Na FARAJA MASINDE
LICHA ya janga la virusi vya corona kuendelea kuitikisa dunia, bado haijawa sababu ya kusimama kwa shughuli mbalimbali za kila siku zikiwamo zile zinazochangia kukua kwa uchumi.
Kama tunavyofahamu kwamba hata Rais Dk. John Magufuli, kwa nyakati tofauti kila anapopata fursa ya kuzungumza na Watanzania amekuwa akihimiza kuweka mbele mawazo ya kuchapa kazi na kuyapa kisogo yale yanayohusu corona.
Mfano, katika hotuba yake ya Machi 22, mwaka huu, alipohudhuria Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padre Onesmo Wisi na kuwataka waumini wasiogope kwenda kanisani na msikitini kumuomba Mungu wao kwa sababu ya corona.
“Watu tusitishane, kila ugonjwa una mahala pake inawezekana huku ukapita kama upepo, tuchape kazi tuendelee kumuomba Mungu, kwa Mungu haka kaugonjwa ka corona ni kadogo,” anasema Rais Dk. Magufuli.
Hakuna shaka hata kidogo kwamba hilo limeendelea kutekelezwa kwani tunaendelea kushuhudia namna ambavyo biashara na shughuli mbalimbali zinavyozidi kuchanja mbuga kwa mbinu tofauti.
Ni bayana kwamba kulingana na namna biashara hizi zinavyoendelea kufanyika kwa lugha rahisi unaweza kusema kwa uwazi bila hata kumung’unya maneno kwamba corona imeweza kuibua fursa mpya za ufanyaji biashara tofauti na awali.
Licha ya kwamba mbinu hizo zingeweza kufanyika hapo awali, lakini jambo hilo lilikuwa halipewi msukumo kwa kiwango cha juu.
Pamoja na hayo, fahamu kwamba licha ya kuwapo kwa mwelekeo wa njia chanya kwa baadhi ya biashara, pia zipo zile ambazo zimelazimika kwenda mlama kutokana na kukosekana kwa walaji au watumiaji wa bidhaa hizo.
Hilo utaliona hata ukipitia kwenye baadhi ya programu tumishi, maarufu APPs mbalimbali zinazojihusisha na biashara na utoaji wa huduma nyingine muhimu.
Pia zipo biashara au huduma nyingine ambazo zimepewa msukomo mkubwa zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Mfano ukiangalia baadhi ya biashara zilizoanguka utabaini ni biashara za usafiri, hii ikiwa ni pamoja na usafiri maarufu wa mtandao mfano kama Uber, Taxi na nyingine zanye kufanana na hizi ni kama zimekwama.
Hii ni kwa sababu katika kipindi cha miezi kadhaa, dunia imekuwa imesimama kutokana na janga la corona hivyo, maana yake ni kwamba hakuna mtu mwenye uwezo tena wa kutumia usafiri huu kama ilivyokuwa awali.
Kwa kiwango cha juu aina ya usafiri kama huu umekuwa ukitumiwa na abiria wanaosafiri kwa ndege kwa maana ya kutoka au kwenda uwanja wa ndege (Airports) hivyo, ujio wa janga la corona ni kama umetia ganzi kwenye aina hii ya usafiri kwani hakuna ndege zinazoruka zaidi ya zile za ndani kwa hapa nchini.
Hili analidhihirisha hata Othman Mohamed (39), dereva taksi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Terminal II, aambaye anakiri kwamba hali imekuwa mbaya ikilinganishwa na mwanzoni mwa mwaka au mwaka jana.
Anasema hii linatokana na kukosekana kwa abiria wa kutosha, hatua ambayo imewalazimu baadhi yao kutafuta maeneo mengine ya kufanya biashara hiyo huku wengine wakiegesha kabisa.
“Unajua ndugu yangu hakuna sekta ambayo haijayumba kutokana na corona, ndiyo maana utaona kwamba awali kabla ndege za kimataifa hazijapigwa marufuku taksi zilikuwa zimejaa hapa, lakini baada tu ya kuzuia ndege za nje kutua ndiyo maana utaona kwamba baadhi wamepaki magari huku wengine wakihamisha vijiwe.
“Lazima nikiri kwamba abiria wa kimataifa walikuwa wanatusaidia ndiyo sababu ulikuwa unaona huku magari yamefurika, ila baada ya janga hili unaona kabisa hali imekuwa tete, unadhani mtafukuzana na abiria wa ndani tu hawa kuanzia madereva wa terminal I, II na III mtaambulia nini sasa.
“Hivyo, tuliobaki ni wabishi tu kama sisi ambao tunasema lazima tukasake mkate wa kila siku ili familia ziweze kula kwa kuwa ndiyo kazi tuliyoichagua, ila kiukweli wengi wetu wamesitisha,” anabaisha Mohammed.
Aidha, anasema pamoja na kwamba ndege za ndani zinafanyakazi lakini kiwango cha abiria wanaosafiri nacho kimepungua huku akiwa na matarajio ya kuona hali ya kawaida ikianza kurejea siku za usoni.
“Kama unavyoona kule ndege zimepaki na zizofanyakazi ni chache, hiyo inaamana kwamba hata abiria wenyewe nao wamepunguza kusafiri. Najua wewe ni mwandishi wa habari utakuwa umesikia kwamba baadhi ya watu wamesafiri kwenda mikoani, nyumbani kwao kwa kuhisi Dar es Salaam nako kungeathirika kama miji mingine mikubwa duniani na janga hili la corona, lakini jambo la kushukuru Mungu, amesimama nasi hatari siyo kubwa.
“Tunaamini kwamba mambo yatatatulia siku za usoni maana tumesikia kwenye mataifa mengine huko kwamba wameanza kuachiwa kwa masharti, hivyo tafsiri ya hii ni kwamba itafika sehemu hata ndege zitaanza kufanyakazi kwa kuwa hili ni janga ambalo huenda lisiishe sasahivi, hivyo maisha lazima yaendelee,” anasema Mohammed.
Wakati unafikiria kwamba sekta ya kina Mohamed imeathirika zaidi, hebu chukua muda kufikiria wafanyakazi na mawakala wa tiketi za safari hasa zile za ndege, unadhani ni kwa kiwango gani watakuwa wanapitia misukosuko?
Ukiacha kuathirika huko kwa huduma za usafiri, kuna sekta za nyumba za biashara ambazo nazo ni kama zimekuwa kwenye wakati mgumu kwa kiwango cha juu.
Ukibahatika kukutana na baadhi ya wamiliki wa nyumba watakwambia kuwa maisha yamekuwa magumu kwakuwa nyumba zao zimekosa wapangaji kwa muda sasa, hata waliopo wanadai hawana fedha hivyo changamoto iko palepale. Hao ni wale wanaopangia nyumba za flemu za biashara je, umewafikiria wale wanaouza nyumba zenyewe?
Kama tunavyofahamu, Waswalihi wanasema kufa kufaana, ndiyo! Pamoja na kuwapo kwa biashara hizo hapo juu ambazo zimepitia shubiri lakini zipo zile ambazo janga hili ni kama limetoa mwanya zaidi kwa biashara hizo kukua.
Baadhi ya biashara hizo ni pamoja na zile za chakula ambazo zinakwenda sambamba na kuchanua kwa soko la mitandao ya kijamii au unaweza kusema biashara mtandao.
Pamoja na kwamba Tanzania Mungu ametusaidia hatukukaa karantini, lakini ukweli ni kwamba wapo wale ambao walikuwa au wanaendelea kuagiza chakula.
Hatua hii imefanya biashara ya chakula kuendelea kuwa muhimu na kuongeza zaidi ubunifu kwa ajili ya kuhakikisha inawafikia wateja kwa wingi hata hivyo, jambo la kusikitisha kwenye hili ni kwamba migahawa mikubwa na wafanyabiashara wenye uwezo ndiyo walioweza kuikamata fursa hii kwa kiwango cha juu huku wakipewa nguvu na uwezo na mitandao ya kijamii katika kuongeza wateja wa huduma zao.
Hivyo, kila jiji kubwa utakalotembelea iwe ni Tanzania utakutana na utaratibu huu ambao corona ni kama umeuongezea kazi zaidi.
Elpidius Mpanju, ni Mkurugenzi Mtandaji wa Mgahawa maarufu wa Kijiji Bar and Grill uliopo katikati ya Jiji la Mwanza, Magharibi mwa Tanzania, ambaye anakiri kuwa kutokana na kuwapo kwa janga la corona amewweza kulitumia vyema jukwaa la kupeleka chakula kwa wateja wake huku wakipewa nguvu na mitandao ya kijamii.
“Kiukweli tulivyoona janga hili limefika na wateja wetu kupungua kwa kiwango kikubwa tuliona hapa kuna haja ya kufanya kila linalowezekana kuhakikisha tunaishinda hii corona kwa kuwapa wateja wetu huduma.
“Hivyo, tulianzisha utaratibu wa kuwapelekea wateja chakula majumbani ambao wao wanalipia nusu ya gharama na nusu nyingine inakuwa juu yetu, tunashukuru kwamba mapokeo haya ya njia mbadala yamekuwa ni makubwa ukizingatia kwamba Jiji la Mwanza siyo kubwa ikilinganishwa na Dar es Salaam hivyo, ni rahisi kufika kila mahali,” anasema Mpanju.
Pamoja na hayo, Mpanju naye ni miongoni mwa walioathirika na janga hili la corona kwani amelazimika kupunguza nusu ya wafanyakazi wake, huku akitoa siri kwa wafanyabiashara wengine kuwa wabunifu licha ya kuwapo kwa Covid-19.
“Awali, nilikuwa na wafanyakazi 52 lakini baada ya janga hili kuja na wateja kukimbia nililazimika kupunguza nusu ya wafanyakazi, sasa hivi ninao 26 pekee, lakini tunaangalia namna gani tunaweza kujiimarisha hapo baadaye.
“Jambo ninaloweza kuwashauri wenzangu na wafanyabiashara kwa ujumla ni kuacha kufanyabiashara ya mazoea, tunapaswa kuwa wabunifu zaidi licha ya janga hili, mfano sisi tayari tulishatengeneza program tumishi (Apps), lakini hatujaizindua, pia watumie vyema mitandao ya kijamii ndiyo maana utaona hata sisi uwapo wetu kwenye Instagram, Facebook au Twitter, imetusaidia kuongeza idadi ya wateja hivyo, niwaombe wenzangu kuiona fursa hii,” anasema Mpanju.
Hakuna asiye fahamu kuwa jukwaa hili la mitandao ya kijamii limeendelea kuwa maarufu zaidi kwani hili linatoa mwanya hata kwa mtu aliyeko karantini kokote duniani kuweza kuangalia kile unachokitangaza au kukiweka kigezo kikubwa ni yeye kuwa rafiki yako.
Hiyo ndiyo imekuwa hata sababu ya wasichana na wanawake wengi kulitumika katika kutangaza bidhaa zao zikiwamo mavazi, vitenge na aina nyingine ya bidhaa ambazo wao pia wamekuwa mashuhuda kwa kusema kwamba zimeweza kuwalipa kwa kiwango cha juu huku kigezo kikubwa kikiwa ni uaminifu na kuuza bidhaa halisi.
“Ni bayana kwamba fursa hii ya kutangaza bidhaa mtandaoni imeniongezea wateja wengi tofauti na vile nilivyokuwa nauza dukani, japo sharti la wateja wa huku ni kwamba lazima uweke bidhaa halisi siyo unaweka picha zenye kupendeza lakini mtu akija kuangalia uhalisia inakuwa ni vitu viwili tofauti.
“Hatua hii imefanya wengi kuwakwaza wateja na hata kughairi kununua bidhaa zao, hivyo kwangu mimi jukwaa hili naliheshimu zaidi kuliko hata duka kwa kuwa kila kukicha fursa zake zinazidi kuongezeka hatua ambayo imeimarisha mtaji wangu zaidi ya mara tatu licha ya janga hili la corona.
“Jambo la msingi tu ni kuwa mwaminifu kwa mteja ukizingatia kwamba wateja wengi hawa wa mitandaoni wanahitaji kutumiwa bidhaa zao, lakini tunajitahidi kufanya hivyo licha ya kuwapo kwa wachache wanaotuharibia kwa kuuza bidhaa feki.
“Lakini huku nako kuna madhira yake, kwani unaweza kukubalina na mteja kuwa unampelekea bidhaa kisha ukafika eneo la tukio simu yake ikawa haipatikani na hamfahamiani bali mmekutana tu mtandaoni,” anasema Esther Mnyika anayejishughulisha na biashara ya mtandao.
Sambamba na bishara hii ya mtandao kuchukua nafasi wakati huu, pia tunameona namna ambavyo huduma za afya kwa njia ya mtandao zilivyoimarika hususan katika janga hili la corona ambapo kwasasa ukiingia mtandaoni utakuta kila aina ya huduma za afya pamoja na majina ya vituo husika vya afya ambapo wengi wanakiri kusaidia na mbinu hii ya maisha.
Hivyo, hii inatoa tafsri ya kwamba simu ya mkononi kwasasa ndiyo zimeshika maisha ya watu wengi zaidi kwa maana iwe ni nyanja ya biashara au nyingine.