*Vijana waandamana kusindikiza mwili wake, vilio kila kona
*Rais Magufuli atoa ndege moja
EVANS MAGEGE Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
RUGE aisimamisha Dar kwa zaidi ya saa tatu, ndivyo unavyoweza kusema, baada ya jana maelfu ya wananchi kujitokeza kuulaki mwili wake ukitokea Afrika Kusini.
Mazingira ya Ruge Mutahaba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media,
kulisimamisha Jiji la Dar es Salaam yalianza kuonekana jana saa tano asubuhi baada ya wananchi wengi kujitokeza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Gazeti hili lilishuhudia makundi ya vijana na watu wazima wakimiminika kwa wingi katika eneo hilo hali ambayo ilishuhudiwa katika barabara zote ambazo ulipita msafara wa gari lililobeba mwili wake.
Njia ndefu kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Tazara, Buguruni, Ilala Boma karibu kabisa na soko linalotumiwa na wafanyabiashara maarufu kama Machinga, Magomeni, Morocco Hotel, Sinza Kijiweni, Makao Makuu ya Ofisi yake ya Clouds, nyumbani kwao Mikocheni yalishuhudiwa makundi ya watu mbalimbali. Waendesha bodaboda waliungana na msafara wa gari lililobeba mwili wa Ruge ambao ulikuwa umeambatana na magari mbalimbali.
Wanafunzi, wasanii, vijana na wafanyakazi wa kampuni mbalimbali ambao walifika katika eneo la kupakulia mizigo la Swissport ambalo lipo ndani ya kiwanja cha ndege cha Mwalimu Julius Nyerere na wengine waliojitokeza katika maeneo ambayo msafara huo ulipita, hali ilikuwa ni ya simanzi, wapo walioshindwa kuzuia machozi yao.
Wengine walionekana kutembea kwa miguu kando ya gari lililobeba mwili wake na kuchungulia mahali alipolazwa.
Simanzi zaidi ilionekana pale saa 11:00 jioni wakati mwili wake ulipofikishwa katika majengo ya Clouds alikokuwa akifanyia kazi kwani wafanyakazi wenzake walishindwa kujizuia kwa vilio.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, ni miongoni mwa viongozi wa Serikali waliojitokeza kuupokea mwili wa Ruge.
Hali ya ulinzi si tu ilionekana katika eneo la Terminal One ulikoshushwa mwili wake, bali katika maeneo yote zaidi askari wa usalama barabarani wakiwa ni miongoni mwa watu walioshiriki kuhakikisha usalama.
Awali, wakati msafara wa kuondoa mwili wa Ruge kutoka Terminal One ukianza saa 10.05 jioni itifaki ya kupanga msafara ikifanyika, moja ya gari lililokuwa kwenye msafara wa wanafamilia lilimgonga na kumvunja mguu mwandishi wa Clouds.
NYUMBANI KWAO
Awali mapema jana kabla ya mwili wa Ruge haujawasili nyumbani kwao Mikocheni, viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, dini na wasanii waliendelea kujitokeza, kuomboleza kifo chake.
Waliojitokeza jana ni pamoja na
aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Dk. Kitila Mkumbo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James na wasanii mbalimbali akiwamo mkongwe, Nguza Viking.
Viongozi wengine ni Mbunge Magreth Sitta, Mwantumu Mwahiza, Mchungaji Josephat Gwajima,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbulu, Hudson Kamoga ambaye aliwahi kuwa mtangazaji katika kipindi cha 360 Clouds TV.
Msemaji wa Familia, Annick Kashasha, alisema mwili wa Ruge ambao jana ulihifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, utaagwa leo katika viwanja vya Karimjee.
Jumatatu mwili huo utasafirishwa kwenda Kijiji cha Kiziru nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera nyumbani kwa baba na mama yake ambako utazikwa Machi 5.
ATCL WATOA NDEGE
Kutokana na msiba huo, Msemaji wa familia, Kashasha, alisema Rais Dk. John Magufuli, ametoa ndege moja ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) itakayobeba mwili wa marehemu na ndugu.
Aidha, ATCL imeanzisha safari mbili za ndege kwenda mkoani humo kwa wale watakaokuwa tayari kuhudhuria mazishi kwa gharama ya Sh 650,000 kwenda na kurudi.
Ndege moja itaondoka kesho huku nyingine ikitarajiwa kwenda huko Jumatatu asubuhi na kurejea Jumanne.
WAMZUNGUMZIA RUGE
Mwanahabari mkongwe na aliyepata kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, kama ilivyo kwa wengine naye amezungumza jinsi alivyomfahamu Ruge tangu mwaka 1999.
Alisema alikuwa ni Meneja wa Clouds aliyejihusisha na maudhui na alifanya kazi kwa karibu na vyombo vingine na kwamba yeye alimfahamu tangu mwaka 1999 kilipoanzishwa kituo cha redio cha Clouds Media huku akiwaomba waandishi kutoka vyombo vingine kufuatilia vipindi vinavyorushwa na kituo chao na kuwapa mawazo.
“Wakati ule kulikuwa na watangazaji kama Lady Jaydee, Ray C. Ninachokiona, nimeifuatilia Clouds Ruge akiwa mgonjwa wamejitahidi kuendeleza falsafa yake. Pengo kubwa lipo katika ubunifu, wanaweza kuendeleza falsafa yake ila ule u-Ruge hautatokea,” alisema Kibanda.
Alisema kwa sababu binadamu huzaliwa na kufa, hivyo watapatikana na kufanya yale ambayo ameyaacha ila pengo lake litabaki.
Kwa upande wake Mwanamuziki, Nguza Viking, alisema Ruge alikuwa mtoto wake katika mateso ya kifungo chake alikuwa ni shahidi yake na hawezi kusema mengi.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema tumempoteza mtu aliyeunganisha jamii.
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, alisema tukio la Ruge ni la kusikitisha kwa sababu ameondoka kabla nguvu kazi yake bado haijatumika vizuri.
“Kwa maneno machache naweza kusema taa ya Clouds imezimika gizani kwa hiyo wajue wanatoka vipi gizani.”
Alisema sababu za kufa zipo nyingi, anaweza kufa kwa sababu umri umefika yaani ametumika sasa anaenda kupumzika, sababu ya pili ni kukatizwa na watu na kwamba anajua wapo ambao wanawashwa kukataa kuwa mtu hawezi kukatizwa.
“Mfano ni Yesu alikatizwa uhai wake na watu na sababu ya tatu ni ugonjwa mtu anaugua na kufa,” alisema Gwajima.