Abdallah Amiri -Igunga
BAADHI ya wananchi wa Kijiji cha Mgazi, Kata ya Lugubu, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wamewatuhumu viongozi wao akiwamo diwani, Magreth Kafumu (CCM) kwa kuuza eneo la hifadhi ya kijiji kwa Sh milioni 25 huku fedha hizo hazijulikani zilipo.
Wananchi hao walitoa tuhuma hizo wakati wakizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki.
Charles Shisho, Idd Juma na Dala Amani walidai kuwa walizuiliwa kufanya shughuli katika msitu huo, lakini cha ajabu mwaka 2016 hadi 2019 msitu huo umeuzwa kimyakimya.
Shisho alidai kuwa walipeleka malalamiko hayo kwa diwani wao, Magreth lakini hakuna hatua iliyochukuliwa na baadaye walibaini naye anahusika kwenye uuzwaji wa msitu huo wa hifadhi ya kijiji.
Pia katika sakata hilo ametajwa Ofisi Mtendaji wa Kijiji cha Mgazi, Masaka Chupa ambaye naye anadaiwa kuhusika katika uuzwaji huo wa msitu.
Mbali na hao, pia wajumbe wa Serikali ya kijiji wamedaiwa kuhusika na uuzwaji huo.
“Jamani waandishi wa habari, suala hili sio majungu. Hata kwa Katibu Kata wa CCM tulishafikisha, nadhani mmefika katika hifadhi hiyo mmeona nyumba zimejengwa, haya mambo ndio anayapiga vita Rais wetu John Magufuli,” alisema Shisho
Naye Katibu wa CCM Kata ya Lugubu, Salimu Mpaki, alikiri kupokea malalamiko ya wananchi wa kijiji hicho kuhusu kuuzwa hifadhi ya kijiji chao na kusema kuwa tayari suala hilo alisharipoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga kwa hatua zaidi.
“Mimi nilishatoa taarifa kwa DC tangu mwaka jana ambapo nimepata taarifa kuwa alishaunda kamati ya ufuatiliaji kuhusu suala hilo, hata tunavyozungumza tayari kamati imemaliza kazi yake,” alisema Mpaki.
Alipotafutwa diwani Kafumu kuhusu tuhuma hizo dhidi yake, alithibitisha kuuzwa kwa msitu huo wa hifadhi ya kijiji na fedha kutumika kuendeshea kesi ambayo walishtakiwa viongozi na mtu binafsi katika Baraza la Ardhi Mkoa wa Tabora.
Naye Mtendaji wa kijiji, Masaka Chupa alikiri kushiriki kuuza hifadhi ya Kijiji cha Mgazi huku akishindwa kutoa ufafanuzi wa matumizi ya fedha hizo na kusema kuwa suala hilo lipo ofisi ya Mkuu wa Wilaya Igunga kwa uchunguzi.
Hata hivyo, Chupa aliwaomba waandishi kutoandika habari hiyo kwa kile alichodai itamletea shida kwani amebakisha muda mfupi ili aweze kustaafu utumishi wa umma.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Igunga, Godslove Kawiche, alisema tayari tume iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya, John Mwaipopo kuchunguza suala hilo imekamilisha kazi yake na wakati wowote itatoa majibu.