29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Diaspora: Tuko tayari kuwekeza nchini kwetu

Seynab Haji Mohammed akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Seynab Haji Mohammed akizungumza na mwandishi wa makala haya.

NA SARAH MOSSI, UPPSALA

MOJAWAPO ya vitu vinavyowaunganisha Watanzania wakiwa nje ya nchi yao ni utaifa na umoja wao katika nchi wanazoishi Ughaibuni. Na ndio maana kila nchi utakayokwenda duniani huwezi kukosa Jumuiya za Watanzania walioamua kujikusanya pamoja kwa lengo moja la kujitambulisha kwa umoja wao lakini pia kuhakikisha wanapeleka maendeleo yao mbele.

Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Sweden ambayo inajulikana kwa jina la Tanzaniska Riksförbundet ni mojawapo ya jumuiya hizo zilizosambaa duniani ambazo mpaka sasa zimeonekana kufanya vizuri katika kufikia malengo yao ya kutambuana na kufikiria namna gani wanaweza kuisaidia nchi yao katika masuala ya jamii na kuinua uchumi.

Seynab Haji Mohammed ameishi nchini Sweden kwa miaka 30 sasa ni Katibu wa Jumuiya ya Watazania waishio Sweden inayojulikana kwa jina la Tanzaniska Riksförbundet.

Hivi karibuni Mwandishi wetu SARAH MOSSI, amefanya mahojiano na Seynab katika Mji wa Uppsala ulioko Kaskazini mwa Jiji la Stockholm. Endelea…

MTANZANIA: Nini kiliwasukuma na kuamua kuwaunganisha Watanzania hapa Sweden na kuunda umoja wenu?

SEYNAB:  Harakati za kuanzisha Jumuiya yetu zilianza mwaka 2010 chini ya aliyekuwa Balozi wakati huo Mohammed Mzale aliyekuwa balozi wetu hapa Nordic alituhamasisha na akatisha mkutano ubalozini tukakutana.

Tumesajiliwa rasmi mwaka 2012 na kuanza kufanya kazi hadi sasa. Tumepita katika uongozi wa wenyeviti wawili, mimi mwenyewe na sasa Mwenyekiti wetu ni Tengo Kilumanga na Makamu wake ni Norman Jason.

MTANZANIA: Ni changamoto zipi ambazo mmezipitia hadi sasa?

SEYNAB: Changamoto yetu kubwa ni kuweza kuwaunganisha Watanzania popote walipo Sweden na kujaribu kuangalia wengi wajiunge katika vyama vilivyoko mikoani na wale ambao hawezi kujiunga katika vyama.

Sasa hivi tuna mpango wa kuitengeneza katiba yetu kwanza tuliitengeneza kwamba wanachama kwanza wajiunge mikoani halafu ndio wanakuwa wanachama katika chama mama.

Tumeamua kubadilisha katiba ili kuona kwamba Je, hawa ambao hawatakiwi kuwa katika vyama vidogo vidogo tutawaweka kuwa wanachama wa namna gani. Hili bado hatujalimaliza.

Hii ndio changamoto kubwa sana kwetu maana si wote wanataka kuwa wenye vyama lakini wapo wengi wanatuunga mkono hiki chama mama.

Wengine wanalipa ada zao moja kwa moja kwetu sisi, hao sasa tunawaita wanachama wa aina gani, maana wanachama hai ndio wale walio katika vyama vya mikoani, sasa hawa tutawaita ni kina nani?

MTANZANIA: Mnawasaidia vipi wale ambao si wanachama hai, lakini wanapata matatizo hapa Sweden?

SEYNAB: Chama chochote duniani, yule aliyelipa ada tu ndiye anayetambulika sasa yule ambaye hakutaka kulipa ada na ambaye amejitenga katika umoja huo, hili hatujaliongelea. Ni ngumu, sasa hapo inahitajika huruma kweli kwa mtu aliyeamua kujitenga mwenyewe.

Jukumu letu sisi sasa ni kuhakikisha tunahamasisha zaidi watu wajiunge katika umoja na hata wale waliojitenga waweze kutambua faida za umoja huu.

MTANZANIA: Ushirikiano wenu na ofisi ya Balozi hapa Sweden ukoje?

SEYNAB: Ushirikiano wetu na Ubalozi ni mkubwa sana na Balozi wetu mpya Dorah Msechu amekuwa karibu na sisi na ametuhamasisha kweli na kila hotuba anayoongeza tunapomuita anasisitiza umuhimu wa umoja huu.

MTANZANIA: Suala la kusaidia wasiojiweza na kupeleka maendeleo katika nchi mliyotoka, hili mnalizungumzia kwa upana kweli?

SEYNAB: Tunalizungumzia sana na lipo kwenye katiba yetu ambayo inasema sisi Watanzania ambao tumeiacha nchi yetu kwa muda mrefu ambao tumepata mawazo mengine katika hizi nchi tunaishi tuhakikishe tunachangia kw ahali na mali. Wengine wanafanya shughuli za kusaidia ‘Organization’ za kule nyumba ambazo ni za Serikali na zisizo za Serikali.

Tunatumia mbinu zote tulizozipata hapa na kuzirejesha nyumbani na tunasisitiza katika mikutano yetu kwamba tunaporudi nyumbani wakati wa likizo zetu wajitahidi kwenda kuhamasisha nyumbani kwa namna moja au nyingine kwa namna yoyote ile hususani katika masuala ya mazingira. Tunahakikisha tunawekeza kule nyumbani na kama hatujarudi tunahakikisha tunasaidia kwa kila namna.

MTANZANIA: Diaspora mlipata kushirikiana vipi na Serikali ya Awamu ya Nne?

SEYNAB: Tulishirikiana sana, nakumbuka Rais Jakaya Kikwete alipokuwa ameanza shughuli zake rasmi kama Rais alikuja hapa Sweden na akaitisha mkutano mkubwa sana katika Hoteli ya Sheraton iliyoko Stockholm na mkutano huo ulihudhuriwa na Watanzania zaidi ya 300.

MTANZANIA: Wewe binafsi umefikiria kurudi nyumbani na kuwekeza?

SEYNAB: Mimi nilishawekeza lakini nipo kwenye development. Na sijawekeza tu nimeshirikiana kikazi, mwaka 2004 ofisi yangu kwa kushirikiana na mimi tulipeleka Development Project nyumbani ya HIV ya kuhamasisha ilikuwa kuanzia mwaka 2004 hadi 2006.

Tulishirikiana na taasisi binafsi ya Kilimanjaro Aids Asociation Centre ambayo mpaka sasa kipo kinaendelea.

Ofisi yangu mimi tunatumia Informal Education kwa ajili ya kuelimisha watu wa chini. Tuliipeleka hiyo project kule nyumbani kuwapa elimu watu wa chini kuweza kupambana na tatizo la HIV.

Kituo hicho mpaka sasa kipo kinaendelea wanakuwapo manesi pale kutoka KCMC wanafanya kazi pale kwa wiki na watu wanakwenda kupewa elimu na kupimwa.

Huo ndio mchango wangu nilioutoa kwa nchi yangu na kulikuwa na åproject nyingine ya teenegers ambao wanatoka Moshi Kilimanjaro katika Shule za Sekondari na wale wa Sekondari wa hapa katika mji wangu ninaoishi mimi wa Uppsala walikwenda pale kuwa na kubadilishana uzoefu.

Walikuwa vijana wanane kutoka Tanzania wasichana wanne na wavulana wanne halikadhalika kutoka Sweden. Hawa wa nyumbani walikaa katika familia za Waswidi. Wale watoto waliotoka Tanzania ni wale waliokuwa wamepoteza watoto wazai wao kwa sababu ya AIDS.

Wale watoto mpaka leo wamekuwa wakisaidiwa na hizo familia na hadi sasa wanasomeshwa na hixo familia na kuwaendelezea maisha yao. Wale watoto wa Kiswidi wao walikwenda kukaa katika shirika la Masista pale Moshi.

Usikose kufuatilia mahojiano haya wiki ijayo ambapo Seynab atazungumza kwa undani masuala ya uchumi na siasa na jinsi wanavyopambana kuhakikisha suala la uraia pacha linafikiriwa kwa mtazamo chanya katika ngazi ya uamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles