Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitashiriki uchaguzi mdogo wa udiwani na ubunge, ukiwamo wa Jimbo la Liwale na udiwani kwenye kata 37 uliotangazwa hivi karibuni, kwa kile walichodai kuwapo uvunjifu wa sheria wakati wa uchaguzi huo.
Kimesema kwa sasa kinaelekeza nguvu katika kujijenga, ikiwamo kufanya mabadiliko ndani ya chama kwa kuanzisha operesheni maalumu nchi nzima.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, wakati akiwasilisha uamuzi wa Kamati Ndogo ya Kamati Kuu iliyokutana juzi kutafakati yaliyotokea kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Ukonga, Monduli na kata 23 uliofanyika Septemba 16.
Wakati Mbowe akisema hayo, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, kupitia ukurasa wake wa Twitter aliwakejeli wapinzani wao hao akitaka waseme wamesalimu amri na kuacha visingizio.
“Mbowe anasema wanasusia chaguzi zijazo kwa sababu CCM wamekwenda kuchukua fomu Chadema ili wakagombee kwa tiketi ya Chadema. Duh! Ama kweli kwa visingizio wenzetu wamezidi. Kumbe na Asia (Msangi) wa Ukonga (aliyegombea ubunge Jimbo la Ukonga) ni CCM aliyegombea kwa tiketi ya CDM? Kwakweli najifunza kila siku siasa za upinzani.
“Mbowe anasema wanasusia uchaguzi kama sehemu ya mkakati wa kujipanga upya na akasema “retreat is not surrender”. Kumbe ni mkakati wa kukimbia chaguzi ili mkajipange, clear, msilete visingizio. Mngesema tu, tunaomba ‘Poo’ tungeelewa na sio kusema vyama vyote ni CCM isipokuwa CDM,” alisema.
KAULI YA MBOWE
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema uchaguzi mdogo wa Septemba 16 uligubikwa na ubakaji wa demokrasia, ikiwamo wakurugenzi kutumika kukwamisha urudishaji fomu kwa wagombea.
Alisema wakurugenzi hao walichangia kuzuia mawakala katika vituo vya kupigia kura na watendaji wa Serikali kutumika kwenye kampeni na kutoa ahadi za maendeleo kwa wananchi wa maeneo ulipofanyika uchaguzi.
“Tumevumilia na kushiriki chaguzi hizi katika mazingira magumu na maumivu makubwa sana, tumelalamika na kunung’unika sana, tukajitia moyo kwamba tuendelee tu kushiriki pengine busara itaonekana mahali… tunaendelea kujifunza.
“Katika kujifunza mambo kadha wa kadha ya kufanya tukajiuliza je, tuendelee kushiriki chaguzi hizi zilizotangazwa ambazo figisu zimeshaanza?
“Mfano kule Bukoba wagombea wanaoitwa wa Chadema wameshachukua fomu kwenye kata ili watakapokwenda wagombea rasmi wa Chadema waseme fomu zimeshachukuliwa.
“Sasa kutokana na haya yanayoendelea chama kupitia Kamati Ndogo ya Kamati Kuu, kimeazimia kuwa hatutashiriki chaguzi zote ndogo ikiwa ni pamoja na hizi zilizotangazwa, ikiwamo Liwale na kata 37.
“Hivi sasa tunaendelea kufanya mashauriano na viongozi wetu katika ngazi mbalimbali za wanachama wetu, kwamba ni hatua gani za ziada zitakazochukuliwa,” alisema.
Pia alisema jopo la wanasheria wa chama na walio katika taasisi mbalimbali wataendelea kufungua kesi ya kikatiba kupinga mfumo mzima wa uchaguzi katika mahakama mbalimbali, ikiwamo Mahakama Kuu ya Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika.
“Kuna mambo mbalimbali ya jinai za kikatiba kuhusu uvunjifu wa sheria uliofanywa na viongozi wa Serikali, Tume ya Uchaguzi na CCM, wanasheria wetu katika hatua za awali ‘wamesha-draft’ mashtaka kadhaa ili kufungua kesi katika mahakama hizo kupinga mfumo mzima wa uchaguzi.
“Nimezungumza na viongozi wa NEC kuwa wao ndio wanaosimamia uchaguzi? Wakanijibu ndiyo wanasimamia… Nikawaambia wakurugenzi wote wanaosimamia uchaguzi ni CCM, lakini Jaji Kaijage (Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage) hajui Mkurugenzi (Dk. Athumani Kihamia) yeye ndiye anayesuka na kubariki haya yanayoendelea kwenye uchaguzi,” alisema.
Alisema katika Jimbo la Ukonga kulikuwa na vituo feki 16 vyenye wapigakura zaidi ya 7,000.
“Hili tulilalamikia kwa msimamizi wa uchaguzi na mkurugenzi wa tume makao makuu, lakini wote walitia pamba masikioni kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya kuingizia kura za wizi.
“Kwa tathimini yetu kama chama, Jimbo la Ukonga waliopiga kura hawakuzidi 30,000 lakini walionyesha wapigakura ni 88,000.
“Kuna vyama vya upinzani ambavyo ni sehemu au matawi ya CCM vilikuwa na mawakala ambao nao waliingia vituoni kwa kuingizwa na CCM pamoja na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.
“Walishiriki kupiga kura na kuzijaza kwenye masanduku wakati bado mawakala wa vyama halisi vya upinzani hawajaruhusiwa kuingia vituoni.
“Kwa mfano katika Jimbo la Ukonga kwenye kituo cha QT2 wapigakura walikuwa 433, waliopiga kura ni 25, kati ya hao CCM ilipata kura 12 na Chadema ilipata kura 13 hizi ndizo kura halisi.
“Kituo kingine cha Kiwanja cha Shule QTB5 wapigakura walikuwa 433, waliopiga ni 23, CCM ilipata kura 11 na Chadema kura 12.
“Kituo cha Viwanja vya Wazi Efatha A2 wapigakura 553, waliopiga 54, CCM kura 18, Chadema kura 36. Sasa tunajiuliza uhalali wa uchaguzi huu uko wapi kama idadi ya wanaoshiriki ni chache hivi?
“Vituo ambavyo vina miujiza ambavyo mawakala wetu walizuiwa, mfano kituo cha Mai Mai Nursery School namba 2, idadi ya wapigakura ni 431, waliopiga kura 309, CCM kura 301 na Chadema kura 7,” alisema Mbowe.
Alisema wakurugenzi wamekuwa wakitumika kuhakikisha wagombea wa chama tawala wanapita bila kupingwa.
“Walikuwa wanafunga milango wanaondoka, muda ukiisha wanatangaza mgombea wa Chadema hakurudisha fomu hivyo wa CCM amepita bila kupingwa, nadhani mlishuhudia kwenye Jimbo la Korogwe namna mgombea wetu alivyofanywa na baadaye wa CCM akapita bila kupingwa.
“Wanashiriki kuvunja sheria bila kujali chochote kabisa, Ukonga leo wana mwakilishi ambaye si chaguo lao.
“Mchakato wa uchaguzi ni wa raia na si kijeshi, lakini leo uchaguzi unapofanyika utaona namna magari ya polisi yalivyojaza na silaha kwenye vituo vya kupigia kura,” alisema Mbowe.
Alisema badala ya kuendelea kushiriki kwenye uchaguzi wa namna hiyo, chama kimeona ni vema kikaelekeza nguvu kwa kuanza operesheni maalumu nchi nzima kujenga mtandao kamili na uchaguzi ndani ya chama.
Pia alisema hivi karibuni watazindua sera mpya ya chama ili wanachama na Watanzania wajue Chadema inasimamia nini.
“Uamuzi huu tumeuchukua kwa umakini sana, ‘ku-retreat’ si ‘ku-surrender’ bali ni mkakati wa kivita wa namna ya kujipanga.
“Tunakwenda kufanya mabadiliko ndani ya chama, tunakwenda kujijenga na hatuwezi kushiriki wakati tunaonewa na sheria hazifuatwi,” alisema.
Pia alisema kuna mambo ya kibatili yalifanyika kwenye uchaguzi, watendaji wa Serikali wakitoa matamko na kutoa ahadi kwa wananchi wakati wa kampeni wakitumia magari ya Serikali.
“Tumewaona Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Wakuu wa Wilaya, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na wengine wengi wakifanya kampeni wakati ni watendaji wa Serikali,” alisema Mbowe.
WITO WA KUJIUZULU
Akizungumzia kuhusu kuwapo kwa shiniko la kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho, Mbowe alisema hataondoka kwenye nafasi hiyo kwa kelele za CCM bali waliomchagua ndio wana wajibu wa kumwondoa.
“Siwezi kuondoka kwa kuambiwa na watu wa CCM bali nitaondoka nikiambiwa na wanachama walioniweka tena kwa kushangilia, lakini kamwe sitakipigia magoti CCM kwa sababu lengo lao ni kunidhoofisha.
“Kila anayetoka na kuhamia CCM anasema wanamwambia wanitaje mimi eti tumeshindwa kwa sababu mimi ni mwenyekiti, kwani Mbowe alikwenda kupiga kura Monduli au Ukonga?
“Kazi ya kuwa kiongozi wa chama si nyepesi ni ya ujasiri na utume wenye misalaba ambayo si kila mtu anaweza kuibeba,”alisema.
Akizungumzia kuhusu wabunge na madiwani wa Chadema kuhamia CCM, alisema kelele za nani anaondoka haziwatoi kwenye reli kwa sababu ni maelfu wanaingia ndani ya chama hicho na kwamba watawaibua utakapofika uchaguzi mkuu.