26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dc Maswa ataka wananchi kulinda miundombinu ya maji

Na Samwel Mwanga, Maswa

MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amewataka wananchi wa kijiji cha Sulu kilichoko wilayani humo kulinda miundombinu ya maji ili mradi wa maji ulioletwa na Serikali katika kijiji hicho uweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

Hayo yameelezwa kijjini hapo katika kikao cha Mkuu huyo wa wilaya na wajumbe wa serikali ya kijiji hicho kufuatia watu wasiojulikana kuhujumu mradi huo wa maji kwa kuiba mabomba ya kusafirishia maji.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini wilaya ya Maswa,Mhandisi Lucas Madaha(aliyesimama)akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Serikali ya kijiji cha Sulu wilayani humo jinsi miundo mbinu ya maji ilivyohujumiwa kijijini humo na watu wasiojulikana.(Picha Na Samwel Mwanga).

Amesema miradi  hii ya maji inaletwa katika maeneo mbalimbali ili kutatua tatizo la maji ambalo lilikuwepo katika kijiji hiki ambapo wananchi hasa wanawake waliokuwa wanahangaika kutafuta maji kwa muda mrefu.

“Mradi ya maji kama hii inaletwa kwa lengo la kutatua tatizo kubwa la maji ambalo lilikuwepo na linawaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake wanaotumia muda mwingi kutafuta maji na sasa maji yamepatikana lakini bado wapo watu wanahujumu miundo mbinu ya maji hili halikubaliki,” amesema Kaminyonge.

Aidha, amewatahadharisha wanaohujumu miundombinu ya maji kuwa serikali haitawafumbia macho kuona wananchi wengi wanataabika kwa sababu ya watu wachache wanaohujumu kwa manufaa yao huku akiwataka viongozi wa kijiji hicho kuwa walinzi wa miundo mbinu hiyo.

“Wote wanaohujumu miundombinu ya maji serikali haitawafumbia macho na kwa sasa miundombinu ya maji ikihujumiwa hapa kijiji nitaanza kuwakamata viongozi wa kijiji ambao ni Mwenyekiti wa kijiji na Mtendaji wa kijiji hivyo kuweni walinzi wa miundo mbinu hii ya maj ,”amesema Kaminyonge.

Aidha amewaagiza viongozi wa kijiji hicho kwa kushirikiana na jeshi la polisi kuwatafuta watu waliohujumu bomba la mradi wa maji katika kijiji hicho  kusababisha hasara kwa serikali na wananchi kukosa huduma ya maji.

Amewahamasisha wananchi hao ambao wengi wao ni wafugaji kuchukua fursa hiyo kuunganisha maji kwa ajili ya familia zao ili kuwaacha wanawake waendelee kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi  huo, Meneja wa Wilaya wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa)Mhandisi Lucas Madaha amesema kuwa wakati wanaanza majaribio ya kusukuma maji walibaini kukatwa kwa bomba vipande viwili kila kimoja kikiwa na urefu wa Mita 262.

Mhandisi Madaha amesema kuwa kwa sasa bomba hilo limetengenezwa na upatikanaji wa maji umerejea katika hali yake ya kawaida baada ya bomba lililokatwa kutengenezwa.

“Kwa sasa huduma ya maji inapatikana hapa kijijini baada ya bomba lililokatwa kuunganishwa na vipande vya bomba vilivyokatwa tumeweka vingine hivyo tuwaombe wananchi mtunze hii miundombinu ya maji maana ni kwa manufaa yenu,” amesema Mhandisi Madaha.

Ameeleza kuwa baada ya mradi huo kukamilika, Ruwasa itakabidhi kwa Jumuiya ya Watumiaji wa Maji ambayo itaundwa kwa ajili ya uendeshaji.

 Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Sulu, Marco Malale amesema kuwa kwa sasa wataimarisha ulinzi katika miundo mbinu ya maji katika kijiji hicho na watatoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na jeshi la jadi la Sungusungu kuhakikisha mabomba yaliyoibiwa katika mradi huo wa maji yanapatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles