Norah Damian, Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amepiga marufuku wananchi kuchangishwa fedha kwa ajili ya kununulia mafuta ya kijiko cha kutengeneza barabara.
Amesema kijiko hicho hutolewa bure na manispaa na wananchi hutakiwa kuainisha barabara korofi ili zikarabatiwe.
Mjema ambaye yuko kwenye ziara katika kata 13 za jimbo la Segerea kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua, amesema hayo leo Alhamisi Septemba 20, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kinyerezi.
“Wananchi wasichangishwe fedha za mafuta kwa ajili ya greda kwa sababu linapotoka manispaa kuja kwenu tayari linakuwa na mafuta,” amesema Mjema.
Awali Mhandisi wa Manispaa ya Ilala, Justin Magoda, alisema kijiko hicho kilifika katika kata hiyo kuanzia Septemba 14 hadi 19 na kwa sasa kimeelekea Kata ya Bonyokwa.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi walisikika wakisema kijiko hicho hakikufanya kazi hatua iliyomlazimu DC huyo kuagiza kirudishwe tena katika kata hiyo.