24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

CHINA WAFANIKIWA KUPANDIKIZA KICHWA CHA MTU KATIKA MWILI TOFAUTI

Joseph Hiza na Mashirika


NINI kinatokea wakati  mtu anapochinjwa kichwa kisha kuunganishwa katika mwili wa mtu mwingine?

Je, hilo linawezekana? Ina maana iwapo inawezekana baadhi ya binadamu watakaopendezwa na kitendo hicho kinachojaribu kushindana na kazi ya Muumba watarajie kuishi milele kwa kubadilisha vichwa na miili yenye ujana kila ile ya awali inapozeeka?

Kama ndiyo inawezekana, kama anavyodai Profesa Sergio Canavero, vipi kuhusu roho? Je, roho nayo itahamishwa kwenda mwili wa binadamu mwingine?

Ni maswali yanayowakanganya wengi baada ya Dk. Canavero kuitangazia dunia kufanikiwa kwa ahadi aliyoitoa mwaka jana, kuwa kama walivyoahidi wamefanikiwa kupandikiza kichwa cha binadamu katika mwili wa maiti nchini China.

Awali daktari huyo mwenye utata raia wa Italia, aliishitua dunia mwaka jana wakati alipotangaza kuwa upandikizaji huo unawezekana na utafanyika kabla ya mwaka 2017 kuisha, ahadi ambayo ni kama imetimia vile.

Wakati wa operesheni hiyo ya saa 18 nchini China, wataalamu walionesha namna inavyowezekana kuunganisha tena uti wa mgongo, neva na mishipa ya damu ya kichwa kilichokatwa.

Profesa Canavero, ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi ya masuala ya ubongo ya Turin Advanced Neuromodulation ya Italia, alitoa taarifa hiyo ya kushtusha kuhusu mafanikio hayo katika mkutano na wanahabari mjini Vienna, Austria asubuhi ya mapema wiki hii.

Mchakato ulifanywa na timu iliyoongozwa na Dk. Xiaoping Ren, ambaye mwaka jana alipandikiza kichwa katika mwili wa nyani.

Kufuatia mafanikio kwa jaribio la kupandikiza katika mwili wa maiti, kwa sasa hatua inayofuata ni kupandikiza kichwa kwa binadamu hai.

Ripoti kamili ya mchakato wa timu hiyo ya Chuo Kikuu cha Harbin Medical na ratiba ya kupandikiza kichwa binadamu hai inatarajia kutolewa siku chache zijazo.

Akizungumza na wanahabari, Professa Canavero alisema: “Kwa muda mrefu ulimwengu umedhihirisha kanuni yake kwetu.

“Tunazaliwa, tunakua, tunazeeka na tunakufa. Kwa mamilioni ya miaka binadamu walivyobadilika wanadamu bilioni 110 wamekufa katika mchakato huo.

“Tumefikia umri ambao turudishe hatima yetu mikononi mwetu,” alisema.

“Itabadili kila kitu, itakubadili katika kila ngazi.Upandikizaji kichwa cha mwanadamu tayari unawezekana.”

“Upandikizaji huu ulidumu kwa saa 18. Taarifa ya kina itatolewa ndani ya siku chache zijazo,” anaahidi.

“Kila mtu anasema haiwezekani, lakini operesheni imefanikiwa.”

Professa Canavero aliongeza kuwa hatua inayofuata kwa timu hiyo ni kubadili kichwa kizima bana ya binadamu watakatoa viungo vya ubongo.

Alipoulizwa iwapo mipango ya sasa ya kupandikiza katika binadamu hai itafanyika kote duniani baada ya majaribio ya awali nchini China, Professor Canavero alisema: “Kutokana na kiwango cha ukosoaji tulichopokea, sidhani kama hii itawezekana si kila nchi watakubali hili.”

Hiyo imekuja kutokana na operesheni hiyo kukosolewa vikali na ulimwengu wa tiba duniani, ikielezwa kuwa uvumbuzi huo hauna uhalisia, hauwezekani na ni kinyume na maadili ya taaluma ya udaktari.

Dk. James Fildes, Mtafiti Mkuu wa Sayansi katika Shirika la Taifa la Huduma ya Afya ya Umma Uingereza (NHS), katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Upandikizaji cha South Manchester nchini Uingereza anasema: “Bila Canavero au Ren (Dk. Xiaoping) kuwa na ushahidi wa kweli kuwa anaweza kufanya upandikizaji wa kichwa kwa ufasaha na kufanya mwili ufanye kazi kikamilifu, mradi huu mzima kimaadili si sahihi.

Naye Dk. Hunt Batjer, rais mteule wa Chama cha Mabingwa wa Upasuaji wa Masuala ya Ubongo nchini Marekani aliliambia Shirika la Habari Marekani (CNN).

“Nisingependa hili kufanyika kwa mtu yeyote. Nisingeruhusu yeyote kunifanyia kwa sababu kuna mengi mabaya zaidi ya kifo.”

“Kama mtaalamu wa masuala ya kichwa na ubongo napenda kila mtu afahamu kuwa si mimi wala wenzangu wanaodhani kuwa kuchinja watu kwa ajili ya majaribio mafupi kunakubalika. Haikubaliki kabisa,” alisema.

Lakini Profesa Canavero anasema uhakika wa asilimia 90 ina maana kuwa mgonjwa atainuka bila kuwa na madhara yoyote na ataweza kutembea katika muda wa mwezi mmoja.

Kwa sasa anasema lengo lake ni kuleta matumaini kwa watu waliovunjwa moyo na madawa ya mataifa ya magharibi pamoja na watu wenye miili yenye maradhi au kasoro inayowaletea mateso.

Licha ya hatari kubwa katika upasuaji huo, Dk. Canavero anasema amepata watu wengi waliojitolea kufanyiwa upandikizaji huo.

Miongoni mwao ni Valery Spiridonov  (31), anayeugua tatizo la kulika kwa misuli, lililomsababisha kuishia kwenye kiti cha magurudumu.

Akizungumza kwenye Kituo cha Televisheni cha ITV Uingereza, mwaka jana mtaalamu huyo wa kompyuta raia wa Urusi alisema yuko radhi kichwa chake kipandikizwe kwenye mwili tofauti.

“Maisha yangu ni magumu, na ninategemea mno watu kunisaidia kila siku, wakati mwingine hata mara mbili kwa siku, kwasababu nahitaji mtu anitoe kitandani, na aniweke kwenye kiti.”

“Inanifanya ninategemea watu kwa sana.Iwapo kuna namna ya kulibadili hili, naamini tunapaswa kujaribu na kuitumia njia hiyo,” anasema.

Hata hivyo, matumaini ya Spiridonov kuwa mtu wa kwanza kupandikizwa kichwa kwa sasa yamepotea.

Ni kwa sababau inaonekana mtu wa kwanza atatokea China, ambako jaribio la kupandikiza kichwa katika maiti linaelezwa kufanikiwa. Mbaya zaidi nchini humo, ambako suala hilo linaonekana kupokelewa, kumejitokeza idadi kubwa ya watu wanaotaka kufanyiwa majaribio.

Vipi upandikizaji wa kichwa utakavyofanikishwa?

Professa Canavero anadai upandikizaji huo utahitaji wahudumu 150 na saa hadi 36 kufanya upasuaji huo.

Anasema hatua ya kwanza itakuwa ni kukigandisha kichwa cha binadamu hai na mwili wa binadamu ili kuzuia usife.

Baada ya hapo shingo itakatwa na mipira kuunganishwa na mishipa tofauti ya mwili.

Kisha inafuata sehemu iliyo ngumu zaidi, kuukata uti wa mgongo. Utakatwa na kisu maalum kilichotengenezwa kwa almasi kutokana na nguvu za jiwe hilo.

Baadaye kichwa kinaunganishwana mwili na uti wa mgongo unashikanishwa pamoja kwa gundi maalumu.

Misuli, mishipa na sehemu za ndani ya mwili zinarudishwa na ngozi inashonwa upya.

Profesa Canavero anasema kutakuwa na majaribio kwa watu waliojitolea walio na ubongo usio fanya kazi.

Majaribio hayo ya binadamu yanafuatia kufanikiwa kwa yale ya panya, ambayo yaliwapa kiburi akina Canavero kugeukia wanadamu wafu sasa wanalenga wanadamu walio hai.

Mei mwaka jana, wanasayansi waliendesha upandikizaji wa kichwa cha panya kama sehemu ya jaribio hilo kuelekea upandikizaji tata kwa binadamu.

Panya watatu waliotumika katika jaribio lililofaulu kupandikiza kichwa

Watafiti walitumia panya watatu kwa kila operesheni: panya mdogo, kuwa mtoaji, na panya wakubwa wawili, mmoja akiwa kwa ajili ya kutolea damu na mwingine mpokeaji wa kichwa na damu.

Ili kuendeleza mtiririko wa damu katika ubongo, waliunganisha mishipa ya damu kutoka panya kwenda mishipa ya damu inayosambaza damu kwenda moyo katika panya wa tatu kwa kutumia bomba la silicon.

Kisha, mara kichwa kikapachikwa katika mwili wa panya wa pili, watafiti walitumia gundi kuunganisha mishipa na uti wa mgongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles