Na ASHA BANI
-DAR ES SALAAM
CHAMA cha Wananchi (CUF) upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, leo wanatarajia kuzindua jengo jipya la ofisi lililopo eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.
Taarifa za ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa ofisi hizo zitatumiwa na viongozi wakiwemo wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif.
Akithibitisha taarifa hizo, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mbarara Maharagande, alisema uzinduzi wa ofisi hiyo mpya utafanyika wakati wowote kuanzia sasa.
Hatua ya kuzindua jengo hilo imekuja wakati ambapo chama hicho kikiwa katika mgogoro mkubwa wa uongozi uliotokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kumrudisha katika nafasi yake ya uenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba na kisha kutwaa jengo lenye ofisi za chama hicho lililopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
“Tutazindua jengo jipya iwe leo au kesho au muda wowote kuanzia sasa, lakini ni jengo la wabunge wote kufanyia shughuli zao hapo na kupanga mikakati mbalimbali ya kukitangaza na kukiimarisha chama,” alisema Maharagande.
Wakati Maharagande akisema hayo, taarifa ambazo gazeti hili limezipata toka kwa vyanzo vyake ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa jengo hilo pia litakuwa na ofisi ambazo zitatumiwa na viongozi wa CUF akiwemo Maalim Seif mwenyewe.
Kwa muda wa miezi sita sasa pande mbili za uongozi zimekuwa zikilumbana juu ya uhalali wa maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho uliofanyika Agosti mwaka jana ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kumwondoa Profesa Lipumba.
Hatua hiyo ilizua tafrani na hata wajumbe kurushiana masumbwi ndani ya ukumbi hali iliyosababisha kuvunjika kwa mkutano huo.
Siku chache baadaye Baraza Kuu la uongozi lilikutana na kutangaza kumvua uanachama wa CUF Profesa Lipumba jambo ambalo lilipingwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Mutungi ambaye alisema taratibu za kufukuzwa kwa Mwenyekiti huyo hazikufuatwa.
Mapema wiki hii upande wa uongozi wa CUF, chini ya Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Lipumba, ulidaiwa kulamba Sh milioni 369.378 za ruzuku kinyume na utaratibu.
Ilielezwa kuwa fedha hizo zilitolewa ndani ya siku moja katika matawi matatu tofauti ya Benki ya NMB kwa kutumia akaunti ya chama na baadaye kuhamishiwa kwa mtu binafsi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF ambaye hatambuliwi na Msajili, Julius Mtatiro, alisema fedha hizo zilitolewa kutoka Hazina na kupelekwa NMB tawi la Temeke.
Wakati Mtatiro akidai hayo, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya, ambaye yupo upande wa Lipumba, alidai fedha hizo zimetolewa kihalali kama walivyofanya upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambao nao walitoa Sh milioni 80 kupitia Benki ya NBC.
Pamoja na hali hiyo, Mtatiro alisema fedha hizo ziliingizwa katika akaunti binafsi ya mtu aliyetambulika katika muamala kwa jina la Mhina Masoud Omary.
Alisema kwa niaba ya Baraza Kuu la Uongozi la CUF ambalo limemteua yeye kuongoza, hana budi kuwajulisha wanachama kuwa CUF imeibiwa fedha hizo za ruzuku ambazo alidai zimetoroshwa na watu wasiojulikana.