Na KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR
Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar, kimesema hakiungi mkono kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hashim Issa Juma, kwamba endapo CUF kitavurugika watawapokea wabunge wote kugombea kwa tiketi ya chama chao pamoja na kumpa nafasi Maalim Seif kuwania urais.
CUF imesema kauli hiyo iliyotolewa na Issa haijawahi kupata baraka wala kujadiliwa kwenye kikao chochote katika chama chao.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana katika ofisi za CUF zilizoko Mtendeni mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui, alisema kauli hiyo ni ya mtu binafsi.
Mazrui alisema CUF kama miongoni mwa wadau wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kupitia umoja huo hawajawahi kuzungumzia jambo lolote kuhusu viongozi wao kuhamia Chadema na kuwania nafasi za uongozi.
Alisema suala la viongozi CUF kuhamia Chadema ni jambo lisilowezekana kwa chama chao kilichokomaa kisiasa.
Marzui alisema pamoja na dhoruba kali na misukosuko ambayo CUF na viongozi wake wanapitia kwa sasa na katika vipindi vyote vya siasa zake tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza mwaka 1995, lakini bado hakijakata tamaa kuingia katika chaguzi nyingine na kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa.
“Bado dhoruba ni kali, lakini chombo kina nahodha madhubuti na chombo kinakwenda vizuri, na tunaamini baada ya muda mfupi chombo kitavuka katika mkondo huu.
“Chama chetu kitasimama tena upya na kitaweza kukabiliana na chaguzi zozote zitakazojitokeza nchini, suala la kuhama na kuhamia Chadema katika chama chetu hakuna,” alisisitiza Mazrui.
Aidha, Mazrui aliwataka wananchi na wanachama wa CUF kuwa wavumilivu na kutoweka akilini kauli ya aina hiyo kwa kuwa lengo la CUF ni kuhakikisha inamkomboa Mzanzibari.
Akizungumza kwa njia ya simu, Msemaji wa CUF visiwani Zanzibar, Salum Dimani, alisema CUF haijaweka ndoto za kuvunja chama chake.
Alisema wao wanaamini chama chao ndio suluhisho pekee la Watanzania.
Dimani alisema si sahihi kwa Chadema kuzungumzia uamuzi huo, kwani migogoro au kesi zinazoikabili CUF, chama hicho kitahakikisha kinashinda.
“Maalim Seif, ambaye ni mwanasiasa mkongwe hana nia ya kujiunga na chama kingine na tunaamini kesi yetu tutashinda na chama chetu kitakuwa imara,” alisema Dimani.
Alisisitiza kuwa, CUF itahakikisha imemaliza hitilafu zote zinazoikabili na kuingia katika chaguzi zijazo hadi kuona kwamba ushindi umepatikana kutoka kwa watawala wa kikoloni, CCM.
Kauli hiyo ya CUF upande wa Zanzibar imekuja baada ya wiki hii Baraza la Wazee wa Chadema kutangaza hadharani kumkaribisha Maalim Seif kuwania urais mwaka 2020 kupitia chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, Issa, alisema kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, wameona kuna kila sababu ya Maalim Seif kuhamia katika chama chao na kwamba tayari wamefanya naye mazungumzo ya awali.
“CUF na Chadema ni kitu kimoja, CUF ikipanguka Zanzibar, Chadema tunachukua nafasi na Maalim atachukua nafasi yake ile ile ya kuchukua fomu ya urais Zanzibar pamoja na wabunge wake wote watachukua fomu kwa tiketi ya Chadema.
“Sisi ndio wazee wa chama, hatuogopi chochote, hatuna siri, ajenda zetu ziko wazi kwamba huu ndio mpango wetu, tunajiamini tunachosema na ndicho kitakachokuwa,” alisema.
Kabla ya Mazrui na Dimani kujibu kauli hiyo, sasa mara tu baada ya Issa kutoa kauli hiyo Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma upande wa Maalim Seif, Mbarara Maharagande, alisema Septemba 2, mwaka huu wakati wa kikao cha madiwani na wenyeviti wa mitaa wa Dar es Salaam, Maalim Seif aliweka wazi msimamo wake kuhusu CUF.
“Maalim (Seif), alisema hakuna sababu ya kufikiria plan B (mkakati) nje ya CUF na imani yake ni kwamba mashauri yaliyopo mahakamani tutashinda pamoja na kupigania haki ya kupokwa ushindi wa urais Zanzibar.
“Kwa hali hiyo, CUF itakuwa imara zaidi. Chadema ni washirika wetu katika Ukawa na tunathamini nia yao ya kushirikiana. Suala la Katibu Mkuu kujiunga Chadema kwa sasa hatujafikiria na hata likifikia, vikao vya chama ndiyo vitaamua.
“Kwa maana hiyo hata baada ya kumalizika kwa mashauri haya, Maalim Seif kama atataka kugombea urais mwaka 2020 basi atagombea kupitia CUF,” alisema Maharagande.
MGOGORO WA CUF
Mgogoro uliopo ndani ya CUF ulianza baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kujiuzulu nafasi yake Agosti 2015, wakati ambao chama chake kilikuwa kikimhitaji kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.
Sababu za Profesa Lipumba kuchukua hatua hiyo ni kutokubaliana na uamuzi wa vyama washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kugombea nafasi ya urais.
Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye kabla ya majibu ya barua yake ya kujiuzulu kukubaliwa au kukataliwa, Agosti mwaka juzi, Profesa Lipumba alitangaza kuirejea nafasi yake na ndipo kulipoanza mgogoro ambao unakitafuna chama hicho hadi sasa.
Profesa Lipumba anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kama Mwenyekiti halali wa chama hicho.
Hata hivyo, CUF upande wa Maalim Seif ililazimika kuunda Kamati ya Uongozi iliyokuwa ikiongozwa na Julius Mtatiro, ambaye hadi anaondoka katika chama hicho hakuwahi kutambuliwa kama kiongozi halali.
Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili umesababisha kufunguliwa mashauri zaidi ya matano Mahakama Kuu, huku kila upande ukisubiri uamuzi wa nani atatambuliwa kama kiongozi halali.