AVELINE KITOMARY– DAR ES SALAAM
DAKTARI bingwa katika Kitengo cha Uti wa Mgongo, Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk. Angela Lameck amesema matumizi ya pombe yanaweza kusababisha watu kupoteza kumbukumbu katika umri wa utu uzima.
Amesema sababu zingine za kupoteza kumbukumbu wakati ya utu uzima ni mtindo mbaya wa maisha unaosababisha magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaweza kuathiri ubongo.
Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki, Dk. Angela alisema kuwa ni bora watu wakazingatia mfumo bora wa maisha wakiwa vijana kwani hiyo itasaidia kutokupunguza kumbukumbu kwa kiwango kikubwa.
“Kiwango cha kumbukumbu hutofautiana kulingana na umri wa mtu, ukiwa na miaka mitano kiwango chako cha kutunza kumbukumbu ni tofauti na ukiwa na miaka 19 au 25, seli za ubongo kama zilivyo seli zingine za mwili, kuna kipindi zinazalishwa sana na kipindi zinakuwa hazizalishwi kwa kiwango cha juu na kuna kipindi zinaanza kufa.
“Kwa hiyo utake usitake wakati wa uzee lazima kutakuwa na uwezekano wa kumbukumbu kupotea japo kiwango kinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kutokana na mtu mwenyewe.
“Pia seli za ubongo zinaweza kutofautiana katika ufanyaji kazi. Tunaweza tukawa tunafanana, lakini wewe unaweza ukawa na asilimia 60, mwingine 50 na mwingine 30 ya ufanyaji kazi,” alisema Dk. Angela.
Alisema kila mtu akifikisha umri wa utu uzima ni lazima kiwango cha kumbukumbu kitapungua, lakini kuna tofauti ya viwango kati ya mtu mmoja na mwingine.
“Kwahiyo kila binadamu akishafikia umri wa utu uzima anapoteza kumbukumbu, kuanzia miaka 50 huwa tunatarajia kwamba uwezo wa kufikiri hautakuwa sawasawa na kijana wa miaka 25 hadi 30.
“Sababu za viwango kutofautiana ni athari katika ubongo, mfano magonjwa, matumizi ya vilevi huweza kuathiri sehemu za utendaji kazi wa ubongo, hivyo mtu ambaye hatumii ubongo wake hauwezi kufanana na mtu aliyetumia wakati wa ujana wake,” alisema Dk. Angela.
Alisema kuwa yapo matatizo yanayoweza kutokea katika ubongo kama majeraha yanayotokana na ajali na uvimbe ambavyo huweza kupunguza kiwango cha kumbukumbu kadiri umri unavyosonga.
Dk. Angela alisema msongo wa mawazo hauwezi kusababisha kiwango cha kumbukumbu kupungua kutokana na suala hilo kuwa la muda na kuweza kudhibitiwa kulingana na mazingira.