Na KADAMA MALUNDE
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro amezitaka taasisi na mashirika yasiyokuwa ya serikali yanayotekeleza miradi ya maendeleo katika jamii kushirikiana na sungusungu, viongozi wa mila na watu maarufu katika maeneo husika kufanikisha miradi yao.
Matiro aliyasema hayo mjini Shinyanga wakati akizindua mradi wa kuzuia ukatili wa jinsia kwa watoto na wanawake.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la lisilokuwa la serikali la The Voice of Marginalized Community (TVMC) linalotoa huduma za jamii kwa vijana, watoto na wanawake na makundi yasiyojiweza.
Matiro alisema taasisi na mashirika mengi yamekuwa yakijisahau kushirikisha viongozi wa sungusungu, viongozi wa mila na hata watu maarufu wakati wa kutambulisha miradi mbalimbali katika jamii.
“Pamoja na kuwapa kipaumbele viongozi wa dini bado mnasahau kushirikisha makundi mengine muhimu kama sungusungu ambao wana nguvu kubwa katika jamii, mkitaka kufanikiwa zaidi washirikisheni watu hao,”aliongeza Matiro.
Aliyataka mashirika yanayotekeleza miradi ya maendeleo kujitambulisha katika jamii badala ya kuanza kutekeleza miradi yao kimya kimya kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza katika jamii.
“Serikali ipo nanyi bega kwa bega, mnapokwama tafadhali tupeni taarifa nasi tutawasaidia kadri tutakavyoweza kwa sababu lengo kuu ni kuwahudumia wananchi wetu kuzuia vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanawake na watoto katika jamii,”aliongeza Matiro.
Awali Mkurugenzi wa TVMC, Mussa Ngangala alisema mradi huo unaolenga kupiga vita vitendo vya ukatili wa jinsia utatekelezwa katika kata tano katika wilaya ya Shinyanga ambazo ni Usanda, Samuye, Nsalala, Tinde na Didia.
Ngangala alisema ili kutekeleza mradi huo kwa ukamilifu shirika hilo litashirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi serikali, dini, wananchi na wadau wengine.
“Matarajio yetu kupitia mradi huu ni kwamba kufikia Januari mwaka 2018 kuwapo mfumo mzuri wa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kutoka ngazi ya jamii hadi dawati la jinsia kwa kushirikiana na maofisa utamaduni, watendaji, maofisa maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii na mashirika mengine,”alieleza Ngangala.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TVMC, Japhet Daud alisema kupitia mradi huo itaibuliwa mijadala kuhusu vitendo vya ukatili wa jinsia kupitia matamasha, michezo, ngoma za asili, kutoa elimu na mbinu nyingine kadha wa kadha.