30.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

CRDB KUWEZESHA UWEKEZAJI VIWANDA TANZANIA

Mkurugenzi Mtendaji CRDB, Dk Charles Kimei.
Mkurugenzi Mtendaji CRDB, Dk Charles Kimei.

Na Mwandishi Wetu,

BENKI ya CRDB imepata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa kiasi cha dola milioni 150 zaidi ya Sh bilioni 300 kwa kukopesha wale wanaotaka kujenga viwanda.

Viwanda hivyo vitasaidia kufikia azma ya Serikali ya nchi kuwa ya uchumi wa kati itakapofikia mwaka 2025.

Serikali ya Tanzania inapata faraja inapoona taasisi nyingine zinajitokeza kujaribu kusaidia nchi ifikie malengo yake.

Kutokana na maendeleo hayo Benki ya CRDB imejipanga kutoa mikopo mingi zaidi mwakani ili kuwawezesha Watanzania wengi kuanzisha viwanda.

Akizungumza na vyombo vya habari mwezi uliopita katika maonyesho ya maendeleo ya viwanda, Meneja wa akaunti, Nashon Chacha, alisema wamepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo Afrika ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 250 ambazo zitawawezesha kutekeleza nia yao hiyo.

“Kutokana na fedha hizo toka AfDB  tunatarajia kutoa mikopo mingi zaidi mwakani, 2017 kuliko mwaka huu,” alisema.

Chacha alisema benki hiyo ina mikopo ya aina mbalimbali kwa wateja wao ikiwa ni pamoja na ile inayotolewa kwa watu katika vikundi na pia ya mtu mmoja moja kulingana na mradi anaotaka kuufanya na makampuni.

“Tunatarajia sasa watu wanaelewa Rais Dk. John Magufuli anataka nini na sisi tunajipanga zaidi kwa mwakani ili kufanya biashara na watu  ambao wako tayari kuanzisha na kuendeleza miradi yao ikiwamo viwanda,” alisema.

Meneja wa akaunti huyo alisema hiyo ni fursa ambayo watu wanatakiwa kuitumia ili waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo na hata vikubwa.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa katika kuwakopesha watu ni ukosefu wa elimu ya ujasiriamali ambapo watu wengi wakishapewa mikopo hawajui namna ya kuifanyia kazi miradi yao.

Rungwe wachangamkia fursa

Katika maendeleo mengine kuhusu suala la uchumi wa viwanda, huko Rungwe wadau wa maendeleo wilayani humo wamedhamiria kuongeza viwanda vidogo kutoka saba vya sasa hadi 70 kuanzia mwakani.

Hili ni azimio lililofikiwa kwenye kongamano lililotathmini maendeleo wilayani Rungwe mkoani Mbeya chini ya mada: ‘Tulikotoka, tulipo na tunakokwenda’ lililowashirikisha wataalamu na wajasiriamali wa ndani na nje ya wilaya.

Kongamano hilo lilifanyika mjini Rungwe hivi karibuni na Mhadhiri wa Chuo cha Biashara na Ujasiriamali, Exaud Mwakihaba, amesema wilaya hiyo ina rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vyema zitawaongezea wananchi kipato cha uhakika.

Mwakihaba amebaini kuwa malighafi  zilizopo wilayani Rungwe zinatosheleza mahitaji ya kuanzishwa viwanda vidogo 70 hadi 700 kadiri ya uzalishaji unavyokuwa.

Mjasiriamali mmoja kutoka Tukuyu, amesema wakazi wa Rungwe wanazalisha maziwa, ndizi, mboga na miti ambayo ni mazao yanayoweza kutumika viwandani kama malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine hivyo ameiomba Serikali iwasaidie kwa kuwapa utaalamu na mitaji.

Huo ulikuwa ni mwendelezo wa kile  Ofisa Tawala wa Wilaya,  Eliud Mwandemele, ambaye alisema kwenye ufunguzi wa kongamano hilo kwa kuwataka wadau hao kujua idadi ya wakazi, shughuli za uzalishaji na kipato cha mtu mmoja mmoja kwa mwaka.

Ofisa Mipango na Uchumi wa Wilaya ya Rungwe, Daniel Mwakitalu, alisema wastani wa kipato ni wa Sh milioni 1.7 kwa mwaka ambacho ni kidogo sana.

Mwakitalu alisema ikilingaishwa na uzalishaji uliopo wilayani humo, kiasi hicho cha fedha ni kidogo.

Wilaya ya Rungwe ina ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha mazao mbalimbali  ya chakula na biashara, pia ni miongoni mwa wilaya zinazolima chai kwa wingi.

Wakati huu kumezuka Chama cha Ushirika wa Rungwe zao la matunda ya parachichi ambayo hutumika kama tunda, dawa na kutengeneza vipodozi  na takwimu zinaonesha kuwa eka moja ina uwezo wa kuzalisha mazao yenye thamani ya dola milioni 13.

Kutokana na maendeleo haya Wilaya ya Rungwe inategemewa baada ya miaka michache itakuwa na uchumi mkubwa kutoka zao hilo na hivyo kufanikiwa azma yao ya kuanzisha viwanda vingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles