Raymond Minja, Iringa
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah ametangaza kiama kwa wazazi na walezi wenye tabia ya kuwaoza wanafunzi kwa lengo la kujipatia mali kwa kuwataka kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Akizungumza katika mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya wasichana Namnyaki iliyoko wilayani Kilolo, Asia amesema kumekuwa na wazazi ambao kwa makusudi kabisa wamekuwa wakiwabadilisha watoto wao na ngombe bila ya kuangalia madhara atakayopata baadaye kwa kukosa elimu.
“Mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu kama wanavyopata watoto wengine kwani kumuelimisha mtoto wa kike ni sawa na kuielimisha jamiii hivyo kila mzazi anapasawa kuwajibika kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora itakayokuja kumkomboa hapo baadaye.
“Niwaonye wazazi wote mnaogeuza watoto wenu na ng’ombe kuacha mara moja kwani mtoto wa kike ni nyara ya serikali hivyo tukikubaini kuwa unamuozesha mtoto ambaye anasoma au wewe unajifanya kidume ukampa mimba mwanafunzi jua kuwa wewe unacheza na nyara ya serikali na sisi hatutakuwa na huruma na wewe sisi tutafyekelea mbali bila ya huruma,” amesema.
Aidha, Asia amewataka walimu kuwa na ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa ya
watoto wanaoanza shule lakini mara wanaendapo likizo hawarudi ili waweze kufuatilia na kujua kuwa mtoto huyo amekumbwa na tatizo gani na kama endapo mtoto huyo ameozeshwa basi wazazi au walezi wake wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Awali, akisoma risala Mkuu wa Shule hiyo, Erick Thomas alisema shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo wazazi kuwaachisha shule wanafunzi na kuwaozesha katika umri mdogo jambo linalowanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.