafasi ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete ikipamba moto, baadhi ya wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Ziwa, wamemtaka Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, agombee urais katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Wananchi hao katika kutimiza dhamira yao, wamemtuma Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa, Dk. Raphael Chegeni, kwenda kumshawishi Lowassa ili awanie nafasi hiyo.

Mjumbe huyo wa NEC ya CCM, Wilaya ya Busega, alisema Lowassa anafaa kuwa rais hivyo atakwenda kumshawishi na atamchangia fedha za kuchukulia fomu ya kugombea kwa kushirikiana na marafiki zake ndani na nje ya CCM.

“Kati ya waliojitangaza kutaka wapitishwe na CCM kumrithi Kikwete, bado hatujaona mwenye sifa zinazotakiwa, sasa Dk. Chegeni kwa ushawishi wake tunamtuma akamwambie Lowassa akubaliane na matakwa yetu, achukue fomu ya kuwania urais kwani ndiye suluhisho la kero na changamoto za maisha ya Watanzania,” alisema mmoja wa makada hao kutoka mkoani Kagera kwa niaba ya wenzake.

Dk. Chegeni akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo akiwa jijini Mwanza jana, alisema ameridhia kauli za makada na wananchi hao wa Kanda ya Ziwa.

Dk. Chegeni alisema kwamba, Lowassa bado hajatangaza nia hiyo, lakini atafunga safari kwenda kumshawishi achukue fomu wakati ukifika.

Alisema kwamba, Lowassa amekuwa kimya muda wote licha ya kutajwa kwenye kinyang’anyiro hicho, lakini atamshawishi agombee nafasi hiyo kwa kuwa anaamini ana uwezo wa kuwatumikia Watanzania kutokana na rekodi yake ya utumishi wa umma alipokuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya nne.
Akihutubia maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM mjini Songea mkoani Ruvuma hivi karibuni, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, aliwasihi Watanzania kuanza kuwashawishi wanasiasa wanaowaona wanafaa kuongoza nchi ambao bado hawajajitokeza kutangaza nia yao ya kugombea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Dk. Chegeni alisema kati ya wanasiasa wote waliokwishatangaza nia yao na ambao hawajatangaza nia ya kutaka kugombea nafasi ya urais baada ya Kikwete kumaliza muda wake, haoni mwenye sifa za kuliongoza taifa, bali mtu pekee mwenye sifa hizo ingawa hajatangaza ni Lowassa.

“Nampongeza sana Rais Kikwete ameona wazi wapo watu makini wenye uwezo na sifa ya kumrithi kama Lowassa hajatangaza nia ya kugombea. Wananchi na wana CCM Kanda ya Ziwa wameliona pia na ndiyo maana wamenituma kwake nikamwombe agombee,” alisema Dk. Chegeni

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles