27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Demokrasia ijenge Taifa si kulisambaratisha

Na LEONARD MANG’OHA

JAMBO kubwa katika uga wa siasa nchini karibu wiki mbili sasa ni uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mei 10, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuwazuia wakurugenzi (DED) kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Uamuzi huo wa kihistoria unaohusu masuala ya kisiasa nchini, ulifikiwa na Mahakama Kuu kutokana na kesi iliyofunguliwa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, aliyekuwa akiwakilishwa na Wakili Fatma Karume.

Katika hukumu ya kesi hiyo ambayo uamuzi wake ulitolewa na jopo la majaji watatu; Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhajj Masoud na Firmin Matogolo, ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka NEC kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi ya niaba yake.

Pia ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi. 

Pia sheria haijaweka ulinzi kwa NEC kumteua mtumishi yeyote wa umma kuhakikisha kuwa anakuwa huru katika kutekeleza majukumu yake pamoja na vifungu vingine kadhaa.

Msingi wa kesi hiyo kulingana na mlalamikaji ni kwamba vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi kwa sababu wakurugenzi hao huteuliwa na Rais, ambaye hutokana na chama kinachotawala na hata baadhi ya wakurugenzi hao ni wanachama wa chama husika jambo linaloathiri utendaji haki.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Chadema imetoa mapendekezo saba kwa Serikali ili itekeleze vema uamuzi huo wa Mahakama Kuu wa kuifuta sheria inayowapa wakurugenzi wa halmashauri mamlaka ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

John Mrema ni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, ambaye katika mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni ameipongeza Mahakama kwa kusimamia Katiba.

Baadhi ya mapendekezo ya chama hicho kwa Serikali ni pamoja na kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi na kuwe na utaratibu wa kuwapata wajumbe.

Kutokana na tume kutokuwa na vyanzo vya mapato, chama hicho kinashauri uanzishwe mfuko maalumu wa tume mpya pamoja na kuondolewa kwa zuio la tume kushtakiwa.

Mengine ni kuweka utaratibu wa matokeo ya urais kupingwa mahakamani pamoja na haki ya mgombea kukata rufaa, kuweka utaratibu wa mgombea atakayepita bila kupingwa apigiwe kura ya ndio na hapana na mgombea asipofikisha asilimia 50 ihesabiwe ameshindwa.

Pendekezo jingine ni kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika ngazi mbalimbali ili makundi yaliyopo yapate wawakilishi badala ya kupitia kwenye vyama vya siasa.

Licha ya Sheria ya Uchaguzi kuzuia mtu ambaye ni mwanachama wa chama chochote cha siasa kujihusisha na uchaguzi inadaiwa kuwa wapo wakurugenzi 86 ambao ni makada wa chama cha siasa na walishashiriki kugombea nafasi mbalimbali na baada ya kushindwa wakateuliwa kuwa katika wadhinya huo.

Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Aderladus Kilangi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Serikali imewasilisha katika Mahakama ya Rufani kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuhusu uamuzi wake huo.

Dk. Kilangi, anadai kuwapo kwa hukumu hiyo hakutaathiri chaguzi nyingine zijazo zikiwamo za marudio, kwani baada tu ya kuwasilisha taarifa hiyo ya kusudio la kukatia rufaa utekelezaji wa hukumu hiyo husimama, hadi pale rufaa ya Serikali itakapoamliwa.

Kwa kuzingatia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ni wazi kuwa hatua kubwa katika kuelekea demokrasia inayoweza kupunguza minong’ono hasa ile inayohusu kutendeka haki katika chaguzi mbalimbali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya vyama vikionesha kutoridhishwa.

Katika mazingira haya ambayo tume inawatumia wakurugenzi ambao miongoni mwao ni wateule wa Rais, ni lazima wapinzani wapoteze kujiamini na kuhisi ‘kupingwa’ waziwazi katika chaguzi hizo hata kama walishindwa kihalali.

Hukumu hii imekuja wakati kukiwa na vilio vingi vya kutaka tume huru ya uchaguzi miongoni mwa wadau wa siasa, vilio ambavyo mara zote vimekuwa vikihitaji mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji ili kuhakikisha uhuru wa tume.

Kumekuwapo baadhi ya wadau ambao wamekuwa wakipendekeza mathalani Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), wamekuwa wakipendekeza kupatikana kwa tume ambayo muundo wake utaakisi majukumu yake, kwa kuwezesha kuwapo kamisheni itakayoongoza tume hiyo katika utendaji kazi wake na kuwajibika kwa mambo yote ya kisera na kimaamuzi, pamoja na kuundwa kwa sekretarieti ya tume itakayokuwa chini ya mkurugenzi wa tume, kama mtendaji mkuu. 

Kutokana na rais anayekuwa madarakani, kuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi au anakuwa kiongozi wa chama kimojawapo cha siasa ambacho kinasimamisha mgombea, inashauriwa kupunguzwa kwa mamlaka yake ya uteuzi, tofauti na sasa ambapo mamlaka yote ya uteuzi yako chini yake. 

Hapa inapendekezwa kuwa mchakato wa kuwapata makamishna wa NEC, utangazwe, ufanyike usaili, kisha majina hayo yafanyiwe mchujo na kupatikana majina 20, yatakayopelekwa kwa rais ambaye atapendekeza majina tisa yatakayopelekwa bungeni kufanyiwa uchambuzi, kujadiliwa na kisha yawasilishwe tena kwa rais ili amteue mwenyekiti wa Tume hiyo. 

Baada ya uteuzi huo wa Rais atayawasilisha majina hayo kwa Jaji Mkuu ambaye atayatangaza na kuwaapisha makamishna wa Tume. Pia rais atamteua Mkurugenzi wa Tume kutokana na majina mawili yatakayopelekwa kwake na Tume ya Uajiri wa Umma kutokana na mchakato huru na wa wazi wa uajiri. 

Kupitia utaratibu huu, Mkurugenzi wa NEC ndiye atakuwa mtendaji mkuu wa Tume hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Katibu wa Kamisheni ya Tume (Board).

Njia hii inatajwa kupunguza kwa kiasi fulani malalamiko dhidi ya tume, kwa sababu watendaji wake wanapatikana kupitia mchakato wa kawaida wa uajiri.

Lakini wakati mwingine ni vigumu kuyapata haya katika hali ya kawaida ya kukaa katika meza moja ya majadiliano na kuafikiana kwa pamoja kufanya marekebisho ya aina hiyo. Na kwa sababu hilo linakuwa gumu uamuzi kama huu uliotolewa na Mahakama Kuu hivi karibuni ni ushindi muhimu katika kuelekea kupata tume iliyo huru.

Hatua hii ni muhimu kwa sababu wakati mwingine mambo haya ya kikatiba yanapokosa maridhiano ya wadau njia sahihi ya kupata ahueni ni kwenda mahakamani ambako haki inaweza kutendeka na kuleta suluhu katika baadhi ya mambo. Waswahili husema kheri kenda shika, kuliko 10 nenda rudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles