Na ASHA BANI – Dar es Salaam
VURUGU kubwa zimetokea katika mkutano wa viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam baada ya kuvamiwa na genge la watu wanane waliokuwa na silaha za moto.
Watu hao waliingia ndani ya chumba cha mkutano huo na kuwapiga viongozi wa CUF na waandishi wa habari.
Tukio hilo lilitokea jana saa 5:10 asubuhi katika Hoteli ya Niva iliyopo Mabibo, wakati Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Juma Nkumbi, alipokuwa akielezea matukio yanayoendelea wilayani kwake, huku akidai kuwa ni kinyume na katiba ya chama hicho.
Akiwa katikati ya mkutano huo, ghafla waliingia watu wanane wakiwa wameziba nyuso kwa vitambaa usoni na walivamia meza kuu waliyokuwa wamekaa viongozi hao na kuanza kuwashambulia kwa mapanga na mikanda, huku mmoja wao akiwanyooshea bastola.
Hata hivyo, bastola hiyo ilipokonywa na kuangushwa chini na mwanachama mmoja anayemuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Maalim Seif waliumizwa kwa kupigwa na wavamizi hao, huku waandishi wa habari licha ya kujitetea, lakini nao waliambulia kipigo.
Waandishi wa habari waliojeruhiwa ni Fred Mwanjala wa Channel Ten ambaye pia aliharibiwa kamera yake, Merry Geofrey (Nipashe) aliyeumia sehemu ya mkono na kushonwa nyuzi mbili, Rachel Chizoza (Clouds Fm), Kalunde Jamal (Mwananchi), Henry Mwang’onde (The Guardian), Mariam Mziwanda (Uhuru), Estherbella Malisa (Azam TV) na mwandishi wa habari hii.
Baada ya kundi hilo kuwapiga viongozi hao kwa takriban dakika 10, huku wengine wakikimbia kujiokoa, ndipo wananchi waliokuwapo nje ya hoteli hiyo walianza kurushia mawe magari mawili waliyokuja nayo.
Magari hayo aina ya Prado yalipigwa mawe na kupasuka vioo vyote, huku mmoja kati ya watu wa kundi hilo, akitajwa kwa jina moja la Kaduguda, alikatwa kifundo cha mguu na kuachwa kikining’inia.
Mtu huyo alianza kulia na kulalamika akiomba kuachiwa, huku akisema yeye alibebwa bila ya kujua, huku akidai kuwa alitumwa na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
“Jamani nisameheni, mimi nimetumwa na Lipumba, naombeni mnisamehe jamani,” alilalamika huku akiendelea kulia.
Tukio hilo lililokuwa kama filamu ya mapigano liliwashtua wananchi wa eneo hilo waliokimbilia hotelini hapo, kila mmoja akisema lake, huku wengi wao wakidhani kundi hilo lililovamia ni majambazi kutokana na magari kukimbia na watu hao wakiwa wamejifunika sura zao.
Baadaye saa 5:25, askari polisi wa Kituo cha Magomeni wakiongozwa na Inspekta wa Polisi, Ahobokile Mwakabosi, walifika eneo la tukio na askari wengine kwa gari mbili.
Gari moja lilimchukua mtu aliyekatwa kifundo na kumpeleka Kituo cha Magomeni na askari wengine walichukua maelezo kwa waliojeruhiwa, wakiwamo waandishi wa habari.
Katika hatua nyingine, uharibifu umefanyika katika hoteli hiyo, ikiwamo kupasuka vioo, kuvunjwa kwa viti na kuumizwa kwa baadhi ya wafanyakazi, akiwamo mlinzi wa getini.
Godfrey Sombi aliyewahi kuwa mgombea udiwani wa Kata ya Mburahati, aliyeumizwa kichwani, alisema jambo hilo si la kunyamaziwa kimya.
Alisema vitendo vya uvamizi vimeendelea kutokea siku hadi siku kwa watu kutekwa na kupelekwa kusikojulikana na wengine kujeruhiwa na kama Serikali haitatoa tamko, kunaweza kusababisha mauaji yasiyo ya lazima.
Mlinzi wa getini katika hoteli hiyo, Mandrit Luanda, alisema wavamizi hao walifika wakiwa na magari yakiwa na bendera za CUF na hakuwa na wasiwasi nao.
Alisema waliingia licha ya kuanza kuwatilia shaka kutokana na kuwa na miili mikubwa, lakini baada ya muda mfupi alianza kusikia mapigano yakiendelea ndani ya hoteli hiyo.
“Baada ya dakika 10 walitoka na kukimbia huku wenzao watatu wakijeruhiwa na vioo vya magari waliyokuwa wamepanda vikivunjwa,” alisema.
MKUTANO
Awali kabla ya mkutano huo kuvamiwa, Nkumbi, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Mohamed Mkandu na Ally Makwilo wanajiita viongozi wa Wilaya ya Ubungo ilhali wakijua wanafanya hivyo kinyume na katiba ya chama hicho.
Alisema katika mkutano wao waliofanya Aprili 16, mwaka huu, walitoa matamko makali kwamba ni marufuku kwa kiongozi yeyote kutofautiana na Lipumba na yeyote atakayefanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Nkumbi alisema kuwa hatambui uongozi wa muda wa Ubungo kwa kuwa hakuna kikao chochote halali kilichotoa mwongozo wa uundwaji wa uongozi wa muda wa wilaya hiyo mpya.
Aliwataka wanachama wa Kinondoni wasitoe ushirikiano wowote kwa hao viongozi aliowaita kuwa ni feki.
Pia alisema anaunga mkono tamko lililotolewa na wanachama wa matawi 20 ya Dar es Salaam la kumkataa Lipumba na kumtaka kuondoka katika ofisi Kuu za Buguruni mara moja.
Aliwataka wanachama wa chama hicho waliopo wilaya hiyo kuungana pamoja kuwakataa Lipumba na lile aliloliita kuwa ni genge lake wanaotaka kuua chama na upinzani kwa ujumla.
BAADA YA TUKIO
Taarifa kutoka kwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa CUF, Mbarara Maharagande, ilisema wanalaani vikali kitendo hicho alichokiita si cha kiungwana na hakiashirii nia njema, uvumilivu na uendeshaji wa siasa za kistaarabu.
Alisema kama Jumatano wiki hii, Katibu wa Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu, alifanya mkutano kama huo kwa amani bila bughudha na Watanzania walisikia alichokizungumza, iweje Nkumbi afanyiwe vurugu hizo?
Kwa niaba ya chama hicho, alitoa pole kwa waandishi wa habari waliojeruhiwa katika tukio hilo na kwamba wataendelea kuwa nao pamoja katika kuhakikisha kuwa wanarejea katika hali yao ya afya ili kutekeleza majukumu ya kuwatumikia Watanzania.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kuwakamata wahusika wote wa tukio hilo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa kuwa matukio kama haya yanayofanywa na kundi linalojulikana yamekuwa yakijirudia mara kwa mara, ikiwamo jaribio la utekaji kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Joran Bashange mbali na wahusika wanne kukamatwa eneo la tukio,’’ alisema.
Maharagande alisema inasikitisha kuona polisi wamekalia mashtaka hayo na kushindwa kuchukua hatua za kisheria.
MATUKIO YALIYOWAHI KUTOKEA
Maharagande alisema matukio kama hayo ni mwendelezo wa matukio mbalimbali yaliyowahi kutokea na kusababisha vurugu zisizokuwa za lazima katika mkutano Mkuu Maalumu wa CUF Taifa uliofanyika Agosti 21, mwaka jana.
Alisema tukio la pili ni la utekaji wa wanachama na viongozi wa chama hicho lililotokea Septemba 16, mwaka jana baada ya Bashange kutekwa akitoka nyumbani kwake Mtaa wa Madenge, Buguruni, Wilaya ya Ilala na kupewa RB namba BUG/IR/5937/2016.
Tukio la tatu alisema lilitokea Ofisi Kuu ya chama hicho iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, Septemba 24, mwaka jana baada ya Lipumba na wafuasi wake kuvamia ofisi hiyo, kuvunja mageti na milango ya ofisi, kuwapiga walinzi binafsi wa Kampuni ya Ironsides Security Guard waliokuwa wakilinda hapo na Jeshi la Polisi likatoa RB Na.BUG/RB/8741/2016.
Alilitaja tukio la nne ni la uvamizi na kuvunja ofisi za Wilaya ya Bagamoyo na Mkuranga lilitokea Novemba 4, mwaka jana na Lipumba na wafuasi wake wakilindwa na polisi walikwenda katika ofisi hizo.
Alisema tukio la tano ni la wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi kuzuiliwa kufanya mikutano na kukamatwa huko Nachingwea.
Alilitaja tukio la sita kuwa lilitokea Oktoba 10, mwaka jana baada mkutano kuzuiliwa kufanyika mkoani Tanga.