29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Dar yaongeza mwamko wa uandikishaji watoto darasa la kwanza

*Watoto 2,000 waandishikishwa kuanza kwa mwaka 2024

Na Patricia Kimelemeta, Mtanzania Digital

Watoto zaidi ya 2,000 wameandikishwa kujiunga na darasa la kwanza kwa Mwaka 2024 ambao ni kati ya umri wa miaka sita na saba kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Mwalimu Abdul Maulid amesema kuwa, idadi hiyo inaongezeka siku hadi siku kwa sababu zoezi la uandikishaji bado linaendelea na kwamba kati ya hao, wapo watoto wenye ulemavu.

Amesema kuwa, kuna baadhi ya watoto walipelekwa kwenye shule za watu binafsi kwa ajili ya kujifunza wakiwa madarasa ya awali, hivyo basi, baadhi yao wanaweza kuletwa kwenye shule za Serikali kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza.

“Tunaendelea na zoezi la kusajili watoto wa darasa la kwanza, na wale wa awali, tunaamini idadi hiyo itaongezeka kwa sababu muda bado upo na kwamba mwamko imekua mkubwa kwa wazazi kuja kuwaandikisha watoto wao,” amesema Mwalimu Maulid.

Ameongeza kuwa, awali, wazazi wa watoto wenye ulemavu wamekua wakishindwa Kuja kuwaandikisha watoto wao kwa ajili ya kusoma, lakini kipindi hiki ni tofauti, wazazi wengi wamekua na mwamko na kuwaleta.

“Kuna baadhi ya wazazi waliwapeleka watoto wao kwenye shule binafsi kujifunza wakiwa madarasa ya awali, hivyo basi na wenyewe tunaamini wanaweza kuletwa kwenye shule zetu za serikali kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza mwakani,” amesema.

Ameongeza kuwa, katika usajili wa mwaka huu kuna ongezeko la zaidi ya asilimia 60 ya wazazi kuleta watoto kuwaandikisha, hii inatokana na mwamko uliopo wa kuwaandikisha watoto ili waweze kupata elimu.

Ameongeza kuwa, mkakati uliopo ni kuendelea kuwahamasisha wazazi kuja kuwaandikisha watoto ili waweze kujiunga na darasa la kwanza kwa wenye umri kuanzia miaka sita na saba na wale wadogo wandikishwe kwenye madarsa ya awali ili waweze kujifunza.

Amesema kuwa, anaamini zoezi hilo litafanikiwa kwa sababu wanashirikisha maofisa elimu kata pamoja na wadau wengine kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili watoto wenye umri wa kuanza shule waandikishwe kwa sababu wazazi wa siku hizi wana mwamko wa elimu na ndomana hata idadi ya watoto wanaosajiliwa shuleni imekua ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Amesema kuwa, serikali imeendelea kuongeza idadi ya walimu wenye sifa ambao watafundisha darasa la kwanza na madarasa ya awali ili kuhakikisha wanawajenga watoto Katika utimamu wa mwili na akili.

“Katika mkoa wetu, darasa la kwanza na la awali ni yale madarasa maalumu yanayozungumza ambayo ndio madarasa yanayowafaa kutokana na umri wao na miongozo iliyotolewa na serikali, lengo ni kuwavutia watoto wetu kwa sababu ni wadogo sana na wanapenda kucheza waweze kusoma katika mazingira bora na rafiki,” amesema.

Ameongeza kuwa, licha ya kuongezeka kwa idadi ya walimu, lakini pia serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuhakikisha watoto anajifunza katika mazingira rafiki.

“Hawa ni watoto wadogo wenye umri kuanzia miaka sita hadi saba, wanahitaji mazingira rafiki ikiwamo choo na njia maalum ya kuingia madarasani ambayo pia utawasaidia hata wale watoto wenye ulemavu, ndomana mkoa wetu umeweza kuboresha miundombinu ya vyoo, sehemu ya kuchezea na madarsa ili kuwavutia watoto waweze kujifunza katika mazingira bora,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kalaghe amesema kuwa, licha ya kuwepo kwa ongezeko la watoto wanaoanza darasa la kwanza na awali, bado ndogondogo ambazo serikali inabidi iendelee kuzifanyia kazi hasa katika baadhi ya mikoa.

Dk. Kalaghe amesema kuwa, baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa walimu, vitendea kazi na miundombinu.

“Licha ya serikali kuendelea kuajiri walimu lakini idadi iliyopo haijitoshelezi kutokana na mahitaji, kuna baadhi ya mikoa walimu wenye sifa ya kufundisha watoto hawa ni wachache na hata miundombinu sio rafiki,” amesema Dk. Kalaghe.

Ameongeza kuwa, serikali inapaswa kuendelea kuajiri walimu wenye sifa, kuboresha miundombinu ya shule pamoja na vitendea kazi ikiwamo vitabu na vifaa vya michezo ya kujifunzia.

Amesema kuwa, lakini pia serikali inapaswa kuendelea kushawishi wazazi kushiriki kwenye utengenezaji wa vifaa kwa ajili ya kujifunzia kwa watoto wao ambavyo baadhi yao vinaweza kutengenezwa kwa mikono kwa kutumia zana duni zinazopatikana kwenye mazingira husika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kaya Foundation, Piliana Ngome amesema kuwa, Serikali ijitahidi kuboresha mazingira ya watoto wenye ulemavu ili waweze kusoma katika mazingira rafiki.

“Shule nyingi za serikali watoto wenye ulemavu hawana mazingira rafiki ya kujifunzia, kuanzia miundombinu ya choo hadi njia ya kuingia madarasani, hivyo basi ni vema kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inaboreshwa ili watoto waweze kujifunza vizuri,” amesema Ngome.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema kuwa, serikali inapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa watoto wadogo wakiwamo wenye ulemavu.

“Shule zetu nyingi za serikali watoto wadogo na wale wenye ulemavu hawana mazingira bora ya kujifunzia, jambo ambalo linachangia baadhi yao kutopenda kusoma, hivyo basi wanapaswa kutafuta wadau mbalimbali ambao wanaweza kuwasaidia hata kuboresha majengo au kuwatengenezea vyoo vya kisasa ambavyo vitatumiwa na watoto wadogo,” amesema Rehema Mohamed (29) mkazi wa kunduchi.

Ameongeza kuwa, mlundikano wa watoto katika shule za serikali kunachangia mmomonyoko wa maadili, watoto wadogo wanajikuta wanajifunza vitu visivyofaa.

“Baadhi ya watoto wa siku hizi wameharibika, wakubwa wanawafundisha hawa watoto wa wadogo wa darasa la kwanza na la awali ambao hawajui chochote na wenyewe wanajikuta wapo kwenye mkumbo, hivyo basi juhudi za ziada zinahitajika ili kuwanusu na hatari zinazoweza kujitokeza,” amesema Mohamed.

Ameongeza kuwa,wazazi, walimu na jamii kwa ujumla, wana wajibu wa kuwalinda watoto ili kuwaepusha na madhira yanayoweza kuwahatarishia maisha yao.

Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya mwaka 2021/26 ambayo imelenga kuongeza kasi ya mafanikio yanayopatikana katika huduma za Programu hiyo katika afua tano za afya, elimu, malezi yenye mwitikio, lishe, ulinzi na usalama.

Programu hiyo itasaidia kuboresha uratibu wa huduma kwa kuimarisha utekelezaji wa Sheria na Sera zinazohusu masuala ya MMMAM, Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2008, Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka 2008, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ambazo kwa pamoja zinashughulikia mahitaji ya mtoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles